Habari Mpya

Kesi ya Bemba itaanzishwa rasmi Aprili 2010 mjini Hague: ICC

Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) imetangaza kwesi ya Jean-Pierre Bemba itaanza kusikilizwa rasmi mwezi Aprili mwaka 2010.

Bagaragaza ahukumiwa kifungo cha miaka minane na ICTR kwa jinai ya halaiki Rwanda

Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) imehukumu kifungo cha miaka minane kwa mtuhumiwa Michel Bagaragaza, aliyekuwa mfanya biashara mkuu katika Rwanda, kwa kushiriki kwenye mauaji ya halaiki yaliotukia nchini mwao katika 1994.

Mjadala wa BK juu ya uchunguzi wa mashambulio ya Tarafa ya Ghaza waingia siku ya pili

Ijumatano Baraza Kuu (BK) la UM lilianzisha majadiliano maalumu kuhusu ripoti ya uchunguzi wa UM, uliofichua vikosi vya Israel pamoja na wapiganaji wa KiFalastina, walipatikana na hatia ya kukiuka haki za kibinadamu wakati wa mashambulio ya katika eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza mapema mwaka huu.

Wafanyakazi wa UNAMA Afghanistan watahamishiwa makazi ya muda kupata usalama

Shirika la UM la Kuisaidia Afghanistan (UNAMA) limetangaza kuwa litawahamisha baadhi ya wafanyakazi wake na kuwapeleka kwenye makazi ya muda, ndani ya nchi au nje ya Afghanistan,

Uokozi wa awali wa watoto waliotoroshwa Sudan kusini kupongezwa na UM

UM umepongeza kuokolewa watoto 28 waliotekwa nyara siku za nyuma katika Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.

Hapa na pale

Leo Alkhamisi KM Ban Ki-moon yupo njiani akirejea New York, baada ya kukamilisha ziara ya Ugiriki. Kabla ya kuondoka Ugiriki asubuhi alihutubia Bunge la Helleniki, na kuwa KM wa kwanza kihistoria kufanya hivyo. Aliwaambia wabunge wa Ugiriki kwamba ziara aliofanya Kabul, mapema wiki hii, ilimtia hamasa sana baada ya kushuhudia ushupavu na dhamana walionyesha watumishi wa UM, wanaohatarisha maisha, kuhudumia umma wa Afghanistan, na alisisitiza kazi muhimu za UM nchini humo hazitopwelewa kwa sababu ya mashambulio ya karibuni, na aliahidi zitaendelea kutekelezwa licha ya kuwepo hatari kadha wa kadha dhidi ya watumishi wa kimataifa. Vile vile KM alizungumzia kuhusu matarajio yake juu ya maafikiano kwenye majajdiliano yaudhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa. Alikumbusha majadiliano ya Copenhagen ni mazito na magumu kwa sababu hujumuisha watendaji wengi na maafikiano ya vipande vipande; na ailitilia mkazo ni muhimu kwa Mataifa Wanachama kuwa na makubaliano ya pamoja, yalio ya jumla, yenye wizani wa kuridhisha, pamoja na usawa na hukumu ya lazima.

KM azisihi serikali za kimataifa kuzingatia kikamilifu matatizo ya uhamaji

Mnamo siku ya leo, KM Ban Ki-moon ambaye yupo Athens, Ugiriki akihudhuria Mkutano Mkuu wa Tatu wa Dunia juu ya Fungamano kati ya Maendeleo na Tatizo la Uhamaji, alihadharisha kwenye hotuba yake kwamba sera zinazohusu kuruhusu wahamaji wa kigeni kuingia nchini au la, ni lazima zibuniwe kwa kutia maanani zile taarifa zenye uhakika na sio chuki na ubaguzi dhidi ya wageni.

Mtaalamu huru wa UM aihimiza Mauritania kuongeza bidii ya kufyeka milele utumwa mamboleo

UM umeripoti kwamba Serikali ya Mauritania na jumuiya za kiraia zimeshirikiana kuchukua hatua muhimu, ili kupambana na aina mpya ya utumwa mamboleo katika nchi.

Ndege za WFP zimeanzisha operesheni za kudondosha chakula Sudan Kusini baada ya mvua kali kuharibu barabara

Shirika la UM Juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeanzisha, Alkhamisi iliopita, operesheni za kudondosha, kutoka angani, misaada ya chakula inayohitajika kuhudumia watu 155,600 katika Sudan Kusini, ambapo barabara hiko zimeharibiwa na mvua kali zilizonyesha katika siku za karibuni, na kukwamisha shughuli za kusafirisha misaada ya kihali kwenye eneo.

Maendeleo muhimu yamepatikana Sudan Kusini katika upokonyaji wa silaha

Mjumbe Maalumu wa UM kwa Sudan, Ashraf Jehangir Qazi, Ijumanne, kwenye mazungumzo ya duru ya meza nchini Sudan juu ya taratibu za kuwajumuisha kwenye maisha ya kawaida wapiganaji wa zamani, alipongeza mafanikio yaliopatikana mwaka huu kwenye utekelezaji wa mradi wa kupokonya, kutawanya na kuwaunganisha na maisha ya kijamii wale wapiganaji wa zamani wanaokadiriwa 15,000, walioshiriki kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ya miaka mingi kati ya Sudan Kaskazini na Sudan Kusini.