Habari Mpya

FAO kuanzisha mashauriano ya kubuni miongozo halisi juu ya umiliki bora wa mali ya asili

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeanzisha mashauriano ya awali kihistoria, na wadau kadha wa kimataifa kusailia miongozo inayohitajika kimataifa juu ya udhibiti bora wa umiliki wa ardhi na rasilmali nyengine za kimaumbile, mathalan, maji safi, rasilmali ya uvuvi na mali ya asili ya misitu.

Ripoti ya WHO imethibitisha 'mamilioni ya vifo vya mapema huzuilika kukiimarishwa afya ya msingi'

Ripoti mpya iliochapishwa siku ya leo na Shirika la Afya Duniani (WHO) ilieleza kwamba mamilioni ya vifo vya kabla ya wakati duniani vinaweza kuzuiliwa, kwa kushughulikia mapema matatizo ya aina tano yenye kuhusu afya.

"Wakati umewadia, kuharakisha utekelezaji wa lengo la tano la MDGs, na kupunguza vifo vya uzazi", asema Mkuu wa UNFPA

Ijumatatu kwenye mji wa Addis Ababa, Ethiopia, kulifanyika Mkutano wa Wadhifa wa Juu kuzingatia maendeleo katika utekelezaji wa suala la tano la Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya kupunguza umaskini na ufukara katika mataifa yanayoendelea.

Hapa na Pale

Ijumapili alasiri, KM Ban Ki-moon ameripoti kuwa na huzuni kuu juu ya ripoti kuhusu shambulio la gari liliobeba bomu, lilioripiliwa katikati ya mji wa Baghdad, ambapo mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa. Alishtumu vikali vitendo hivi vya kutumia mabavu, kihorera, vitendo ambavyo mara nyingi huwalenga raia na hudhamiria kuchafua juhudi za kurudisha utulivu na amani katika Iraq. KM aliwahimiza umma wote wa Iraq kutunza maendeleo yao ya kisiasa yaliofikiwa nchini kwa sasa, licha ya kuwa wanakabiliwa na matukio ya vurugu la kukirihisha la mara kwa mara, na aliwasihi wasibadilishe tarehe ya kufanyisha uchaguzi ya 16 Januari 2010, na kutarajia upigaji kura utakuwa huru na wa haki.

Mahakama Maalum juu ya Makosa ya Vita katika Sierra Leone imekataa rufaa ya wahukumiwa waasi wa RUF

Hukumu ya mwisho ya Mahakama Malumu juu ya Makosa ya Vita katika Sierra Leone, imeidhinisha adhabu iliopitishwa kabla, dhidi ya viongozi watatu wa kundi la waasi la RUF, iendelee kutekelezwa kwa kulingana na makosa waliotuhumiwa nayo, ikijumlisha makosa ya kufanyisha ndoa za kulazimishwa, kitendo ambacho kilitafsiriwa kuharamisha ubinadamu, na vile vile yale makosa ya kuhujumu walinziamani wa kimataifa - na hii ni mara ya kwanza kwa mahakama za kimataifa kuchukua hatua hii ya kisheria. Mahakama ya Maalumu ya Sierra leone ilikataa kabisa maombi yote ya rufaa ya washtakiwa, isipokuwa ombi moja la mtuhumiwa Agustine Gbao, ambaye hapo kabla alishtakiwa kuendeleza adhabu za jamii, hukumu ambayo ilibatilishwa. Hata hivyo, Gbao ataendelea kutumikia kifungo cha miaka 25 gerezani.

Halaiki ya raia milioni moja ziada wang'olewa makazi kutoka maeneo ya kati na mashariki barani Afrika: OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti mnamo miezi sita iliopita, kutukia muongezeko halisi wa wahamiaji wa ndani (IDPs) milioni moja ziada katika mataifa ya Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.

Baraza la Usalama lakutana kusailia uhusiano bora wa kulinda amani Afrika kati ya UM na UA

Asubuhi ya leo, kwenye ukumbi wa Baraza la Usalama, Manaibu KM wawili juu ya Masuala ya Ulinzi Amani - yaani Alain Le Roy, anayehusika na Operesheni za Ulinzi Amani, pamoja na Susana Malcorra, anayesimamia huduma za nje za mashirika ya ulinzi amani, waliwakilisha mapendekezo yao kuhusu hatua za kuimarisha, kwa vitendo, uwezo wa vikosi vya Umoja wa Afrika, kujenga na kudumisha amani kwenye maeneo yaliojivua kutoka vipindi vya fujo na vurugu, na vile vile walizingatia taratibu za kuimarisha uhusiano bora kati ya shughuli za UM na Umoja wa Afrika.

Utekaji nyara wa mtumishi wa ICRC Darfur kulaaniwa na ofisa wa UM kwa Sudan

Mratibu wa UM juu ya Masuala ya Kiutu kwa Sudan, Ameerah Haq amelaani vikali utekwaji nyara wa mtumishi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) anayeitwa Gauthier Lefevre, mwenye uraia wa Kiingereza/Ufaransa, unyakuzi uliofanyika Alkhamisi iliopita, wakati mtumishi huyo alipokuwa anarejea nyumbani kwake Al Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi.

Hatari ya nzige Mauritania imedhibitiwa kwa akali ya kutia moyo, imeripoti FAO

Shirika la UM juu ya [Maendeleo ya] Chakula na Kilimo (FAO), limeripoti ya kuwa opereshini za kienyeji, za kudhibiti miripuko ya uvamizi wa nzige katika taifa la Mauritania, zimefanikiwa kuzuia wadudu hawa kutosambaa nchini au kuenea kwenye maeneo jirani ya mataifa ya kaskazini, na kuangamiza mazao na uwezo wa wakulima kupata riziki.

Hapa na pale

Ijumaa usiku KM Ban Ki-moon alifungua rasmi Tafrija ya Muziki kwenye ukumbi wa Baraza Kuu, kuadhimisha Siku Kuu ya UM, ambayo kikawaida, huadhimishwa kila mwaka mnamo tarehe 24 Oktoba. Mwaka huu Siku Kuu ya UM inaadhimishwa Makao Makuu tarehe ya leo kwa sababu, tarehe 24 Oktoba 2009 imeangukia Ijumamosi, ambapo maofisi huwa yanafungwa kwa sababu ya mwisho wa wiki. Mada ya taadhima za mwaka huu ina kaulimbiu isemayo "Tuwahishimu Walinzi Amani". Kwenye risala yake KM alipongeza mchango muhimu wa walinzi amani wa kimataifa, waume na wake 115,000 waliojitolea mhanga kurudisha utulivu na amani katika yale maeneo ya ulimwengu yalioambukizwa na machafuko na hali ya wasiwasi. Alikumbusha walinzi amani wa UM ni miongoni mwa "mabalozi bora kabisa" wa taasisi yetu ya kimataifa.