Sheria na Kuzuia Uhalifu

ICTR imeidhinisha hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya M. Muhimana

Korti Ndogo ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) iliopo Arusha, Tanzania imeidhinisha na kuthibitisha tena ile hukumu ya 2005 ya kifungo cha maisha kwa Mikaeli Muhimana aliyetuhumiwa kuendeleza makosa ya jinai dhidi ya utu katika Rwanda mnamo 1994. Miongoni mwa makosa yaliyomtia hatiani Muhimana ni pamoja na kushtakiwa kushiriki kwenye jinai ya mauaji ya halaiki, vitendo vya kunajisi kihorera wanawake wawili na vile vile kumwua mwanamke mwengine mja mzito.

Maofisa wa UM washtumu mauaji ya wanajeshi 4 wa Uganda katika Usomali

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Francois Lonseny Fall ameshtumu vikali mauaji ya wanajeshi 4 wa Uganda wa vikosi vya ulinzi wa amani vya AU, yaliotokea hivi majuzi mjini Mogadishu, Usomali.

Mahakama Maalumu ya Sierra Leone imetangaza tarehe ya kesi ya C. Taylor

Mahakama Maalumu kwa Sierra Leone inayohusika na kesi za jinai ya vita imetangaza rasmi kuwa utaanza kusikiliza kesi ya aliyekuwa Raisi wa Liberia, Charles Taylor mnamo tarehe 04 Juni mwaka huu. Uamuzi huu ulifikiwa kwenye kikao kilichokutana kwenye mji wa Hague, Uholanzi kuandaa taratibu za usikilizaji wa mashtaka. Taylor ametuhumiwa makosa 11 yanayoambatana na makosa ya kushiriki kwenye jinai ya vita pamoja na ukiukaji uliovuka mipaka ya sheria ya kimataifa dhidi ya utu, ikijumuisha mauaji ya halaiki, vitendio vya kunajisi kihorera, ukataji viungo, utumwa wa kijinsia na kuwalazimisha watoto wenye umri mdogo kupigana.

Vikwazo vya almasi Liberia kuondoshwa na Baraza la Usalama

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Liberia, Alan Doss amepongeza uamuzi wa karibuni wa Baraza la Usalama, wa kuondoa vikwazo dhidi ya biashara ya kuuza almasi kutoka taifa hili la Afrika Magharibi.