Sheria na Kuzuia Uhalifu

Asilimia kubwa ya watoto walionyakuliwa Chad wanaishi na wazee

Mashirika ya UM, ikijumuisha lile shirika linalohusika na mfuko wa maendeleo ya watoto, UNICEF na lile linalosimamia huduma za wahamiaji, UNHCR yakichanganyika na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC yameripoti kwa kauli moja ya kuwa wale watoto 103 waliotuhumiwa kuibiwa hivi karibuni nchini Chad, kwa madai walikuwa ni watoto mayatima wanaohitaji familia za kuwatizama kihali na mali imebainika kihakika, baada ya uchunguzi kufanyika na wahudumia misaada ya kiutu kwamba kati ya idadi hiyo watoto 91 walikuwa na wazee wao halali na sio mayatima abadan. Watoto 12 waliosailia sasa hivi wanaendelea kufanyiwa uchunguzi ziada kutafutiwa wazee wao na kuthibitisha kama ni mayatima au la.

UNESCO imelaani mauaji ya mwandishi habari Usomali

Koichiro Matsuura, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ameshtumu vikali mauaji yaliotukia wiki iliopita nchini Usomali ya Bashir Nor Gedi, mwandishi habari na mkurugenzi wa steshini maarufu ya redio Shabelle iliopo kwenye mji wa Mogadishu. Marehemu Gedi alipigwa risasi mbele ya nyumba yake mnamo tarehe 19 Oktoba na mhalifu asiyejulikana. Matsuura alionya kwamba wauaji wahalifu wanaonuia kufunga midomo ya wanahabari na vyombo vya habari humalizikia kudhoofisha na kutengua haki isiofutika ya umma kuwa na mawazo huru, kufikiri na kuamua wanachotaka bila ya vitisho.

ICC kumtia mbaroni kiongozi wa FRPI, mtuhumiwa wa jinai ya vita DRC

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Halaiki (ICC) imetangaza kumshika na kumweka kizuizini kwenye mji wa Hague, Uholanzi, Germain Katanga, aliyekuwa Kamanda wa kundi la wanamgambo wa FRPI (Force de Resistance Patriotique en Ituri) katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Katanga, mwenye umri wa miaka 29, ametuhumiwa kushiriki kwenye jinai ya vita na makosa yaliotengua haki za kiutu.

WFP imeshtumu mauaji ya madereva wake watatu katika Darfur

Shirika la Miradi ya Maendeleo Duniani (WFP) limetoa ilani yenye kulaani, kwa kauli moja, mauaji ya madereva watatu wa malori waliokodiwa kugawa vyakaula, ambao walipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Darfur. WFP bado haijapokea taarifa yenye kuthibitisha ni makundi gani hasa yalioendeleza jinai hii. Kawaida WFP huajiri madereva wa muda na wasaidizi wao 2,000 katika Darfur, ambao hutumiwa kuhudumia chakula watu milioni tatu, kuwakilisha operesheni kubwa kabisa ya shughuli hizi duniani.

Suala la Iran lazonga kikao cha mwaka cha IAEA mjini Vienna

Mnamo Ijumatatu, 17 Septemba (2007) Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Kinyuklia (IAEA)lilianza mijadala ya wawakilishi wote mjini Vienna, Austria kwenye kikao cha mwaka.

ICTR imependekeza kifungo cha muda mrefu kwa aliyekuwa meya Rwanda

Hassan Jallow, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) kwenye hoja za kufunga kesi ya Juvenal Rugambarara, aliyekuwa meya wa Kitongoji cha Bicumbi kuanzia 1993-1994, alipendekeza mtuhumiwa huyo ahukumiwe kifungo cha miaka 12 kwa kushiriki kwenye jinai dhidi ya ubinadamu.

Operesheni za UNMIL kuongezewa muda kukuza amani Liberia

Baraza la Usalama limepitisha azimio la kuendeleza operesheni za shirika la UM la ulinzi wa amani katika Liberia (UNMIL) kwa miezi 12 ziada hadi Septemba 30 2008.

'Jukumu la polisi katika kutunza amani ni lazima litambuliwe': asema Mkuu wa Polisi wa UNMIS

Kai Vittrup, Kamishna wa Polisi wa Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani Sudan (UNMIS) ameliambia Shirika la Habari la UM kwamba Mataifa yote Wanachama ya UM yanawajibika kutambua jukumu muhimu la kazi za polisi wa kimataifa katika uendeshaji wa operesheni za amani za UM. Kamishna Vittrup aliyahimiza Mataifa Wanachama yaridhie pendekezo la kupeleka raia polisi wa vyeo vya juu, katika Darfur kusaidia operesheni zijazo za ulinzi wa amani za UM.

MONUC yajaribu kupatanisha makundi yanayohasimiana DRC

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) inajishirikisha katika jukumu, lisio rasmi, la kujaribu kupatanisha vikosi vya serekali vya FARDC na wafuasi wa Jenerali aliyetoroka jeshi, Laurent Nkunda. Huduma hii inafanyika katika jimbo la kaskazini-mashariki ya nchi.

Mjumbe wa UM kwa tatizo la Uganda kaskazini afanyisha mazungumzo ya amani na viongozi husika

Wiki hii Raisi mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano na pia Mjumbe Maalumu wa KM juu ya mzozo wa sugu wa Uganda kaskazini, ameanza kukutana kwa mazungumzo ya amani na viongozi kadha wa eneo, ikiwa miongoni mwa juhudi za kimataifa za kuwasilisha suluhu ya kudumu kati ya makundi yanayohasimiana, yaani Serekali ya Uganda na kundi la waasi la LRA.