Haki za binadamu

Wataalamu wa UM wamehadharisha wajumbe wa Kikao cha BK juu ya Mzozo wa Uchumi kutosahau kufungamanisha haki za binadamu kwenye maamuzi yao

Magdalena Sepúlveda na Cephas Lumina, Wataalamu Huru wawili wa UM wanaohusika na masuala ya haki za kibinadamu kwenye mazingira ya umaskini uliovuka mipaka na kuhusu athari haribifu za madeni, wametuma taarifa maalumu kwenye Mkutano wa Baraza Kuu juu ya Mizozo ya Uchumi na Kifedha, iliohimiza Mataifa Wanachama "kuchukua hatua za dharura, zitakazosaidia kuendeleza ufufuaji wa muda mrefu wa shughuli za kiuchumi na fedha, kwa kutunza haki za kimsingi kwa umma mamskini wenye kusumbuliwa zaidi na matatizo haya ya kiuchumi" kwa kupatiwa huduma za jamii.

KM amehuzunishwa sana na uvamizi wa kunajisi kimabavu wanawake wafungwa katika JKK

KM Ban Ki-moon ametangaza kuhuzunishwa sana na ripoti alizopokea karibuni, kuhusu tukio la uvamizi na vitendo vya kunajisi kimabavu, wafungwa wanawake 20 waliojaribu majuzi kukimbia kutoka gereza kuu la Goma, liliopo katika eneo la mashariki ndani ya JKK.

Idadi kubwa ya wakazi wa eneo la mapigano katika JAK wamehajiri mastakimu: OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti mashambulio yaliotukia Ijumapili alfajiri, tarehe 21 Juni, kwenye mji wa Birao, kaskazini-mashariki ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yamesababisha idadi kubwa ya wakaazi kuhama kidharura eneo hilo.

UNHCR ina wasiwasi na kunyanyuka kihadhi kwa vyama baguzi vipingavyo wageni katika EU

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetoa mwito maalumu wenye kuisihi Serikali ya Sweden kutumia wadhifa uliokabidhiwa nao sasa hivi, wa uraisi wa Umoja wa Ulaya (EU), kutilia mkazo umuhimu wa nchi wanachama kusimamia shughuli za mipaka yao, kwa kuzitekeleza kanuni za huruma za kuruhusu wahamaji wa kigeni kupata hifadhi, kama ilivyoidhinishwa na haki za kimsingi za kiutu.

Idadi kubwa ya wahamaji wa Usomali na Ethopia wanaotoroshwa Afrika Kusini huteswa na wafanya magendo, inaripoti IOM

Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM) limetoa ripoti mpya kuhusu "uhamaji usio wa kawaida" ambao huwatesa wale watu wanaotoroshwa kimagendo kutoka Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, wanaopelekwa Afrika Kusini.

ICTR imetangaza kifungo cha miaka 30 kwa mtuhumiwa Kalimanzira

Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) imetangaza hukumu ya kifungo cha miaka 30, kwa Callixte Kalimanzira, aliyekuwa ofisa Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Rwanda katika 1994, ambaye alipatikana na hatia ya jinai ya mauaji ya kuangamiza makabila, na pia makosa ya kuchochea watu kuendeleza mauaji ya halaiki.

Siku ya Dunia Dhidi ya Ajira ya Watoto Wadogo

Kwenye kumbukumbu ya miaka 10 ya Siku ya Dunia dhidi ya Ajira ya Watoto wa Umri Mdogo, siku ambayo huadhimishwa tarehe ya leo kulitolewa mwito maalumu na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), likijumuika na mashirika wenzi wa kuhimiza jamii ya kimataifa kukabiliana na sababu za msingi zenye kuchochea umasikini na ufukara, hali ambayo inaaminika ndio yenye kuwalazimisha watoto wenye umri mdogo kutafuta ajira ya kumudu maisha.

Walimwengu waandamana kuunga mkono juhudi za WFP kupiga vita njaa duniani

Ijumapili ya tarehe 07 Juni (2009) makumi elfu ya watu, katika sehemu mbalimbali za dunia, walikusanyika kwenye miji kadha ya kimataifa, na kuandamana kuunga mkono juhudi za Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) katika kupiga vita tatizo la njaa ulimwenguni, hususan miongoni mwa watoto wadogo.

Wawakilishi wa tamaduni za kijadi Afrika Mashariki wazingatia kikao cha mwaka juu ya haki za wenyeji wa asili

Wiki hii tutakamilisha makala ya pili ya yale mahojiano yetu na wawakilishi wawili wa jamii za makabila ya wenyeji wa asili kutoka Afrika Mashariki, ambao karibuni walihudhuria kikao cha nane cha ile Tume ya Kudumu ya UM juu ya Haki za Wenyeji wa Asili Duniani kilichofanyika Makao Makuu.

Hali ya usalama wa kigeugeu Kivu Kaskazini inaitia wasiwasi OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti hali ya usalama wa raia, ulioregarega Kivu Kaskazini, inaitia wasiwasi mkubwa wahudumia misaada ya kiutu waliopo katika JKK.