Haki za binadamu

Uzuizi wa kihorera, askari wa kukodiwa na taka za sumu kusailiwa na BHB

Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu (BHB) limekutana mjini Geneva Ijumatatu kuzingatia ripoti tatu muhimu: awali, ripoti kuhusu taathira mbaya ya afya kutokana na utupaji haramu wa mabaki ya bidhaa za sumu, hususan katika mataifa yanayoendelea; pili, ripoti juu ya uzuizi wa kihorera unaowanyima watuhumiwa fursa ya kufikishwa mahakamani kuhukumiwa na, tatu, Baraza limezingatia ripoti kuhusu matumizi ya askari wa kukodiwa ambao hutumia mabavu kuuzuia umma usitekeleze haki yao halali ya kujiamulia wenyewe. ~~

Mchochezi wa mauaji Rwanda kumalizia kifungo Utaliana

Georges Omar Ruggu, mwandishi habari wa redio aliopatikana na hatia ya kuchochea mauaji ya halaiki dhidi ya raia wenye jadi ya KiTutsi nchini Rwanda katika 1994, na ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 12 na Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) alihamishwa Alkhamisi kwa ndege ya kijeshi kutoka kizuizini Arusha, Tanzania na kupelekwa kifungoni Utaliana kumaliza adhabu yake.

Mashirika ya UM yanuia kukomesha ukeketaji wa watoto wa kike duniani

Mashirika kumi ya Umoja wa Mataifa - yakijumuisha yale mashirika yanayoshughulikia huduma za kudhibiti UKIMWI (UNAIDS), kuimarisha miradi ya maendeleo (UNDP), maendeleo ya elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), Kamisheni ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (UNECA) na Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani, UNFPA; na vile vile yale yanayohusika na ulinzi wa haki za binadamu (OHCHR), huduma za wahamiaji (UNHCR), mfuko wa maendeleo ya watoto (UNICEF), mfuko wa maendeleo ya wanawake (UNIFEM) na pia afya ya kimataifa (WHO)- Ijumatano yametoa ripoti ya pamoja iliyoahidi kuchangisha kila juhudi ili kukomesha ile tabia haribifu ya kutahiri watoto wa kike, katika kipindi cha kizazi kimoja, pote duniani.

'Twachoka kusubiri', unyanyasaji wa wanawake ukomeshwe halan - KM Ban

KM Ban Ki-moon Ijumatatu alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri kadha walioshiriki kwenye taadhima za ufunguzi rasmi wa kikao cha mwaka cha 52 cha Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake (CSW). Kwenye risala ya ufunguzi, mbele ya wawakilishi wa kimataifa, KM Ban alichukua fursa ya kuanzisha kampeni ya kimataifa itakayojumuisha UM na mashirika yake yaliozagaa kote duniani, na kuchangisha serikali za Nchi Wanachama na jumuiya za kiraia, halkadhalika, kufyeka kidharura, na kwa nguvu moja, vitendo vyote vya unyanyasaji, utumiaji mabavu na udhalilishaji wa wanawake. Alisema vitendo karaha kama hivi dhidi ya wanawake havistahamiliki kamwe. ~~Sikiliza taarifa kamili kwenye idhaa ya mtandao.

KM ameanzisha rasmi kampeni ya kimataifa dhidi ya unyanyasaji wa wanawake

Asubuhi ya leo, Ijumatatu, Februari 25, KM wa UM Ban Ki-moon alianzisha rasmi kampeni ya kimataifa ya kukomesha na kufyeka tabia ya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya wanawake na watoto wa kike duniani. Kampeni ilitilia mkazo umuhimu na ulazima wa kukomesha kidharura vitendo vyote vya udhalilishaji wa kijinsia. Kampeni hii imeanzishwa siku ile ile ambapo Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake (CSW)ilipfungua rasmi, kwenye Makao Makuu ya UM, kikao cha mwaka, cha 52. Tutakupatieni taarifa zaidi juu ya Mkutano wa CSW hapo kesho. ~

OHCHR inalaani ukiukaji wa haki za binadamu Chad

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki Binadamu (OHCHR) imearifu kupokea taarifa za kutia wasiwasi zilizoonyesha vikosi vya usalama vya Serikali viliwateka nyara viongozi kadha wa upinzani, pamoja na kuwashika viongozi wa jumuiya za kiraia na kuwatia kizuizini baada ya kutukia mashambulio ya waasi karibuni kwenye mji mkuu wa N’Djamena, Chad .

Mazungumzo ya amani ya Uganda Kaskazini yabashiria matokeo ya kutia moyo

Wawakilishi wa Serikali ya Uganda pamoja na wale wa kundi la waasi wa LRA, wanaokutana hivi sasa katika mji wa Juba, Sudan Kusini kujadilia mamsuala ya upatanishi na amani wamekubaliana kuunda idara maalumu ya mahakama kuu itakayodhaminiwa madaraka ya kusimamia mashtaka ya watuhumiwa wa jinai ya vita viliyoshtadi nchini mwao kwa miaka ishirini na moja.

Baraza la Usalama lazungumzia hifadhi ya watoto wanaonaswa kwenye mazingira ya mapigano

Baraza la Usalama liliitisha kikao maalumu cha siku moja katika Makao Makuu, ambapo wajumbe kadha wa kadha walishauriana hatua za kuchukuliwa na Mataifa Wanachama ili kuwalinda watoto wenye umri mdogo dhidi ya vitimbi vya udhalilishaji, mateso na uonevu wanaokabiliwa nawo wakati wanapozongwa na mazingira ya migogoro na mapigano, unyanyasaji ambao umeonekana kukithiri katika miaka ya karibuni, hasa kwenye yale maeneo yalioghumiwa na kukumbwa na hali ya mapigano.~

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani (UNIFEM) imeihimiza jamii ya kimataifa kuongeza juhudi za kukomesha kihakika, tabia hatari ya kutahiri watoto wa kike. UNIFEM imependekeza kwa nchi wanachama kuheshimu haki za wanawake pamoja na watoto wakike pote duniani, mwito ambao ulitangazwa Februari 7 (08) katika kipindi ambacho walimwengu walikuwa wakiiadhimisha na kuiheshimu Siku ya Kimataifa dhidi ya Ukeketaji wa Wanawake.

'Wahamiaji wanaorejea JKK kutoka Tanzania wamefikia 50,000': UNHCR

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kwamba wahamiaji 184 waliorejeshwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kutokea Tanzania hivi majuzi, wamejumuisha wahamiaji 50,000 – fungu ambalo liliamua kurejeshwa makwao kwa hiyari.