Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mkariri wa masuala ya ubaguzi ashtumu mashambulio ya wageni Afrika Kusini

Doudou Dienne, Mkariri Maalumu wa UM anayehusika na masuala ya ukabila, ubaguzi wa rangi wa kisasa, chuki za wageni wa nchi na utovu wa ustahamilivu, leo amewasilisha taarifa maalumu yenye kuelezea huzuni alionayo kuhusu kiwango kilichofurutu ada cha yale mashambulio ya chuki yaliofanyika Afrika Kusini karibuni, dhidi ya wahamiaji wa mataifa jirani, na pia dhidi ya kundi la makabila madogo ya wahamiaji yaliopo nchini, hujuma ambazo alisema ziliendelezwa mjini Johannesburg na vile vile kwenye vitongoji jirani, na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 40 na majeruhi kadha.

UM imeanzisha uchunguzi wa udhalilishaji wa kijinsia katika JKK

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) limeripoti Ofisi ya Uchunguzi ya UM (OIOS) imeanzisha upelelezi maalumu wa kufuatilia madai ya kwamba wanajeshi fulani wa UM kutoka India walishiriki kwenye vitendo haramu vya kuajiri watoto wadogo wa kike na kujamiana nao kwa malipo. Msemaji wa MONUC, Kemal Saiki amenakiliwa akisema vitendo hivi vilidaiwa kutukia kwenye jimbo la vurugu la Kivu Kaskazini.

Idadi ya wakimbizi wa mashua kwa Yemen imezidi mardufu

UNHCR imeripoti kwamba idadi ya wahamiaji wanaotokea maeneo ya Pembe ya Afrika, na ambao huvushwa magendo katika Ghuba ya Aden na kupelekwa kwenye mwambao wa Yemen, imeongezeka kwa mara mbili zaidi kwa mwaka huu.