Sheria na Kuzuia Uhalifu

UM imeshtumu mauaji ya ukabila ya raia wa Nigeria katika Ukraine

Jennifer Pagonis, Msemaji wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) Ijumanne aliripoti kwa waandishi habari mjini Geneva kuwa wamepokea taarifa zenye kuelezea mauaji ya raia mmoja wa Nigeria katika mji wa Kyiv, Ukraine, mnamo tarehe 29 Mei, mauaji ambayo UNHCR inaamini yalikuwa ya kikabila:~

Baraza Kuu linajadilia biashara haramu ya kutorosha watu

Baraza Kuu la UM Ijumanne lilifanyisha kikao maalumu kujadilia tatizo la kudhibiti biashara haramu ya kuvusha watu, kwa ajira isiokubalika kisheria, ambayo sasa hivi inaendelezwa na kupaliliwa kimataifa.

Mkariri wa masuala ya ubaguzi ashtumu mashambulio ya wageni Afrika Kusini

Doudou Dienne, Mkariri Maalumu wa UM anayehusika na masuala ya ukabila, ubaguzi wa rangi wa kisasa, chuki za wageni wa nchi na utovu wa ustahamilivu, leo amewasilisha taarifa maalumu yenye kuelezea huzuni alionayo kuhusu kiwango kilichofurutu ada cha yale mashambulio ya chuki yaliofanyika Afrika Kusini karibuni, dhidi ya wahamiaji wa mataifa jirani, na pia dhidi ya kundi la makabila madogo ya wahamiaji yaliopo nchini, hujuma ambazo alisema ziliendelezwa mjini Johannesburg na vile vile kwenye vitongoji jirani, na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 40 na majeruhi kadha.

UM imeanzisha uchunguzi wa udhalilishaji wa kijinsia katika JKK

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) limeripoti Ofisi ya Uchunguzi ya UM (OIOS) imeanzisha upelelezi maalumu wa kufuatilia madai ya kwamba wanajeshi fulani wa UM kutoka India walishiriki kwenye vitendo haramu vya kuajiri watoto wadogo wa kike na kujamiana nao kwa malipo. Msemaji wa MONUC, Kemal Saiki amenakiliwa akisema vitendo hivi vilidaiwa kutukia kwenye jimbo la vurugu la Kivu Kaskazini.

Idadi ya wakimbizi wa mashua kwa Yemen imezidi mardufu

UNHCR imeripoti kwamba idadi ya wahamiaji wanaotokea maeneo ya Pembe ya Afrika, na ambao huvushwa magendo katika Ghuba ya Aden na kupelekwa kwenye mwambao wa Yemen, imeongezeka kwa mara mbili zaidi kwa mwaka huu.

ICC kutangaza hati rasmi ya kumshika kiongozi wa CNDP katika JKK

Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) imetoa hati rasmi ya kumkamata Bosco Ntaganda, kiongozi wa jeshi la mgambo la CNDP, baada ya kutuhumiwa, katika siku za nyuma, kuwalazimisha watoto wenye umri mdogo kujiunga na kundi lao na kushiriki kwenye mapigano, hasa katika wilaya ya utajiri mkubwa wa maadini ya Ituri, iliopo mashariki ya JKK; na alituhumiwa kurudia vitendo hivyo pia katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Siku ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Rwanda kuheshimiwa Makao Makuu

Leo magharibi, tarehe 07 Aprili KM wa UM Ban Ki-moon atatoa risala maalumu ya kuwakumbuka wale raia walioangamizwa Rwanda miaka 14 iliopita kutokana na jinai ya mauaji ya halaiki. KM anatarajiwa kuikumbusha jumuiya ya kimataifa kuhusu dhamana ya maadili waliokabidhiwa nayo na umma, ya kuunga mkono, kwa kauli moja, juhudi za UM za kuzuia janga karaha la mauaji ya halaiki kuibuka tena ulimwenguni. Kwa mujibu wa takwimu za UM watu 800,000 ziada waliangamia Rwanda na waathiriwa kadha wengineo walionusurika na mauaji walidhurika kiakili. KM ameahidi ya kuwa ataendelea kutumia muda wa utumishi wake katika UM kuhakikisha walimwengu tunafanikiwa kuuzuia milele hatari ya mauaji ya halaiki kuibuka tena duniani.

BINUB kulaani hujuma za waajiriwa wenyeji dhidi ya ofisi ya UM Burundi

Ofisi ya UM Inayofungamanisha Huduma za Amani na Maendeleo Burundi (BINUB) imelaani vikali mashambulio yaliofanyika karibuni dhidi ya watumishi wake na kuendelezwa waajiriwa wenyeji waliokuwa wakitumikia shirika jengine la UM la ulinzi wa amani Burundi la ONUB, katika miaka ya 2004 hadi 2006.

Makao Makuu yawakumbuka na kuwaheshimu waathiriwa wa utumwa

Kuanzia Ijumanne ya leo, tarehe 25 Machi, UM umeanzisha taadhima za karibu wiki moja za kuwakumbuka waathiriwa wa janga la utumwa pamoja na kuadhimisha siku Biashara ya Utumwa kwenye ngambo ya Bahari ya Atlantiki ilipositishwa na Marekani miaka mia mbili iliopita.

Bukini imetia sahihi ya kuridhia Mkataba wa Roma

Mapema wiki hii taifa la Bukini limetia sahihi ya kuridhia Mkataba wa Roma, ambao ndio ulioanzisha Mahakama ya Kimataifa ya ICC. Mahakama ya ICC ni mahakama huru na ya kudumu, iliyodhaminiwa na jumuiya ya kimataifa madaraka ya kuhukumu wale watu waliotuhumiwa kufanya makosa mabaya ya jinai, mathalan, mauaji ya halaiki, jinai ya vita na vile vile yale makosa ya uhalifu dhidi ya utu.