Sheria na Kuzuia Uhalifu

Walimu wa sayansi ya polisi kufunza vikosi vya ulinzi wa amani kwa Darfur

Tangu Ijumatatu, walimu wa kimataifa wa mafunzo ya polisi, wenye vyeo vya juu, wameanzisha mafunzo kwa maelfu ya polisi wa UM juu ya taratibu za kudhibiti bora usalama kwenye mazingira ya vurugu na mapigano. Polisi hawa wanatarajiwa kupelekwa Darfur, Sudan kulinda amani.

KM atoa wito unaohimiza mchango maridhawa kwa vikosi vya UNAMID Darfur

Baada ya kuripoti kwenye kikao cha faragha mbele ya Baraza la Usalama juu ya mizozo iliozuka barani Afrika hivi karibuni, KM Ban Ki-moon alikutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu na aliwaambia kwamba wakati umewadia kwa yale mataifa yalioshadidia kupelekwa vikosi vya ulinzi wa amani Darfur, kutekeleza ahadi ya kuipatia UM zana na vifaa vinavyohitajika haraka kuhudumia operesheni zake katika eneo husika la Sudan, hususan ndege za helikopta na vile vile vifaa vinavyohusikana na huduma za usafiri. Kadhalika KM alisema vikosi mseto vya UM na UA kwa Darfur, au vikosi vya UNAMID vinahitajia kuongezewa wanajeshi ziada haraka iwezekanavyo pamoja na vifaa vya kuendesha shughuli zake kwa mafanikio.

Kiongozi wa waasi Kongo amekamatwa na kupelekwa Mahakama ya ICC Hague

Mathieu Ngudjolo Chui, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) anayedaiwa kuongoza kundi la waasi la National Integrationist Front (FNI) amekamatwa kati ya wiki na kuhamishwa kwenye Mahakama ya Mauaji ya Jinai ya ICC iliopo mjini Hague, Uholanzi. Kwa mujibu wa taarifa ya Bruno Cathala, Msajili wa Mahakama, mnamo Februari 2003 mtuhumiwa Chui anadaiwa aliandaa, na kuongoza mashambulio katili kwenye kijiji cha Bogoro, kilichopo kaskazini-mashariki ya Ituri katika JKK na kusababisha vifo kadha wa kadha kwa watu wasio hatia.

Mtuhumiwa wa jinai ya halaiki Rwanda ajisalimisha kwa ICTR

Leonodis Nshogoza ameripotiwa kujisalimisha, kwa khiyari, mbele ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) iliopo mjini Arusha, Tanzania baada ya kutolewa ilani ya kimataifa ya kumshika. Nshogoza alishtakiwa kushiriki kwenye jinai ya vita Rwanda katika miaka ya tisini. Hivi sasa Nshogoza yupo kizuizini chini ya hifadhi ya Mahakama ya ICTR akisubiri kesi.

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani (UNIFEM) imeihimiza jamii ya kimataifa kuongeza juhudi za kukomesha kihakika, tabia hatari ya kutahiri watoto wa kike. UNIFEM imependekeza kwa nchi wanachama kuheshimu haki za wanawake pamoja na watoto wakike pote duniani, mwito ambao ulitangazwa Februari 7 (08) katika kipindi ambacho walimwengu walikuwa wakiiadhimisha na kuiheshimu Siku ya Kimataifa dhidi ya Ukeketaji wa Wanawake.