Asia Pasifiki

Sera za uwekezaji kwenye nchi za G-20 zaonyesha kinaa

Ripoti ya mapitio ya Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), juu ya uwekezaji katika vitega uchumi wa kitaifa na kimataifa, imeeleza uchunguzi wao umebainisha zile nchi wanachama wa kundi la G-20 zimejizuia, kwa sasa, kuchukua hatua za dharura kudhibiti uwekezaji ndani ya nchi na katika mataifa ya nje, licha ya kuwa ulimwengu, kwa ujumla, unakabiliwa na mizozo aina kwa aina ya kiuchumi na kifedha.

DPRK imeshtumiwa na BU kwa kufanya majaribio ya makombora

Ijumatatu magharibi Baraza la Usalama (BU) lilitoa taarifa maalumu kwa waandishi habari wa kimataifa, ilioshtumu majaribio ya makombora yalioendelezwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea/Korea ya Kaskazini (DPRK) mnamo mwisho wa wiki iliopita, hali ambayo Baraza linaamini iliharamisha maazimio ya jamii ya kimataifa, na kuhatarisha usalama wa eneo pamoja na utulivu wa kimataifa.

Kamishna wa Haki za Binadamu ameshtushwa na idadi ya majeruhi na maututi katika Xinjiang

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu amenakiliwa Ijumanne akieleza kuwa ameshtushwa sana na idadi kubwa ya majeruhi na mauaji yaliotukia mwisho wa wiki iliopita, kutokana na fujo zilizofumka katika eneo la Urumqi, mji mkuu wa Jimbo la Uchina Linalojitawala la Xinjiang.

Taarifa mpya ya homa ya mafua ya A(H1N1) - Rakamu ya 58

Taarifa mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya homa ya mafua ya aina ya A(H1N1), yenye rakamu ya 58, iliotolewa Ijumatatu, tarehe 06 Julai 2009, imeeleza watu zaidi ya 94,000 walisajiliwa rasmi kuambukizwa na maradhi haya ulimwenguni, na kusababisha vifo 400 ziada.

Kamisheni ya CAC inazingatia mabadiliko ya kudhibiti kemikali zinazodhuru kwenye chakula

Kamisheni iliobuniwa bia na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), yaani Kamisheni ya CAC (the Codex Alimentarius Commission) kutathminia vipimo juu ya usalama wa vyakula, imetangaza vipimo 30 vipya vitakavyotumiwa kimataifa kuongoza ukaguzi juu ya usalama wa chakula duniani.

Matatizo ya uchumi duniani hozorotisha juhudi za kuzuwia na kutibu VVU katika nchi masikini

Tukiendelea na ripoti nyengine juu ya masuala ya uchumi wa kimataifa, Benki Kuu ya Dunia na Jumuiya Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) leo yamewasilisha ripoti ya pamoja, yenye kuthibitisha nchi 22 katika Afrika, na kwenye maeneo ya Karibian, Ulaya na Asia ya Kati pamoja na zile sehemu za Asia na Pasifiki, yatakabiliwa na misukosuko na vizingiti kadha wa kadha kwenye utekelezaji wa majukumu yanayohusu miradi ya kutibu na kuzuia maambukizi ya VVU kwa mwaka huu, kwa sababu ya mizozo ya uchumi iliopamba duniani.

KM awahimiza wajumbe wa Kundi la G-8 kuharakisha misaada, hasa kwa Afrika

Kadhalika, kwenye hotuba aliotoa Ijumatatu, mbele ya wawakilishi wa Vyeo vya Juu, waliohudhuria Mkutano wa Baraza la UM juu ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) Geneva, KM alizisihi nchi wanachama wa jumuiya ya mataifa yenye maendeleo ya viwandani, wa Kundi la G-8, kuhakarisha misaada walioahidi kuzipatia nchi masikini kwa mwaka ujao, hasa nchi za Afrika.

Ripoti ya UM inasema, mafanikio ya karibuni kufyeka njaa na umaskini yanahatarishwa na mizozo ya chakula na uchumi

"Ripoti ya UM juu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)" kwa mwaka huu, ilowasilishwa rasmi Geneva hii leo na KM Ban Ki-moon, ilitahadharisha ya kuwa mzoroto/mdodoro wa uchumi uliojiri ulimwenguni sasa hivi, na vile vile bei ya juu ya chakula ilioselelea kimataifa katika 2008, ni matukio yaliojumuika kurudisha nyuma yale maendeleo yaliopatikana miaka 20 iliopita ya kupunguza umaskini katika dunia.

UNHCR yafadhilia utafiti wa athari za KiIslam kwenye sheria ya hifadhi ya wahamiaji

Profesa Ahmed Abu al-Wafa, mtaalamu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Cairo, ameandika kitabu chenye jina lisemalo "Utafiti wa Kulinganisha: Haki ya Kupata Hifadhi na Usalama Baina ya Shari\'ah ya KiIslam na Sheria ya Kimataifa ya Wahamiaji".

IAEA imeteua Mkurugenzi Mkuu mpya

Bodi la Utawala la Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) lenye wajumbe 35, ambalo linakutana hivi sasa kwenye mji wa Vienna, Austria leo limemteua Balozi Yukiya Amano wa Ujapani kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa taasisi hii ya kimataifa.