Tabianchi na mazingira

IAEA inaashiria kuongezeka kwa matumizi ya umeme unaozalishwa na nyuklia katika miaka ijayo

Ripoti iliochapishwa rasmi na Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA), na kutangazwa Alkhamisi (11/09/08) ilibashiria ya kwamba matumizi ya nishati ya nyuklia duniani yataongezeka kwa mara mbili zaidi katika miongo miwili ijayo, kushinda kima cha hivi sasa, kwa sababu ya kukithiri kwa mahitaji ya nishati ulimwenguni.

Ubashiri wa hali ya hewa ni muhimu kupunguza umasikini na kutunza rasilimali ya maji

Michel Jarraud, Mkurugenzi wa Shirika la UM juu ya Upimaji wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) aliwaambia wawakilishi waliohudhuria Mkutano wa Dunia juu ya Maji unaofanyika kwenye mji wa Montpellier, Ufaransa kwamba ni muhimu kwa nchi wanachama kutumia ujuzi wa kisasa wa kutabiri hali ya hewa wakati wanapoandaa miradi ya maendeleo ya uchumi na kupunguza umaskini unaochochewa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa, hususan wanapotathminia akiba ya maji.

UNEP imenasihi ajali zisokwisha za kimaumbile zaweza kukomeshwa panapo udhibiti bora wa hali ya hewa

Achim Steiner, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) leo ametoa taarifa iliohadharisha kwamba pindi mabadiliko ya hali ya hewa yatashindwa kudhibitiwa kama inavyostahiki kisayansi, kuna hatari ya maaafa ya kimaumbile kukithiri na kuathiri kihali na mali umma wa kimataifa, kama ilivyotukia wiki hii katika mji wa New Orleans, Marekani ambapo Kimbunga Gustav kilisababisha maelfu ya watu kuhamishwa makwao na kupelekwa kwenye maeneo salama.

Mataifa ya Afrika kusaidiwa kudhibiti bora hewa safi

Benki Kuu ya Dunia imetoa ripoti maalumu yenye kumurika suala la uwezo wa Afrika kudhibiti vizuri zaidi Mradi wa Maendeleo Safi (CDM) kwa kupunguza ile hewa chafu inayomwagwa kwenye anga kutokana na harakati za viwandani na pia kutoka kwenye magari.

Ripoti ya OCHA/CARE imewakilisha orodha ya mataifa yanayohatarishwa na vurugu la kimazingira

Ripoti iliodhaminiwa na Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) pamoja na shirika lisio la kiserikali linalohudumia misaada ya kiutu la CARE imewasilisha orodha mpya ya maeneo ya kimataifa ambayo yanabashiriwa yatakabiliwa na hatari ya vurugu la kimazingira katika miongo ijayo, mathalan, ukame mbaya, mafuriko yasio kikomo na pia vimbunga vikali.

Fungamano za madhara ya mazingira na afya kuzingatiwa na mawaziri wa Afrika Gabon

Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP), kwa ushirikiano na Serikali ya Gabon wametayarisha, kwa mara ya kwanza Mkutano wa Mawaziri juu ya Fungamano za Afya na Mazingira katika Afrika utakaofanyika wiki ijayo kwenye mji mkuu wa Libreville, Gabon kuanzia tarehe 26 hadi 29 Agosti (2008).

Majadiliano ya kina yameanza Ghana kusailia mkataba wa kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa duniani

Wawakilishi 1,600 kutoka nchi wanachama 160 wamekusanyika hivi sasa kwenye mji wa Accra, Ghana kuhudhuria kikao cha wiki moja (21-27 Agosti 2008)kujadilia nidhamu za kuchukuliwa kipamoja kudhibiti bora tatizo la hewa chafu inayomwagwa angani, tatizo ambalo limethibitika kuwa ndio lenye kuharibu mazingira na kutifua mabadiliko ya kigeugeu ya hali ya hewa kimataifa. Mkutano umeandaliwa na Taasisi ya UM juu ya Mfumo wa Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (UNFCCC).

UN-HABITAT imetia sahihi makubaliano ya UM kushiriki kwenye Maonyesho ya Dunia ya Shanghai 2010

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Makazi (UN-HABITAT) yaani Anna Tibaijuka mapema wiki hii ametia sahihi maafikiano maalumu nchini Uchina yatakayoiwezesha UM na mashirika yake kadha kushiriki kwenye Maonyesho Makuu ya Dunia ya Shanghai katika 2010, maonyesho ambayo yatalenga zaidi nidhamu mpya za kuimarisha miji na maendeleo.

Yao Ming ameteuliwa Mshindi wa Kwanza wa UNEP

Mwanariadha wa Olimpiki na ambaye pia mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu kutoka Uchina, Yao Ming ametangazwa kuwa ni Mshindi wa Kwanza wa Tunzo ya Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP). Tangazo hili lilitolewa Ijumamosi kwenye mji wa Beijing.

Naibu mkurugenzi wa IAEA anazuru Iran

Naibu Mkurugenzi wa Shirika la IAEA, Olli HEINONEN, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Usalama amewasili Teheran Alkhamisi, kwa ziara maalumu ya siku mbili. Anatarajiwa kuongoza mazungumzo na maofisa wa vyeo vya juu wa Iran wanaohusika na sera za matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.~