Sheria na Kuzuia Uhalifu

UNESCO imelaani mauaji ya mwandishi habari Usomali

Koichiro Matsuura, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ameshtumu vikali mauaji yaliotukia wiki iliopita nchini Usomali ya Bashir Nor Gedi, mwandishi habari na mkurugenzi wa steshini maarufu ya redio Shabelle iliopo kwenye mji wa Mogadishu. Marehemu Gedi alipigwa risasi mbele ya nyumba yake mnamo tarehe 19 Oktoba na mhalifu asiyejulikana. Matsuura alionya kwamba wauaji wahalifu wanaonuia kufunga midomo ya wanahabari na vyombo vya habari humalizikia kudhoofisha na kutengua haki isiofutika ya umma kuwa na mawazo huru, kufikiri na kuamua wanachotaka bila ya vitisho.

ICC kumtia mbaroni kiongozi wa FRPI, mtuhumiwa wa jinai ya vita DRC

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Halaiki (ICC) imetangaza kumshika na kumweka kizuizini kwenye mji wa Hague, Uholanzi, Germain Katanga, aliyekuwa Kamanda wa kundi la wanamgambo wa FRPI (Force de Resistance Patriotique en Ituri) katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Katanga, mwenye umri wa miaka 29, ametuhumiwa kushiriki kwenye jinai ya vita na makosa yaliotengua haki za kiutu.

WFP imeshtumu mauaji ya madereva wake watatu katika Darfur

Shirika la Miradi ya Maendeleo Duniani (WFP) limetoa ilani yenye kulaani, kwa kauli moja, mauaji ya madereva watatu wa malori waliokodiwa kugawa vyakaula, ambao walipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Darfur. WFP bado haijapokea taarifa yenye kuthibitisha ni makundi gani hasa yalioendeleza jinai hii. Kawaida WFP huajiri madereva wa muda na wasaidizi wao 2,000 katika Darfur, ambao hutumiwa kuhudumia chakula watu milioni tatu, kuwakilisha operesheni kubwa kabisa ya shughuli hizi duniani.