Msaada wa Kibinadamu

Cameroon inahitaji misaada ya dharura kuhudumia kihali wahamiaji wa CAR

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetoa ombi maalumu linaloitaka jumuiya ya kimataifa kuharakisha mchango wa misaada ya kihali kunusuru maisha ya wahamaiji 45,000 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaoishi sasa hivi kwenye eneo la mashariki katika taifa la Cameroon.

UNMIL kushirikiana na Serikali Liberia kuzalisha ajira

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani Liberia (UNMIL), likishirikiana na Benki Kuu ya Dunia, UNDP, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) na shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) linaendeleza mradi maalumu wa pamoja wa kujenga barabara zilizoharibiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, mradi utakaosaidia kuzalisha ajira kwa watu 50,000 vijijini. Mradi huu unaendelezwa shirika na Serikali ya Liberia, halkadhalika.

Demokrasia inaanza kushika mizizi DRC, asema KM Ban

Katika ripoti ya UM iliowasilishwa karibuni kusailia hali katika JKK (DRC) KM Ban Ki-moon alithibitisha kwamba usalama wa taifa uliathiriwa nchini na haki za binadamu ziliharamishwa kwa sababu ya kuzuka migogoro miwili; kwanza, uhasama uliochipuka, baada ya kufanyika uchaguzi, baina ya serikali na wafuasi wa Makamu Raisi wa zamani, Jean-Pierre Bemba na, pili, mikwaruzuano ilioselelea kieneo kati ya Jeshi la Taifa na wanajeshi waasi, ambao huongozwa na Jenerali aliyetoroka jeshi Laurent Nkunda.

Darfur: wajumbe wa UM na AU waimarisha juhudi za kutafuta muelewano kati ya waasi.

Majumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, kwa ajili ya mzozo wa Darfur, Jan Eliasson na Salim Ahmed Salim wa Jumuia ya Afrika AU, wamesema wanaimarisha juhudi zao za kuyahimiza makundi makubwa yanayotengana huko Darfur kutafuta muelewano wa pamoja kabla ya mkutano wa amani ulopangwa kufanyika na Serekali ya Sudan mwezi ujao.

IFAD kusaidia wanavijiji masikini Lesotho

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) limeanzisha mradi mpya wa dola milioni 8.7 kusaidia wanavijiji masikini 37,000 katika Lesotho. Mradi huu utawafadhilia wanavijiji husika mchango wa fedha za kuekeza kilimo chenye natija kiuchumi na kijamii kwenye maeneo yao.

KM kuwapongeza watunukiwa Tunzo ya Amani ya Nobel kwa 2007

KM wa UM Ban Ki-moon amepongeza uamuzi wa Kamati ya Nobel kwa kutunikia, shirika, Tunzo ya Amani ya Nobel kwa 2007 kwa aliyekuwa Makamu-Raisi wa Marekani Al Gore na pia kwa ile Tume ya Serikali za Kimataifa ya Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (IPCC).

Hapa na pale

Tarehe 16 Oktoba huadhimishwa na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na aila nzima ya UM kuwa ni ‘Siku ya Chakula kwa Wote Duniani’. Siku hii hutumiwa kuwazindua walimwengu ya kwamba watu milioni 854 bado wanaendelea kuteswa na kusumbuliwa, kila siku, na tatizo sugu la njaa na ukosefu wa chakula, idadi ya waathiriwa ambayo inazidi kukithiri kwa sababu ya mifumo dhaifu ya kilimo, ugawaji usiotosheleza wa chakula, uwezo usiofaa wa kuhifadhia chakula, na vile vile kutokana na hali ya vurugu na mapigano, mazingira ambayo hukwamisha huduma za kilimo kwenye maeneo husika.

UNMIS yalalamika watumishi wa NGOs washambuliwa kihorera Sudan

Shirika la UM juu ya Amani kwa Sudan (UNMIS) limeripoti watumishi wa mashirika yasio ya kiserekali (NGOs) wanaohudumia misaada ya kiutu katika eneo hilo la vurugu bado wanaendelea kushambuliwa kihorera na makundi mbalimbali ya waasi na wahalifu wengine.

UNHCR inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za kuhudumia wahamiaji wa Sudan

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kuwa linakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha ambazo zinahitajika haraka kutumiwa kwenye zile huduma za kuwarejesha makwao Sudan Kusini wahamiaji waliopo mataifa jirani, na pia kuwahudumia kihali wahamiaji milioni 2 wengine wa kutoka Darfur magharibi.

UM bado kuendeleza operesheni za kihali kwa waathiriwa wa mafuriko Uganda

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura Duniani (OCHA) imeripoti mafuriko bado yanaendelea kuisumbua Uganda, hali ambayo imeilazimisha UM kuendeleza zile operesheni za kuhudumia misaada ya kihali ya kunusuru maisha ya raia waathiriwa na janga hili la kimaumbile. OCHA imeripoti kuhitajia mchango ziada wa dharura, kuweza kukidhia mahitaji ya kimaisha ya umma husika.