Haki za binadamu

'Haiwafalii Ghana kuhamisha kwa mabavu wahamiaji wa Liberia', yanasihi UNHCR

Ofisi ya UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) imewanasihi wenye madaraka Ghana kujitahidi kusitisha haraka uhamisho wa nguvu kwa wahamiaji wa Liberia. Nasaha hii ilitangazwa baada ya Ghana kuamua Ijumapili kuwaondosha nchini wahamiaji 16 ambao walirejeshwa makwao kwa mabavu, kinyume na kanuni za kimataifa. Wingi wa wahamiaji hawa walikuwa wamesharajisiwa na UM wakisubiri kufarijiwa mahitaji yao ya kihali na UNHCR.

Makao Makuu yawakumbuka na kuwaheshimu waathiriwa wa utumwa

Kuanzia Ijumanne ya leo, tarehe 25 Machi, UM umeanzisha taadhima za karibu wiki moja za kuwakumbuka waathiriwa wa janga la utumwa pamoja na kuadhimisha siku Biashara ya Utumwa kwenye ngambo ya Bahari ya Atlantiki ilipositishwa na Marekani miaka mia mbili iliopita.

'Ni dhamana ya walimwengu kuufyeka kipamoja ubaguzi', anasihi KM

Tarehe 21 Machi huadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa Kuondosha Ubaguzi; na kwenye risala ya kuiheshimu siku hiyo, Katibu Mkuu Ban Ki-moon alikumbusha tena kwamba sera za ubaguzi hazijatoweka bado na zinaendelea kudhuru watu binafsi na jamii kadha wa kadha katika sehemu mbalimbali za dunia. Kwa hivyo, alizinasihi nchi zote wanachama, pamoja na makundi ya jumuiya za kiraia, halkadhalika, kuongeza juhudi zao na michango yao ili kuhakikisha tunadhibiti vyema zaidi ukabila na ubaguzi wa rangi kote ulimwenguni.

Pande zinazohasimiana Darfur zaharamisha haki za binadamu dhidi ya raia

Mkariri Maalumu wa Baraza la UM juu ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu kwa Sudan, Sima Samar, baada ya kumaliza ziara ya siku 13 nchini humo ametoa ripoti yenye kuonesha “kushtushwa sana” kwa kuendelea kuharibika kwa hali ya utulivu katika eneo la Darfur Magharibi baada ya kufumka mapigano huko katika siku za karibuni.

Ajira ya askari wa kukodiwa ni lazima idhibitiwe kisheria - UM

Baraza la Haki za Binadamu linalokutana hivi sasa mjini Geneva Ijumatatu lilizingatia ripoti ya UM iliyotoa onyo ya kwamba kunahitajika kidharura kudhibiti kisheroa zile kampuni za binafsi, zinazoendelea kuenea na kuongezeka kila siku ulimwenguni, ambazo huajiri polisi na wanajeshi wa kukodiwa. Iligundulikana kampuni hizi huendeleza shughuli zao kitaifa na kwenye maeneo yenye uhasama, kama Afghanistan, Iraq na Colombia bila ya kuheshimu kanuni za kimataifa kwa sababu imedhihirika yanapokiuka sheria, huwa hakuna wa kuyakosoa, na wala hayafanyiwi mapitio ya shughuli zao, na hawajibiki kwa matendo yao yasiofuata sheria za kimataifa. ~

Uzuizi wa kihorera, askari wa kukodiwa na taka za sumu kusailiwa na BHB

Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu (BHB) limekutana mjini Geneva Ijumatatu kuzingatia ripoti tatu muhimu: awali, ripoti kuhusu taathira mbaya ya afya kutokana na utupaji haramu wa mabaki ya bidhaa za sumu, hususan katika mataifa yanayoendelea; pili, ripoti juu ya uzuizi wa kihorera unaowanyima watuhumiwa fursa ya kufikishwa mahakamani kuhukumiwa na, tatu, Baraza limezingatia ripoti kuhusu matumizi ya askari wa kukodiwa ambao hutumia mabavu kuuzuia umma usitekeleze haki yao halali ya kujiamulia wenyewe. ~~

Mchochezi wa mauaji Rwanda kumalizia kifungo Utaliana

Georges Omar Ruggu, mwandishi habari wa redio aliopatikana na hatia ya kuchochea mauaji ya halaiki dhidi ya raia wenye jadi ya KiTutsi nchini Rwanda katika 1994, na ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 12 na Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) alihamishwa Alkhamisi kwa ndege ya kijeshi kutoka kizuizini Arusha, Tanzania na kupelekwa kifungoni Utaliana kumaliza adhabu yake.

Mashirika ya UM yanuia kukomesha ukeketaji wa watoto wa kike duniani

Mashirika kumi ya Umoja wa Mataifa - yakijumuisha yale mashirika yanayoshughulikia huduma za kudhibiti UKIMWI (UNAIDS), kuimarisha miradi ya maendeleo (UNDP), maendeleo ya elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), Kamisheni ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (UNECA) na Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani, UNFPA; na vile vile yale yanayohusika na ulinzi wa haki za binadamu (OHCHR), huduma za wahamiaji (UNHCR), mfuko wa maendeleo ya watoto (UNICEF), mfuko wa maendeleo ya wanawake (UNIFEM) na pia afya ya kimataifa (WHO)- Ijumatano yametoa ripoti ya pamoja iliyoahidi kuchangisha kila juhudi ili kukomesha ile tabia haribifu ya kutahiri watoto wa kike, katika kipindi cha kizazi kimoja, pote duniani.

'Twachoka kusubiri', unyanyasaji wa wanawake ukomeshwe halan - KM Ban

KM Ban Ki-moon Ijumatatu alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri kadha walioshiriki kwenye taadhima za ufunguzi rasmi wa kikao cha mwaka cha 52 cha Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake (CSW). Kwenye risala ya ufunguzi, mbele ya wawakilishi wa kimataifa, KM Ban alichukua fursa ya kuanzisha kampeni ya kimataifa itakayojumuisha UM na mashirika yake yaliozagaa kote duniani, na kuchangisha serikali za Nchi Wanachama na jumuiya za kiraia, halkadhalika, kufyeka kidharura, na kwa nguvu moja, vitendo vyote vya unyanyasaji, utumiaji mabavu na udhalilishaji wa wanawake. Alisema vitendo karaha kama hivi dhidi ya wanawake havistahamiliki kamwe. ~~Sikiliza taarifa kamili kwenye idhaa ya mtandao.

KM ameanzisha rasmi kampeni ya kimataifa dhidi ya unyanyasaji wa wanawake

Asubuhi ya leo, Ijumatatu, Februari 25, KM wa UM Ban Ki-moon alianzisha rasmi kampeni ya kimataifa ya kukomesha na kufyeka tabia ya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya wanawake na watoto wa kike duniani. Kampeni ilitilia mkazo umuhimu na ulazima wa kukomesha kidharura vitendo vyote vya udhalilishaji wa kijinsia. Kampeni hii imeanzishwa siku ile ile ambapo Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake (CSW)ilipfungua rasmi, kwenye Makao Makuu ya UM, kikao cha mwaka, cha 52. Tutakupatieni taarifa zaidi juu ya Mkutano wa CSW hapo kesho. ~