Msaada wa Kibinadamu

UM kuomba dola milioni 42 kuhudumia misaada ya kiutu kwa Wakenya 500,000

John Holmes, Mshauri wa UM juu ya Misaada ya Dharura karibuni aliitisha mkutano maalumu na waandishi habari kwenye Makao Makuu mjini New York, na alidhihirisha kwamba machafuko yaliojiri Kenya baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa yaliathiri kihali watu 500,000. Kwa hivyo UM unahitajia kufadhiliwa na wahisani wa kimataifa msaada wa dharura, uliokadiriwa dola milioni 42 kuhudumia misaada ya kiutu na faraja ya kimaisha umma huu ulioathirika na vurugu liliofumka Kenya mwanzo wa mwaka.

UNICEF kuiombea Malawi msaada wa dharura kudhibiti mafuriko

Shirika la UM kuhusu Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF)limetangaza ombi maalumu linaloishinikiza jumuiya ya kimataifa kufadhilia mchango wa dharura wa dola milioni 2.5 kuhudumia chakula ule umma ulioathirika na mafuriko yaliosambaa Malawi. UNICEF imetahadharisha kwenye taarifa yake kwamba pindi ombi lao halitokamilishwa kwa wakati kuna hatari ya watu milioni moja kukabiliwa na njaa maututi katika Malawi.

UM yahudumia misaada ya kiutu kwa waathiriwa wa mafuriko kusini ya Afrika

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) ikishirikiana na jumuiya zisio za kiserekali imo mbioni kuhudumia mataifa ya kusini ya Afrika kupata misaada ya kihali kuwavua makumi elfu ya raia katika Msumbiji, Zambia na Zimbabwe na hatari iliozuka karibuni katika eneo lao, baada ya mvua kali kunyesha nje ya majira ya kawaida na kusababisha Mto Zambezi kufura kwa kasi na kueneza mafuriko.

Utekelezaji wa MDGs Kijijini Mbola, Tanzania - Kilimo na Mazingira (Sehemu ya Pili)

Wasikilizaji, kwenye makala ya kwanza kuhusu huduma za wanavijiji wa Mbola, katika Mkoa wa Tabora, Tanzania za kuyakamilisha yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa wakati, tulikupatieni dokezo na fafanuzi za Kaimu Naibu wa Kilimo na Mazingira, Eliezer N. Kagya ambaye anasimamia utekelezaji wa malengo hayo kwenye eneo husika. Alielezea namna wanavijiji wanavyoshiriki na kushirikishwa kwenye huduma za pamoja za kuondosha njaa kwenye eneo lao, kwa kutumia kilimo cha kisasa. Kwenye sehemu ya pili ya mazungumzo yetu, Kagya anazingatia matokeo ya aina gani yatakayojiri katika mwaka wa pili, kwenye sekta ya kilimo na mazingira, baada ya kuanzishwa mradi huu muhimu wa MDGs wenye lengo la kuondosha njaa na kuimarisha maendeleo ya kuchumi na jamii yatakayokuwana natija kwa wote.

Utekelezaji wa MDGs Kijijini Mbola, Tanzania - Kilimo na Mazingira (Sehemu ya Kwanza)

Mnamo siku za nyuma tulianzisha vipindi maalumu kuhusu juhudi za kizalendo za wenyeji wa kijiji cha Mbola, katika Mkoa wa Tabora, Tanzania za kuharakisha utekelezaji wa ile miradi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ili kuikamilisha kwa wakati, kama ilivyopendekezwa na maafikiano ya jumuiya ya kimataifa katika mwaka 2000. Miradi hii ipo chini ya uongozi wa UM na hufadhiliwa na wahisani mbalimbali wa kutoka sehemu kadha wa kadha duniani.

UM kujumuika na Kenya kudhibiti utulivu na kuhudumia misaada ya kiutu nchini

KM wa UM Ban Ki-moon ameripotiwa kuingiwa na ‘wahka’ mkuu kuhusu ongezeko la hali ya wasiwasi, na mfumko wa vurugu liliotanda karibuni nchini Kenya, kufuatia uchaguzi uliomalizika wiki iliopita. Msemaji wa KM aliripoti kwamba Bw. Ban alishtushwa sana na taarifa alizopokea zilizothibitisha kwamba darzeni za raia waliunguzwa moto majuzi katika mji wa Eldoret walipokuwa ndani ya kanisa. Kadhalika KM aliarifiwa watu mia tatu ziada walishauawa baada ya kufumka ghasia na vurugu kufuatia kumalizika kwa uchaguzi wa taifa na kutangazwa matokeo ambayo hayakuwaridhisha baadhi ya vyama vilivyoshiriki kwenye upigaji kura huo.

Tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya UM zapungua 2007 Liberia

Ripoti ya karibuni ya Shirika la UM juu ya ulinzi wa amani katika Liberia (UNMIL) imethibitisha kwamba shtumu dhidi ya wafanyakazi wa UM, ambao siku za nyuma walidaiwa kuendeleza ukandamizaji na tuhumu za unyanyasaji wa kijinsia, zimeteremka kwa asilimia 80 katika kipindi cha nusu ya pili ya mwaka 2007, tukilinganisha na kipindi hicho hicho katika 2006.

Jimbo la Wasomali wa Ethiopia lakabiliwa na tatizo la njaa

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imearifu ya kuwa hali katika lile eneo la Ethiopia la Ogaedn ambapo huishi raia wenye asili ya Kisomali, linaitia wasiwasi jamii ya kimataifa kwa sababu ya kutanda kwa tatizo la chakula.

Wahajiri wa Burundi kufadhiliwa makazi na UNHCR

Katika miaka mitano iliopita Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limefadhilia makazi wahamiaji 58,000 waliorejea Burundi kutoka matifa jirani na nchi za kigeni, msaada ambao uliowawezesha kujenga nyumba mpya na kupata matumaini ya maisha bora kwa siku zijazo.