Ray Chambers, Mjumbe Maalumu wa KM Kudhibiti Malaria, ameripotiwa kupongeza mchango wa UNICEF ambapo msaada wa dola milioni 8.5 ulitengwa makhsusi kuhudumia ugawaji wa vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa ya kuua vijidudu, katika mataifa ya Afrika yaliopo kusini ya Sahara.
Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti, kwa akali, watu 16,000 waling\'olewa makazi kwa sababu ya mafuriko katika majimbo ya Usomali ya Hiraan, Gedo na Shabelle ya Chini.
Alkhamisi jioni, Baraza Kuu la UM limepitisha azimio la kuidhinisha ripoti ya tume ya uchunguzi kuhusu ugomvi uliosababisha mashambulio yaliotukia mwanzo wa mwaka, dhidi ya eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza, ripoti ambayo iliwatia hatiani vikosi vya jeshi la Israel pamoja na wapiganaji wa KiFalastina, kwa makosa ya kukiuka pakubwa haki za binadamu dhidi ya raia.
Ijumaa alasiri KM Ban Ki-moon alihutubia Baraza la Usalama, kwenye kikao maalumu cha faragha, kuzingatia hali katika Afghanistan. Alitazamiwa kusailia hali ya usalama na kuwasilisha fafanuzi zake juu ya ziara aliifanya majuzi kwenye mji wa Kabul, Afghanistan kufuatia shambulio la magaidi dhidi ya watumishi wa UM, tukio liliosababisha vifo vya wafanyakazi watano na majeruhi tisa.
Shirika la UM juu ya Hifadhi ya mazingira (UNEP) limechapisha ripoti mpya, ilioandaliwa na wataalamu wa sheria, inayozingatia kanuni zinazohitajika kubuniwa na kuimarishwa ili kutunza mazingira, wakati wa mapigano, uhasama, vurugu na vita.
Shirika la UM la Kuisaidia Afghanistan Kurudisha Utulivu (UNAMA) Alkhamisi lilitangaza ya kuwa limeamua kuhamisha baadhi ya wafanyakazi wake, waliopo katika sehemu kadha wa kadha nchini Afghanistan, na kuwapeleka kwenye makazi ya muda ndani ya nchi, na wengine nje ya taifa hilo, kwa matarajio ya kuwapatia ulinzi unaofaa.
Shirika la UNHCR limetoa ombi maalumu linalowataka wahisani wa kimataifa kuchangisha msaada wa dharura wa dola milioni 2.8 zinazohitajika kushughulikia hatari ya mafuriko, inayowakabili watu 300,000,
Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetangaza kuingiwa wasiwasi mkubwa juu ya mapigano makali ya kikabila yalizuka wiki iliopita, kwenye jimbo la Equateur, katika JKK, juu ya haki za uvuvi.
Kikao cha mwisho, cha mashauriano, kabla ya mkutano ujao wa Copenhagen (Denmark), kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, kimekamilisha mahojiano mjini Barcelona, Uspeni hii leo hii.