Msaada wa Kibinadamu

Wahamiaji wa Usomali waomba hifadhi katika mataifa jirani

UNHCR imeripoti kwamba kuanzia 2008 walirajisisha raia 15,000 wa kutoka Usomali ambao waliomba kupatiwa mahali pa hifadhi katika mataifa jirani ya Kenya, Djibouti, Ethiopia na Sudan mashariki.

Mashirika ya UM yajiandaa kusaidia kihali Comoros pindi yatahitajika

Mashirika ya UM yanayohusika na misaada ya kiutu - ikijumuisha zile taasisi zinazohusika na maendeleo ya watoto, UNICEF; afya, WHO; Misaada ya Dharura, OCHA na pia usalama, UNDSS – yametangaza kipamoja kwamba yameshijiandaa kuhudumia misaada ya dharura Masiwa ya Comoros, pindi msaada huo utahitajika baada ya kuripotiwa kwamba vikosi vya Serikali, vikisaidiwa na majeshi ya Umoja wa Afrika kutokea Sudan na Tanzania walishambulia kisiwa cha Anzuwani Ijumanne, na kumwondosha raisi muasi Mohamed Bacar.

UM imetangaza huzuni kubwa kwa mauaji ya madereva wanaohudumia chakula Sudan

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kusikitishwa na kushtushwa sana na ile taarifa iliyothibitisha madereva watatu walioajiriwa na UM Sudan kuhudumia misaada ya kiutu waliuawa hivi karibuni. Ijumamosi, dereva mmoja anayeitwa Mohamed Ali alipigwa risasi na kuuawa na washambuliaji wasiojulikana, na walimjeruhi vibaya msaidizi wake pale walipokuwa kwenye barabara inayoelekea Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.

UNICEF yahitaji msaada wa dharura kwa waathiriwa mafuriko Namibia

UNICEF imetoa ombi linalotaka ifadhiliwe msaada wa dharura wa dola milioni 1.2 ili kufarajia misaada ya kiutu kwa watu 65,000 waliopo eneo la Namibia kaskazini, umma ambao makazi yao yaliangamizwa na mvua kali zilizonyesha katika miezi ya Januari na Februari mwaka huu. Mvua hizi zilikiuka kiwango cha kawaida na zilisababisha mafuriko yaliogharikisha mastakimu kadha wa kadha nchini humo.

UNICEF yahudumia kidharura waathiriwa wa Tufani Ivan Bukini

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) limo mbioni kuifadhilia Bukini huduma za kihali, baada ya Tufani Ivan Maututi kupiga kwenye eneo hilo mwezi uliopita, na kuangamiza makazi ya watu karibu 200,000. Hivi sasa UNICEF inafadhilia makumi elfu ya waathiriwa madawa, vyandarua, mablangeti pamoja na vifaa vya huduma ya afya.

Msumbiji yafadhiliwa misaada ya dharura baada ya madhara ya Tufani Jokwe

Mashirika ya UM juu ya maendeleo ya watoto (UNICEF) na miradi ya chakula (WFP) hivi sasa yanashiriki kwenye huduma za dharura za kusaidia umma wa Msumbiji kihali. Majuzi Tufani Jokwe, iliopiga eneo la kati na kaskazini ya taifa ilisababisha uharibu mkubwa wa zaidi ya nyumba 8,000 kwenye sehemu za mwambao na kuathiri watu 40,000 waliolazimika kungo\'lewa makwao.

Mamia ya walimu Sudan kufadhiliwa na Ujapani misaada ya kuimarisha taaluma

Serikali ya Ujapani imelifadhilia Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) msaada wa dola milioni 8.7 zitakazotumiwa mnamo miaka mitatu ijayo, kuwapatia mafunzo ya ualimu, Sudan kusini, mamia ya watu wanaohitajika kusomesha watoto wa eneo hilo.

Operesheni za WFP Darfur zapwelewa kwa sababu ya uharamia

Shirika la la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuwa linakabiliwa na tatizo ambalo “halijawahi kutokea hapo kabla” wakati linapoendeleza operesheni zake za kugawa misaada ya kihali kwa watu milioni 2 wanaohitajia chakula ambao huishi katika Darfur, Sudan.

Ziara ya Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji nchini Tanzania

Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) anazuru Tanzania hivi sasa. Kwa mujibu wa Msemaji wa UNHCR, Guterres anatarajiwa kuanzisha mradi wa miaka miwili nchini Tanzania uliokusudiwa kuhitimisha lile tatizo kongwe la wahamiaji karibu 218,000 wa kutoka Burundi waliopo Tanzania, umma ambao ulihama nchi baada ya machafuko ya 1972 kwenye maeneo yao.~

Wahamiaji wa Darfur kufadhiliwa misaada ya dharura na UNHCR

Ron Redmond, Msemaji wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), aliwaambia waandishi habari mjini Geneva Ijumanne kwamba UM unaendelea kutoa misaada ya dharura kwa wahamiaji wa Darfur Magharibi waliomiminikia maeneo ya Birak na Sorok, Chad mashariki katika siku za karibuni wakikimbia mapigano. UNHCR imeripoti kwamba itawapeleka wale wahamiaji waliodhoofika kwenye kambi za Kounoungou iliopo mbali na mipaka na Sudan. Takwimu za UNHCR zimethibitisha kwamba kuanzia mwezi Februari wahamiaji wa Darfur Magharibi 13,000 walisajiliwa kuingia Chad kutoka Sudan.