Tume ya Kuchunguza Ukweli juu ya Mzozo wa Tarafa ya Ghaza inatazamiwa kuwakilisha ripoti ya matokeo ya ziara ya uchunguzi wao, mbele ya wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu, Ijumanne asubuhi, mjini Geneva. Ripoti itawakilishwa na kiongozi wa tume, Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini. Wajumbe watatu wengine wa tume wataungana na Jaji Goldstone kuwasilisha ripoti yao, ikijumlisha Bi Hina Jilani, Profesa Christine Chinkin na Kanali Desmond Travers. Kadhalika, Baraza la Haki za Binadamu litasikia ripoti nyengine juu ya Ghaza kutoka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Navi Pillay, ikifuatiwa na taarifa za wawakilishi wa Falastina na Israel. Mswada wa azimio la kikaohicho umeshatayarishwa na Baraza la Haki za Binadamu, na utazingatiwa kupitishwa Alkhamisi au Ijumaa.