Msaada wa Kibinadamu

WFP yafungua ofisi mpya Usomali ya Kati

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limefungua ofisi mpya katika eneo la Usomali ya Kati. Hatua hii muhimu iliochukuliwa na UM inatarajiwa kurahisisha shughuli za kuhudumia chakula watu muhitaji milioni moja ziada, waliokuwa wakitegemea shirika lisio la kiserikali, ambalo liliondoka nchini mwaka jana, kwa sababu ya ukosefu wa usalama wa wafanyakazi.

UNDP na UNAIDS washirikiana na wabunge wa Afrika na Mashariki ya Kati kupambana na UKIMWI

Karibuni kulianzishwa ushirikiano mpya baina ya mashirika ya UM na taasisi ya wabunge wa kutoka Afrika na Nchi za Kiarabu, kwa makusudio ya kujumuisha jitihadi zao kwenye kadhia ya kudhibiti bora maambukizi ya vimelea vya UKIMWI kwenye maeneo yao.

UM wajitayarisha kuhudumia waathirika wa ukama Kenya

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripotiwa wiki hii kuandaa operesheni za kuhudumia misaada ya kunusuru maisha ya watu milioni 3.5, walioathirika na mavuno haba, kutokana na mvua chache katika Kenya mashariki.

WFP imeanza operesheni za kuhudumia chakula wakazi waliotengwa na mvua kali Kaskazini-Mashariki katika JKK

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeanza kudondosha vyakula, kutoka kwenye ndege, katika eneo la Dungu, kaskazini-mashariki katika JKK kwa lengo la kuwaokoa njaa wahamiaji 130,000 waliong\'olewa makazi pamoja na wenyeji wao, ambao wameng\'olewa makazi na kutenganishwa baada ya mvua kali kunyesha karibuni kwenye maeneo yao.

Operesheni za kuwarejesha wahamiaji wa Burundi zaihusisha UNHCR

Mapema wiki hii, Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) Ijumatatu lilishiriki kwenye juhudi za kuwarejesha Burundi wahamiaji 529, kutoka kambi ya Kigeme, iliopo kwenye Wilaya ya Nyammgabe katika Rwanda kusini.

Mfuko wa maafa ya dharura waipatia Kenya dola milioni 8.6 kuhudumia misaada ya kihali

John Holmes, Mratibu Mkuu wa UM juu ya Misaada ya Dharura, ameidhinisha dola milioni 8.6 zitolewe kutoka Mfuko wa UM wa Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF, ili kufadhilia miradi ya kuwavua mamia elfu ya watu nchini Kenya na matatizo ya ukame, bei ya juu ya chakula duniani, na kujistiri kimaisha na mabaki ya athari za vurugu la baada ya uchaguzi, pamoja na kudhibiti mripuko wa maradhi ya kipindupindu, na vile vile kukidhi mahitaji ya umma wa Usomali uliopo Kenya kwa sababu ya mifumko ya mapigano nchini mwao.

Makisio ya UM kuhusu hali katika jimbo la NWFP, Pakistan

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti hali kwenye eneo la mapigano la Jimbo la Mpakani Pakistan katika Kaskazini-Magharibi (NWFP) inashuhudia muongezeko mkubwa wa mateso kwa raia walionaswa katikati ya mapigano.

Makundi yanayopigana Sri Lanka yatakiwa kuhishimu usalama wa raia

Verinoque Taveau, Msemaji wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) aliwaambia waandishi habari Geneva kwamba makundi yanayopambana katika Sri Lanka, yaani vikosi vya Serikali na waasi wa kundi la LTTE [Tamil Tiger], yamenasihiwa na UNICEF kufanya kila wawezalo kuwahakikishia raia ushoroba wa kupita, bila ya kushambuliwa kwenye mazingira ya uhasama.

Kuharibika ghafla kwa usalama Chad Mashariki kwaihangaisha UM

Jamii ya wahudumia misaada ya kiutu katika Chad imeripoti kushtushwa kwa kuharibika kwa ghafla hali ya usalama Chad mashariki katika wiki za karibuni.

John Holmes ameanza ziara ya siku sita Sudan Kusini na Darfur

John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu amewasili Sudan kuanza ziara ya siku sita ili kufanya mapitio juu ya miradi ya kuhudumia misaada ya kihali katika Sudan Kusini na Darfur.