Tabianchi na mazingira

G8 inalenga kupunguza hewa chafu kwa nusu katika 2050

Viongozi wa Kundi la G8, ambalo huwakilisha mataifa yenye maendeleo makubwa ya viwandani duniani, wameafikiana kupunguza kwa asilimia 50 umwagaji wa hewa chafu angani itakapofika 2050. Ahadi hiyo ilitolewa kwenye majadiliano yanayofanyika kwenye kisiwa cha Hokkaido, Ujapani. Maafikiano haya yanadaiwa yatasaidia udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

BK linajadilia mabadiliko ya hali ya hewa kwa nchi dhaifu

Baraza Kuu (BK) la UM linakutana kujadilia masuala yanayohusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye nchi dhaifu na masikini, hususan yale mataifa ya visiwa vidogo vidogo.

UM kuonya, rasilmali ya ardhi inaendelea kuchafuliwa, kwahitajika uangalizi bora

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limetangaza kwamba kutokana na utafiti wa miaka 20 imebainika kwamba mali ya asili ya ardhi, katika sehemu nyingi za dunia, inaendelea kuharibiwa na kuharibika kwa nguvu na kasi kubwa.

UNEP inasema uwekezaji wa nishati safi ulimwenguni ulikithiri 2007

Achim Steiner, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) ameripoti ya kuwepo uwekezaji mkubwa wa nishati zenye matumizi ya mara kwa mara katika sehemu mbalimbali za dunia, katika kipindi cha karibuni.

KM amenasihi Mataifa kuharakisha Mkataba mpya kudhibiti bora uchafuzi wa hali ya hewa

Ijumapili KM Ban Ki-moon alihutubia Chuo Kikuu cha Kyoto, Ujapani kwenye mhadhara maalumu uliokusanyisha mamia ya wanafunzi, wasomi na wawakilishi wa sekta binafsi, pamoja na jumuiya za kiraia. Kwenye risala yake KM alikumbusha juu ya umuhimu wa kuyahamasisha Mataifa Wanachama kushirikiana, kidharura, kwenye zile kadhia zitakazosaidia kufikia mapatano mapya mnamo mwisho wa 2009, kama ilivyokubaliwa naMkutano wa Bali mwaka jana.

Mjadala wa kiwango cha juu wafunguliwa Makao Makuu na ECOSOC

Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) Ijumatatu ya tarehe 30 Juni limeanzisha majadiliano ya kiwango cha juu, kitachoendelea mpaka Alkhamisi Julai 03 ambapo wanachama wa kimataifa watazingatia masuala yanayoambatana na taratibu za kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa duniani, hususan katika nchi zinazoendelea, pamoja kujadilia tatizo la muongezeko wa bei za chakula na nishati kwenye soko za kimataifa na vile vizingiti vinavyokwamisha na kuzorotisha juhudi za kusarifisha maendeleo.

Mradi wa PACE umepitishwa na Mkutano wa Bali

Wajumbe wa kimataifa waliokutana wiki hii kwenye mji wa Bali, Indonesia kuzingatia Mkataba wa Basel juu ya udhibiti bora wa taka za vifaa na zana za elektroniki wameafikiana kuanzisha mradi mpya utakaojulikana kama mpango wa PACE. Mradi wa PACE unatarajiwa kuandaa mwongozo maalumu wa kiufundi juu ya namna ya kurejeleza matumizi ya zile kompyuta zilizokwishatumika, hasa katika matengenezo madogo madogo na kwenye huduma za vipimo vya kisasa vya kompyuta, ili kutathminia matumizi ya vifaa hivyo vya elektroniki havitochafua mazingira.~

Taka za elektroniki zahatarisha afya ya umma: UNEP

Achim Steiner, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi Mazingira (UNEP)ametoa onyo linalohadharisha walimwengu ya kuwa mamilioni ya zile simu za mkononi na kompyuta zinazotupwa ovyo kwenye majaa ya kimataifa, katika sehemu mbalimbali za dunia, huhatarisha afya ya umma kijumla.

Mukhtasari wa Mkutano wa Norway kwa Wanaharakati Vijana Kutunza Mazingira

Mkutano wa Watoto wa Kimataifa wa Tunza unaofanyika kwenye mji wa Stavanger, Norway kuanzia tarehe 17 hadi 21 Juni uliandaliwa na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) pamoja na Shirika lisio la Kiserekali la Norway linaloitwa Ajenda ya [Karne ya] 21 kwa Vijana, wakichanganyika na wafadhili wengine wa kimataifa. Mkutano ulikusanyisha vijana 700 wa umri kati ya miaka 10 mpaka 14, wakiwakilisha zaidi ya nchi 100, ambao waliongozwa na watu wazima 300.

Mazungumzo na Vijana wa Afrika Mashariki juu ya Masuala ya Mazingira

Kuanzia tarehe 17 mpaka 21 Juni 2008, Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP)iliandaa mkutano mkuu wa kimataifa katika mji wa Stavanger, Norway kusailia miradi ya kuhifadhi bora mazingira ulimwenguni. Mkutano ulikusanyisha wanaharakati vijana kati ya umri wa miaka 10 mpaka 14, ambao hushiriki kwenye huduma mbalimbali za kutunza mazingira katika mataifa yao. Wajumbe 700 kutoka zaidi ya mataifa 100 walihudhuria mkutano.