Msaada wa Kibinadamu

UM imewapatia waathiriwa wa zilzala Uchina fedha na mahema 11,000

UM umeifadhilia Serikali ya Uchina msaada wa dola milioni 8 kutoka ule Mfuko wa Misaada ya Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF. Msaada huu utakuwa miongoni mwa michango ya kimataifa iliotolewa kuwahudumia kihali waathiriwa wa zilzala iliopiga nchini huko wiki iliopita katika jimbo la kusini la Sichuan, Uchina.

Wahamiaji waliopo Yemen wanaombewa misaada ziada na UNHCR

Kwenye mkutano wa siku mbili uliofanyika kwenye mji wa Sana\'a, Yemen kuzingatia juhudi za kimataifa za kuwapatia hifadhi bora wahamiaji wanaovushwa kimagendo kwenye Ghuba ya Aden kutoka Pembe ya Afrika, kikao ambacho kilikamilisha mijadala yake hii leo, kulitolewa ombi la dharura na Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) Antonio Guterres aliyoitaka jumuiya ya kimataifa kuharakisha, na pia kuongeza mchango wao, unaohitajika kuwasaidia wahamiaji hawa kunusuru maisha.

Huduma za kiutu za UM zaendelea kuokoa waathiriwa wa kimbunga Myanmar

John Holmes, Naibu KM juu ya Misaada ya Dharura na Masuala ya Kiutu leo alioanana na wenye mamlaka nchini Myanmar ambapo aliwaomba wakuu wa Serikali kukuza haraka ushirikiano wao na UM, pamoja na mashirika ya kimataifa, ili waweze kuhudumia misaada ya kiutu kwa watu milioni 2.4 waliodhurika na Kimbunga Nargis.

Maziwa yaliofumwa na zilzala yanahatarisha maisha Sichuan

UM umetangaza kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa wale raia wa Uchina wenye makazi kwenye nyanda za chini, katika jimbo la Sichuan, lilioathirika na zilzala iliopiga huko katika siku za karibuni.

ASEAN kuanzisha tume ya kuharakisha misaada ya kiutu Myanmar

Wajumbe wa Umoja wa Mataifa ya Kusini-Mashariki ya Asia, yaani Umoja wa ASEAN waliokutana Singapore, leo wameafikiana kuanzisha tume maalumu itakayodhaminiwa madaraka ya kurahisisha ugawaji wa misaada ya dharura, ya kihali, kutoka wafadhili wa kimataifa kwa Myanmar, tume ambayo itaongozwa na KM wa Umoja wa ASEAN, kwa madhumuni ya kuondosha wasiwasi wa wenye mamlaka kuhusu dhamira hasa ya michango ya baadhi ya mataifa ambayo huyatafsiri adui. Tume hiyo inatarajiwa kushirikiana, kwa karibu zaidi, na UM katika kuongoza huduma za kiutu nchini Myanmar.

Mkuu wa UNHCR azuru kambi za wahamiaji wa Usomali Yemen

Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) ambaye hivi sasa anafanya ziara rasmi nchini Yemen, aliripotiwa akitoa mwito maalumu kwa wahisani wa kimataifa kufadhilia msaada wa fedha maridhawa,za dharura, kuwahudumia kihali wahamiaji wa Usomali wanaoishi kwenye kambi za muda nchini Yemen, umma ambao ulihajiri makwao kujiepusha na mapigano yalioselelea nchini katika miaka ya karibuni. Mwito huu ulitolewa baada ya Guterres kuzuru Kambi ya Karaza ambapo wahamiaji 10,500 wa Usomali huishi, eneo liliopo kilomita 140 magharibi ya mji wa Aden.

UM bado wakabili vizingiti kwenye huduma za kiutu Myanmar

UM umetangaza Ijumaa kwamba bado unakabiliwa na vizingiti kadha wa kadha katika shughuli zake za kugawa misaada ya kukidhia mahitaji ya kimsingi kwa raia wanaokadiriwa milioni 2.5, walioathirika kihali na mali, kutokana na Kimbunga Nargis kilichopiga nchini humo wiki mbili zilizopita.

IFRC inayaombea Uchina, Myanmar na Ethiopia misaada ya dharura

Shirika la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) Ijumaa, mjini Geneva, limeanzisha kampeni maalumu ya kuchangisha msaada wa fedha zinazohitajiwa kuendeleza shughuli zake kidharura katika Myanmar, Uchina na pia Ethiopia. IFRC iliripoti itahitajia msaada wa dola milioni 20 kuhudumia kihali aila 100,000 walionusurika na zilzala katika Uchina; dola milioni 50 kuusaidia umma uliosibiwa na madhara ya Kimbunga Nargis katika Myanmar; na vile vile dola milioni 1.7 kuhudumia chakula Ethiopia. ~

UM inawapatia lishe bora watoto 44,000 wa Usomali

UM unaendelea kuhudumia kidharura chakula watoto 44,000 waliopo kwenye kambi za wahamiaji wa ndani ya nchi katika Usomali. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) ndilo linaloongoza katika huduma hizi za kuwapatia watoto lishe ya kunusuru maisha, licha ya kuwa wafanyakazi wake hukabiliwa na vizingiti aina kwa aina katika operesheni zao, ikijumuisha upungufu wa usalama na mioundombinu halisi ya kurahisisha kadhia ya kugawa misaada ya kihali kwa mafanikio kwa umma muhitaji.

KM akutana na wawakilishi wa ASEAN kuzingatia Myanmar

KM Ban Ki-moon alimaliza mashauriano muhimu Ijumatano usiku na wawakilishi wa kutoka Mataifa Wanachama wa Umoja wa ASEAN, walio jirani na Myanmar, na vile vile kujumuisha wawakilishi wa yale mataifa wafadhili kuzingatia hali katika Myanmar na kuzingatia hatua za kuchukuliwa, kidharura, kuharakisha misaada maridhawa inayotakikana kunusuru maisha ya umma ulioathirika na Kimbunga Nargis katika Myanmar. Wajumbe hawa waliafikiana kuitisha kikao maalumu mwezi ujao cha kuchangisha msaada unaotakikana kuihudumia Myanmar kufufua tena shughuli zake za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya umma, kwa ujumla.