Haki za binadamu

Ofisa wa UM kuonya, vita, vurugu na uhasama huumiza mamilioni ya raia duniani

Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu, John Holmes aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama Ijumanne kwamba fungu kubwa lenye kuathirika kihali na mali kunapojiri uhasama, vita na vurugu katika maeneo ya kimataifa ni mamilioni ya raia wasio hatia.

Naibu Kamishna Mkuu juu ya Haki za Binadamu azuru Cote d'Ivoire na Liberia

Naibu Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Kyung-wha Kang wiki hii ameanza ziara maalumu, ya pili, katika mataifa ya Cote d\'Ivoire na Liberia ambapo atafanya mazungumzo na viongozi wenye mamlaka, makundi yanayowakilisha jumuiya za kiraia, pamoja na wanadiplomasiya, na vile vile watumishi wa vyeo vya juu wa UM na kushauriana nao kuhusu hatua za kuchukuliwa kipamoja, zitakazohakikisha kadhia ya kuhifadhi haki za raia itatumiwa kuwa ni kipengele muhimu cha upatanishi miongoni mwa makundi yanayohasimiana, na pia katika kufufua kadhia za kiuchumi na jamii kwenye mataifa husika.

IOM/UNICEF yashirikiana kuhudumia waathiriwa wa mashambulio ya chuki za wageni Afrika Kusini

Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM) limeripoti kwamba linashirikiana na UNICEF kuwasaidia waathiriwa wa mashambulio ya chuki za wageni Afrika Kusini kurejea makwao. Msemaji wa IOM Geneva, Jemini Pandya alitupatia fafanuzi zake kuhusu suala hili.

Mkutano wa Mapitio ya Mapatano ya Durban kufanyika mwakani Geneva

Baada ya mvutano wa majadiliano miongoni mwa wanadiplomasiya wa kimataifa, wanachama wa Kamati ya Matayarisho ya Mkutano wa Mapitio ya Mapatano ya Durban, waliokutana Geneva, Ijumatatu wamekubaliana kuitisha kikao hicho Geneva mwezi Aprili, 2009 ambapo wajumbe wa kimataifa wanatarajiwa kuzingatia hatua za kuchukuliwa, kukabiliana, kwa nguvu moja, na masuala sugu ya ubaguzi na chuki za wageni. Matatizo haya bado yanaendelea kusumbua umma wa kimataifa katika karne tuliomo hivi sasa.

UNHCR itachunguza hadhi ya sheria mpya Utaliana inayofananisha uhamiaji na jinai

Shirika la Wahamiaji la UNHCR limeripoti kuwa litafuatilia, kwa ukaribu na makini zaidi, maana hakika ya sheria mpya iliopitishwa Ijumatano kwenye Mji wa Naples na Baraza la Mawaziri Utaliana, inayothibitisha kitendo cha uhamiaji usio halali kuwa sawa na kosa la jinai na uhalifu, ambao utastahiki hukumu ya kifungo cha muda mrefu gerezani kwa mtuhumiwa. ~~Kwa mujibu wa sheria hii mpya watu ambao ombi lao la kupata hifadhi ya kisiasa limekataliwa watalazimika kuondoka Utaliana bila ya fursa ya kukata rufaa; na wale wanaotaka kuomba hifadhi, ambao mara nyingi huingia nchini kwa njia zisio rasmi, wao watashitakiwa kufabya kosa la jinai lenye hukumu ya kifungo cha angalau miaka minne.~~ ~

Ripoti ya UNICEF kuonya, watoto duniani bado hulazimishwa kushiriki vitani

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripoti kwamba tatizo la kuajiri watoto wenye umri mdogo, ambao hushirikishwa kimabavu kwenye vurugu la vita na mapigano, ni suala liliothibitishwa kuendelezwa katika 2008, kinyume na kanuni za kimataifa.

Mkataba wa Kulinda Haki za Walemavu unasherehekewa na Baraza Kuu

Baraza Kuu la UM lilikusanyika kwenye Makao Makuu kwenye sherehe maalumu ya kuwaheshimu na kuwatambua wale wajumbe wajasiri wa kutoka Serikali Wanachama kadha, wakichanganyika na jamii ya watu walemavu pamoja na watumishi wa Taasisi kadha wa kadha za UM, kwa juhudi zao za muda mrefu ambazo zilifanikiwa kuwasilisha Mkataba mpya wa Kimataifa juu ya Haki za Watu Wenye Ulemavu pamoja na Itifaki ya Khiyari. Karibuni Mkataba wa Walemavu Duniani uliidhinishwa rasmi kuwa chombo cha sheria ya kimataifa, na utatumiwa kudhamini na kulinda haki za walemavu milioni 650 wanaoishi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu.

Mkataba wa Haki za Walemavu waridhiwa rasmi kimataifa

Ijumamosi ya tarehe 03 Mei 2008 Mkataba wa UM juu ya Haki za Watu Walemavu ulithibitishwa na kuidhinishwa kuwa chombo rasmi cha sheria ya kimataifa, mwezi mmoja tu baada ya taiifa la ishirini kuuridhia mkataba, ambao unatarajiwa kuwahakikishia watu walemavu milioni 650 duniani kuwa haki zao zinatambuliwa na kuheshimiwa. Mkataba wa Haki za Walemavu umeshatiwa sahihi na nchi wanchama 127 na kuridhiwa na mataifa 25 – Jamaika ikiwa nchi ya awali kufanya hivyo, wakati sahihi ya taifa la Ecuador ndio iliyouruhusu Mkataba kufanywa chombo rasmi cha Sheria ya Kimataifa.

Haki za msingi za nchi 16 zinafanyiwa mapitio na Baraza la Haki za Binadamu

Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu limeanza kufanya mapitio kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu kwa raia waliopo katika orodha ya pili ya nchi wanachama 16 wa UM. Mataifa ya Afrika yaliomo kwenye orodha hii ni pamoja na Gabon, Ghana, Zambia na Mali. Mikutano ya mapitio inaendelezwa katika Kasri la Kimataifa liliopo Geneva na itaendelea hadi tarehe 19 Mei.

Siku ya Kumbukumbu ya Kumaliza Biashara ya Utumwa Ulimwenguni (Sehemu ya II)

Katika makala iliopita, tulimsikiliza Mjumbe wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UM, Balozi Augustine Mahiga akitufafanulia maana halisi ya hii Siku ya Kumbukumbu ya Kumaliza Biashara ya Utumwa Ulimwenguni, kwa wanachama wa Umoja wa Afrika.