Kabla ya kumaliza ziara ya siku moja mjini Washington D.C. mnamo siku ya Ijumanne, KM Ban Ki-moon alifanya mahojiano na waandishi habari, ambapo alitilia mkazo umuhimu wa kukamilisha mapatano yenye nguvu, kwenye mkutano ujao wa Copenhagen, itifaki ambayo itatumiwa kama ni msingi wa mkataba mpya wa kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa katika ulimwengu. KM alikiri, utekelezaji wa kadhia hiyo utahitajia gharama kadha wa kadha. Lakini vile vile alikumbusha ya kuwa gharama hizo hazitojumlisha fedha nyingi tukilinganisha na gharama zitakazorundikana kwa siku za baadaye, pindi walimwengu watashindwa kuchukua hatua zinazotakikana kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa kimataifa. Wabunge watatu wa Marekani walishiriki kwenye mahojiano hayo na waandishi habari, wakijumuisha Seneta John Kerry, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge juu ya Masuala ya Nchi za Kigeni, Seneta Richard Lugar na Seneta Joe Lieberman, kufuatia mkutano wa maseneta wengine na KM kuzingatia suala la mabadiliko ya hali ya hewa.