Mashariki ya Kati

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon ameshtumu, kwa kauli kali, mashambulio ya mabomu yaliofanyika leo Ijumaa kwenye hoteli mbili za Jakarta (Indonesia), ambapo taarifa ya kwanza inasema watu tisa waliuawa. Taarifa ya KM kuhusu tukio hili ilielezea juu ya ushikamano wake na Serikali pamoja na umma wa Indonesia, na alisisitza kwamba anatambua juhudi thabiti za Serikali ya Indonesia katika kukabiliana na matatizo ya ugaidi, kwa ujumla. Alisema anatumai Serikali ya Indonesia itafanikiwa kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na mashambulio hayo. KM aliwatumia mkono wa taazia aila zote za waathiriwa wa mashambulio na pia kuwaombea majeruhi wapone haraka.

ICRC inazingatia udhibiti wa biashara haramu ya silaha ndogo ndogo ulimwenguni

Kwa muda wa angalau miaka kumi hivi, Kamati ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (ICRC) ilijishirikisha kwenye jitihadi za kuyashawishi Mataifa Wanachama wa UM, kwa ujumla, kubuni kanuni kali mpya zitakazotumiwa kudhibiti biashara haramu ya silaha ndogo ndogo duniani.

WHO inasema itarekibisha utaratibu wa matangazo rasmi kuhusu A(H1N1)

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti leo kwamba ongezeko la kasi la idadi ya watu wenye kuambukizwa na maradhi ya homa ya mafua ya aina ya A(H1N1), katika nchi nyingi wanachama mnamo kipindi cha sasa hivi, ni tukio lenye kutatanisha juhudi za mataifa za kuthibitisha maambukizi ya maradhi kwa raia wao, kwa kulingana na vipimo vya kwenye maabara yao ya afya.

UNCTAD inasisitza kunahitajika wizani bora kuhamasisha maendeleo katika LDCs

[Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), kwenye ripoti yake iliotolewa rasmi Ijumanne, yenye mada isemayo Ripoti ya 2009 kwa Nchi Zinazoendelea - Utawala wa Kitaifa na Maendeleo, ilihimiza serikali ziruhusiwe kuongoza majukumu ya kufufua shughuli halisi za uchumi na maendeleo kwa hivi sasa.

'Bei za chakula kwenye nchi maskini bado ni za juu sana' kuhadharisha FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limewasilisha ripoti mpya yenye kuhadharisha ya kuwa bei za chakula za ndani ya nchi, kwenye mataifa kadha yanayoendelea, zimesalia kuwa za juu sana, licha ya kuwa kimataifa bei za chakula, kijumla, zimeteremka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha karibuni, ambapo pia palishuhudiwa mavuno mazuri ya nafaka.

Mchango wa NAM ni muhimu kwa suluhu ya kimataifa, asema KM

KM Ban Ki-moon, ambaye hivi sasa yupo Misri, Ijumatano alihutubia Mkutano wa Hadhi ya Juu wa Jumuiya ya Mataifa Yasiofungamana na Madola Makuu (NAM), unaofanyika kwenye mji wa Sharm el-Sheikh.

Amani ya chakula ndio msingi wa usalama wa dunia:IFAD

Kanayo Nwanze, Raisi wa Taasisi ya UM juu ya Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwenye mahojiano aliofanya na Redio ya UM alisisitiza juu ya umuhimu wa ile rai ya walimwengu kuhakikisha kunakuwepo akiba maridhawa ya chakula duniani.

Uwezo wa kufanyiza dawa ya chanjo dhidi ya A(H1N1) ni mdogo, ahadharisha mkuu wa WHO

Imeripotiwa na UM kwamba uwezo uliopo sasa wa kutengeneza chanjo kinga dhidi ya homa ya mafua ya aina ya A(H1N1) ni mdogo na hautoweza kukidhi mahitaji ya watu bilioni 6.8 waliopo ulimwenguni sasa hivi, idadi ambayo inakabiliwa na uwezo wa kuambukizwa kirahisi na kuathirika na virusi vipya hatari vya homa hiyo.

Hapa na pale

Ad Melkert, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Iraq ameripoti kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulio ya karibuni nchini, ambapo Wakristo walio wachache walihujumiwa pamoja na taasisi zao za kidini na makundi yasiotambulikana. Alieleza hisia hizo baada ya makanisa kadha kushambuliwa Ijumapili katika miji ya Baghdad na Mosul, mashambulio yaliosababisha vifo vya watu wanne na darzeni za majeruhi. Melkert alisema "kampeni hii ya vurugu imekusudiwa kupalilia vitisho miongoni mwa makundi yalio dhaifu, na kwa lengo la kuzuia watu wa dini tofauti kuishi pamoja kwa amani, kwenye moja ya eneo maarufu miongoni mwa chimbuko kuu la kimataifa lenye kujumlisha anuwai za kidini na kikabila. Melkert alitoa mwito uyatakayo makundi husika yote, ikijumlisha Serikali ya Iraq, kuongeza mara mbili zaidi jitihadi zao za kuwapatia wazalendo walio wachache ndani ya nchi, hifadhi kinga na kuimarisha anuwai ya kidini, kikabila na kitamaduni iliopo katika Iraq kwa karne kadha wa kadha.

Hapa na pale

Siku ya Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani itaadhimishwa rasmi mwaka huu na UM mnamo Ijumamosi ya tarehe 11 Julai 2009; na mada ya safari hii inasema "Tuwekeze mchango wa maendeleo kwa masilahi ya wanawake na watoto wa kike." UM unaamini uwekezaji miongoni mwa watoto wa kike na wanawake, utakaowapatia fursa ya kipato utawafanya kuwa raia wenye uwezo na madaraka ya kuzalisha matunda yatakayochangisha pakubwa kwenye zile juhudi za kitaifa katika kufufua na kukuza uchumi wa kizalendo. Kadhalika utasaidia kuwapatia watoto wao wa kike ilimu yenye natija kimaendeleo, na kuwapa taarifa kinga juu ya afya bora, uzazi wa mpangilio na madaraka ya uhuru wa kujiamulia kimaisha.