Haki za binadamu

Radovan Karadzic awekwa rumande Hague kwenye kituo cha UM

Radovan Karadzic Ijumatano asubuhi alihamishwa kutoka Serbia, eneo aliokamatwa mnamo tarehe 21 Julai 2008, na amepelekwa kizuizini mjini Hague, Uholanzi penye Kituo cha Kufungia Watu cha UM. Nerma Jelacic, Msemaji wa Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya UM juu ya Yugoslavia ya Zamani (ICTY) alithibitisha taarifa hiyo kwenye mazungumzo na Redio ya UM.~

OCHA imeripoti Wakongo 65,000 wafukuzwa Angola

Christophe Illemassene, Msemaji wa Shirika la UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) katika JKK ameiambia Redio ya UM-Geneva kwamba wana taarifa iliothibitisha kuwa tangu Mei mwaka huu raia wa Kongo 65,000 walifukuzwa na kuondoshwa kutoka Angola, wingi wao wakiwa wale wahamiaji walioingia Angola bila sheria, wakitafuta ajira kwenye viwanda vya migodi.

Tume ya waliotoweka bila khiari duniani inakutana Argentina

Tume ya Utendaji ya UM juu ya Watu Waliolazimishwa Kutoweka na Kupotea Bila Khiari inakutana katika mji wa Buenos Aires, Argentina kuanzia Julai 24 mpaka 26 kufanya mapitio ya kesi za watu 300 waliotoweka duniani, kuambatana na matatizo ya kisiasa. Tume hiyo ina wajumbe wataalamu watano na inakutana, kwa mara ya kwanza katika taifa la Amerika ya Latina la Argentina, taifa ambalo katika miaka ya sabini na mwanzo wa miaka ya themanini liliathirika sana na tatizo la kupotea kwa wapinzani wingi wa kisiasa, bila ya aila zao kujua walipo.

Sera ya EU kudhibiti wahamiaji yashtusha wataalamu wa haki za binadamu wa UM

Wataalamu kumi wanaohusika na Masuala Makhsusi ya Baraza la Haki za Binadamu wamemtumia barua maalumu Raisi wa Baraza la Umoja wa Ulaya, uraisi ambao unashikwa na Ufaransa kwa sasa, inayobainisha wasiwasi wao kuhusu pendekezo la \'Mwongozo wa EU juu ya Udhibiti wa Uhamiaji\' kwenye nchi wanachama wa EU. Sera imependekeza mataifa yote yakubali kutekeleza kipamoja sheria za kuwarejesha makwao, bila khiyari, wale raia wwenye kuishi kwenye mataifa ya EU ambao waliokiuka ruhusa ya muda wa ukaazi.

Adhabu za kifo Marekani zinatathminiwa na Mkariri Maalumu wa Haki za Binadamu

Profesa Philip Alston ni Mkariri Maalumu wa UM anayehusika na haki za binadamu zinazofungamana na masuala ya hukumu ya vifo, nje ya sheria, pamoja na mauaji ya kihorera. Majuzi Alston aliwakilisha mbele ya waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu ripoti maalumu iliosailia namna hukumu ya vifo inavyotekelezwa katika taifa la Marekani.

Tume ya UM inasema hali katika OPT inazidi kuharibika

Tume ya Wataalamu Watatu wa Kamati Maalumu ya Kuchunguza Vitendo vya Israel dhidi ya Haki za Binadamu za Wafalastina na Waarabu Wengine kwenye Maeneo Yaliokaliwa Kimabavu (OPT) baada ya kukamilisha ziara yao Jordan, na baada ya kusikiliza ushahidi kutoka watu wanaoshidi kwenye maeneo hayo, walibainisha kuwa na wasiwas mkubwa juu ya kuzidi kuharibika kwa hali za kiutu na ukiukaji wa haki za kibinadamu kwenye maeneo husika, hususan katika Tarafa ya Ghaza.