Asia Pasifiki

Mkutano juu ya Mwito wa Durban Kupinga Ubaguzi wahitimishwa Geneva

Mkutano wa Mapitio juu ya Mwito wa Durban dhidi ya Ubaguzi, uliofanyika wiki hii mjini Geneva, Uswiss ulikamilisha shughuli zake leo Ijumaa. Kwenye mahojiano na waandishi habari wa kimataifa juu ya kikao hicho, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Bindamau, Navi Pillay alisema anaamini Mkutano ulikuwa wa mafanikio makubwa, licha ya kwamba mapatano yalikuwa magumu na yalichukua muda mrefu kukamilishwa.

Bei kuu ya chakula katika nchi masikini inaendelea kutesa mamilioni, kuhadharisha FAO

Kwenye ripoti iliotolewa na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) - yenye mada isemayo ‘Hali ya Chakula na Matarajiao ya Baadaye ya Mavuno\' - ilieleza kwamba bei ya juu ya chakula katika mataifa yanayoendelea inaendelea bado kusumbua na kuwatesa mamilioni ya umma masikini, raia ambao tangu mwanzo umeathirika na matatizo sugu ya njaa na utapiamlo, licha ya kuwa mavuno ya nafaka ulimwenguni, kwa ujumla, yameongezeka katika kipindi cha karibuni, na bei za chakula ziliteremka kimataifa, hali kadhalika.

Mkuu wa UNHCR ashtumu sera za ubaguzi dhidi ya waombao hifadhi ya kisiasa

Ijumatano, Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) aliwaambia wajumbe waliohudhuria Mkutano wa Geneva wa Mapitio ya Utekelezaji wa Mwito wa Durban Kupinga Ubaguzi Duniani, tangu kumalizika kwa Mkutano wa Awali wa Durban dhidi ya Ubaguzi miaka saba na nusu iliopita, waathirika wa mateso ulimwenguni bado wanaendelea kunyimwa hifadhi kwenye yale maeneo yenye uwezo wa kuupatia umma huo hali ya usalama.

ILO yaadhimisha miaka 90

Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) linajiandaa kuadhimisha kumbukumbu ya kutimia miaka 90 tangu kubuniwa katika kipindi ambacho walimwengu hukabiliwa na mzozo mkuu wa fedha, ukichanganyika na ukosefu wa ajira.

UNEP inatayarisha mkutano wa kuzingatia upigaji marufuku madawa 12 ya kuuwa wadudu waharibifu

Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) linatazamiwa kuandaa mkutano maalumu Geneva kusailia tatizo la afya, linalosababishwa na aina 12 za madawa yanayotumiwa kuuwa wadudu waharibifu wa mazo, madawa ya kemikali ambazo husemekana zinahatarisha afya ya wanadamu na kusababisha maradhi thakili ya saratani.

Mkutano wa UM kupinga ubaguzi waingia siku ya pili

Mkutano wa UM dhidi ya Ubaguzi wa Rangi Duniani unaofanyika mjini Geneva sasa hivi leo umeingia siku ya pili ambapo wawakilishi wa hadhi ya juu wamenedelea na mahojiano yao.

Mkutano Dhidi ya Ubaguzi waanza rasmi Geneva

Mkutano wa UM juu ya Mapitio ya Mwito wa Durban dhidi ya Ubaguzi wa Rangi Duniani umeanza rasmi hii leo mjini Geneva. Kwenye risala ya ufunguzi, KM Ban Ki-moon alieleza masikitiko juu ya uamuzi wa baadhi ya nchi wanachama, wa kutohudhuria kikao hiki, licha ya kuwa ushahidi uliopo umethibitisha dhahiri kwamba ubaguzi wa rangi ni tatizo ambalo linaendelea kuselelea, na kujizatiti katika maeneo kadha wa kadha ya ulimwengu.

IFAD inasisitiza ruzuku kwa wakulima masikini ndio ufunguo wa kuuvua ulimwengu na mzoroto wa uchumi

Kanayo Nwanzeon, Raisi wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ameyasihi mataifa yenye maendeleo ya viwanda kuharakisha misaada yao maridhawa kwa wakulima wadogo wadogo, hasa wale waliopo katika nchi masikini, ruzuku ambayo anaamini ikitekelezwa kidharura itasaidia sana kwenye zile juhudi za kuuvua ulimwengu na mzoroto wa uchumi uliotanda kimataifa sasa hivi.

Mataifa yanayomiliki viwanda vya nyuklia yakutana Beijing kusailia sera ya karne ya 21

Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) limeandaa Mkutano wa Kimataifa mjini Beijing, Uchina uliokusanyisha mawaziri 30 wa nishati pamoja na wajumbe kutoka nchi 65, kwa madhumuni ya kuzingatia matumizi ya nishati ya nyuklia kwa karne ya ishirini na moja.