Shirika la afya duniani, WHO limesema katika siku nne zilizopita, watu wengine 27 wamethibitika kuwa na virusi vya Ebola huko jimbo la Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limefikisha mahema 435 ya dharura katika eneo la Balikpapan ili yagawiwe kwa familia ambazo zimeachwa bila makazi na zahma ya tetemeko na tsunami kwenye jimbo la Sulawesi.
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeorodhesha mateso kwa raia wa kawaida katika eneo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini ambapo watu 900 walitekwa na wengine 24,000 walilazimishwa kukimbia makazi yao kutokana na kuongezeka kwa ghasia kati ya mwezi Aprili na Agosti mwaka huu kabla ya makubaliano ya amani nchini humo.
Umoja wa Mataifa umesema bado una imani na uongozi wa Afrika katika kutatua matatizo ya bara hilo na kwamba Umoja wa Mataifa una nia ya dhati kutumia fursa zilizopo sasa kufanya kazi kwa karibu zaidi na Muungano wa Afrika, AU.
Mkutano wenye lengo la kutathmini na kuchagiza ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU unaanza leo katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.
UNICEF inasema zaidi ya watoto milioni 4 nchin Syria wameanza elimu rasmi mwezi uliopita wa Septemba lakini wengine milioni 2 bado hawana fursa ya elimu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani nchini Indonesia, leo ametembelea eneo la Sulawesi lililokumbwa na tetemeko la ardhi na tsunami tarehe 28 mwezi uliopita wa Septemba.
Sudan Kusini inashuhudia ongezeko la idadi ya watu wanaojiua au wanaojaribu kujiua kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takribani miaka mitano sasa, ambayo pia vimesababisha watu milioni 2 kukimbilia nchi jirani na wengine milioni 1.9 kusalia wakimbizi wa ndani nchini humo. Flora Nducha na ripoti kamili.
Fedha za ufadhili kwa mamilioni ya watu waliolazimika kukimbia makwao na wasio na utaifa zinazidi kuwa finyu na kuwaacha watu hao wakibeba gharama kubwa ya kutotimiziwa mahitaji yao ya msingi. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na kitengo cha wahisani na huduma ya kukusanya fedha cha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.
Amani ya kudumu na endelevu haitopatikana nchini Sudan Kusini endapo jamii hususan wanawake hawatoshirikishwa katika mchakato wa kuileta. Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa operesheni za ulinzi wa Umoja wa Mataifa Jean Pierre Lacroix baada ya kukutana na wanawake wakimbizi wa ndani kwenye eneo la Bentiu nchini humo.