Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti nchi ziliopo kwenye Pembe ya Afrika, ambazo karibuni zilisumbuliwa na ukame wa kihistioria, hivi sasa zinajiandaa kukabilina tena na maafa mengine yanayoletwa na majira ya hali ya hewa ya El Nino, hali ambayo inatarajiwa kuzusha mafuriko makuu kwenye eneo hilo. OCHA ilitahadharisha kuna uwezekano mkubwa mataifa ya Kenya, Usomali, Tanzania na Uganda huenda yakadhurika na miporomoko ya ardhi kwa sababu ya El Nino, mfumo wa hali ya hewa unaotarajiwa pia kuathiri na kuharibu mavuno, kuzusha maradhi yanayosababishwa na maji machafu na kuharibu mitandao ya mabarabara. Kadhalika, OCHA imesema maafa hayo huenda yakadhuru vile vile mataifa ya Djibouti, Eritrea na Ethiopia. John Holmes, Mratibu wa Misaada ya Kufarajia Dharura alidhihirisha ya kuwa watu milioni 23 sasa hivi wanapepesuka, na kusumbuka, na athari za upungufu wa chakula na maji safi na salama, na vile vile wanakabiliwa na uhaba wa maeneo ya malisho ya wanyama, migogoro sugu na hali ya wasiwasi ambayo huathiri sana jamii za wakulima, wafugaji na wale wenye kuishi kwenye mitaa ya mabanda ya vitongoji vya miji mikuu, na huathiri pia wahamiaji wa ndani ya nchi na kutoka mataifa jirani."