Hivi karibuni Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), likijumuika na wanaharakati wa Marekani wanaogombania haki za wanawake wanaowakilisha kundi linalojulikana kwa umaarufu kama Jumuiya ya V-Day, walitayarisha warsha mbili muhimu za pamoja, katika miji ya Goma na Bukavu. Kauli mbiu ya mkusanyiko huo ilikuwa na mada isemayo “Wanawake Wavunja Ukimya na Miko” – ambapo kwa mara ya kwanza, kihistoria, wale wanawake walionusurika na janga ovu la kunajisiwa kimabavu, walipata fursa ya kujieleza, hadharani, mbele ya kadamnasi ya raia, juu ya mateso waliopata kutokana na udhalilishaji wa kijinsia.