Sheria na Kuzuia Uhalifu

ICC kutangaza hati rasmi ya kumshika kiongozi wa CNDP katika JKK

Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) imetoa hati rasmi ya kumkamata Bosco Ntaganda, kiongozi wa jeshi la mgambo la CNDP, baada ya kutuhumiwa, katika siku za nyuma, kuwalazimisha watoto wenye umri mdogo kujiunga na kundi lao na kushiriki kwenye mapigano, hasa katika wilaya ya utajiri mkubwa wa maadini ya Ituri, iliopo mashariki ya JKK; na alituhumiwa kurudia vitendo hivyo pia katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Siku ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Rwanda kuheshimiwa Makao Makuu

Leo magharibi, tarehe 07 Aprili KM wa UM Ban Ki-moon atatoa risala maalumu ya kuwakumbuka wale raia walioangamizwa Rwanda miaka 14 iliopita kutokana na jinai ya mauaji ya halaiki. KM anatarajiwa kuikumbusha jumuiya ya kimataifa kuhusu dhamana ya maadili waliokabidhiwa nayo na umma, ya kuunga mkono, kwa kauli moja, juhudi za UM za kuzuia janga karaha la mauaji ya halaiki kuibuka tena ulimwenguni. Kwa mujibu wa takwimu za UM watu 800,000 ziada waliangamia Rwanda na waathiriwa kadha wengineo walionusurika na mauaji walidhurika kiakili. KM ameahidi ya kuwa ataendelea kutumia muda wa utumishi wake katika UM kuhakikisha walimwengu tunafanikiwa kuuzuia milele hatari ya mauaji ya halaiki kuibuka tena duniani.

BINUB kulaani hujuma za waajiriwa wenyeji dhidi ya ofisi ya UM Burundi

Ofisi ya UM Inayofungamanisha Huduma za Amani na Maendeleo Burundi (BINUB) imelaani vikali mashambulio yaliofanyika karibuni dhidi ya watumishi wake na kuendelezwa waajiriwa wenyeji waliokuwa wakitumikia shirika jengine la UM la ulinzi wa amani Burundi la ONUB, katika miaka ya 2004 hadi 2006.