Msaada wa Kibinadamu

Uhaba wa msaada kuhatarisha huduma za kihali kwa raia 53,000 Djibouti

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuwa litalazimika kusitisha karibuni ugawaji wa chakula kwa watu muhitaji 53,000 nchini Djibouti, wanaotegemea misaada ya kimatifa, kwa sababu ya upungufu mkubwa uliopo wa misaada ya fedha zinazohitajika kununulia chakula.

Mshauri Mkuu wa UM juu ya Misaada ya Dharura anazuru Sudan

Mshauri Mkuu [mpya] wa UM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes ambaye anazuru Sudan hivi sasa, alifanya mazungumzo na viongozi wa serekali kuhusu masuala ya kuhudumia kihali waathiriwa wa vurugu la Darfur.

UNHCR yasaidia Wakongomani 35 kuhajiri Marekani kuanza maisha mapya

Kundi la kwanza la Wakongomani 35, kati ya 500 walionusurika mauaji ya halaiki katika Burundi, wanatarajiwa karibuni kuanza safari ya uhamishoni Marekani kuanzisha maisha mapya. Msaada huu ulichangiwa na Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamaiji (UNHCR).

Juhudi za kidiplomasiya zachacha kusuluhisha mzozo wa Darfur

Tume ya Baraza la Haki za Kibinadamu iliyodhaminiwa madaraka ya kufanya uchunguzi kuhusu utekelezaji wa haki za kimsingi katika Darfur, majuzi ilichapicha ripoti yenye kuishinikiza Serekali ya Sudan kuharakisha uamuzi wa kuisaidia Umoja wa Mataifa (UM) pamoja na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU)kupeleka vikosi vya mseto vitakavyotumiwa kulinda amani katika jimbo la Sudan magharibi la Darfur.

Maendeleo yaripotiwa Burundi kuhusu ulinzi wa watoto walioathirika na vita

Radhika Coomaraswamy, Mjumbe Maalumu wa KM kuhusu Hifadhi ya Watoto katika Mazingira ya Mapigano, alizuru Burundi wiki hii. Alisema kwamba ameshuhudia maendeleo ya kutia moyo katika juhudi za Serekali kuwapatia watoto walionaswa kwenye hali ya uhasama na vita, ulinzi bora na hifadhi inayotakikana kisheria.

Mashirika ya UM yahitajia dola milioni 18 kusaidia waathiriwa wa kimbunga na mafuriko Msumbiji

UM pamoja na mashirika wenzi yanayohudumia misaada ya kiutu, yameanzisha kampeni ya dharura kuchangisha karibu dola milioni 18 ili kuisaidia Msumbiji kukabiliana na mahitaji ya kihali, hususan kwa umma muathiriwa na mafuriko pamoja na uharibifu wa vimbunga, maafa ambayo yalisababisha uharibifu mkubwa nchini humo hivi karibuni.

Mahakama Kuu ya Zimbabwe kupongezwa na UM kwa uamuzi juu ya kiongozi wa upinzani

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour amenakiliwa akisema anaunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe ulioishurutisha Serekali kumruhusu kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC, Morgan Tsvangirai kupelekwa hospitali kupatiwa matibabu baada ya kuthibitika kwamba alipigwa na kujeruhiwa vibaya na vikosi vya polisi alipokuwa kizuizini.

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limewaslisha wiki hii mjini Roma, Utaliana ripoti yenye mada isemayo "Hali ya Misitu Duniani 2007". Ripoti ilisema maeneo kadha duniani yamefanikiwa kudhibiti uharibifu wa misitu ulioendelezwa karne kwa karne. Kwa mujibu wa ripoti misitu kadha imefanikiwa kufufuliwa na kupanuliwa kwenye kanda mbalimbali za kimataifa kwa sababu ya usimamizi mzuri, na wa hadhari, ikichanganyika na sera za kisasa zilizotumiwa na mataifa husika katika kuhifadhi mazingira kwa ujumla. Ripioti ilisema mataifa 100 ziada hivi sasa yameandaa mipango ya kizalendo kuhifadhi misitu.

WFP inabashiria tatizo la njaa kusini ya Afrika

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuingiwa na wasiwasi unaoashiria kufumka, kwa mara nyengine tena katika maeneo ya kusini ya Afrika, janga la njaa kwa sababu ya kujiri karibuni kwa hali ya hewa ya kigeugeu. Hali hii imezusha ukame na mafuriko ambayo yaliharibu mavuno na kuathiri mamilioni ya watu watakaotegemea kusaidiwa chakula na jamii ya kimataifa kwa mwaka mzima.

UM unatarajia matokeo mazuri Usomali

Eric Laroche Mshauri wa UM kuhusu Misaada ya Kiutu kwa Usomali alipokutana na waandishi habari wa kimataifa hapa Makao Makuu wiki hii aliashiria ya kwamba Usomali, kwa sasa, imebahatika kushuhudia “vuguvugu la mabadiliko” yaliyowapatia umma matumaini ya kwamba Serekali mpya itajinyakulia fursa ya utawala iliyobarikiwa karibuni na kurudisha amani na utulivu katika taifa ambalo limenyimwa uongozi wa Serekali halali tangu 1991.~~