Habari Mpya

Waathirika wa uhasama katika JKK wafadhiliwa $7 milioni na Mfuko wa CERF kukidhi mahitaji ya kimsingi

Taasisi ya Mfuko wa UM juu ya Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF imetangaza ya kuwa itafadhilia msaada wa dola milioni 7, kukidhi mahitaji ya dharura kwa watu 250,000 waliopo kwenye majimbo yenye matatizo ya Kivu Kusini na Kaskazini.

OCHA inasema waasi wa Uganda wanaendelea kutesa raia katika JKK

Tawi la Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) iliopo Nairobi, Kenya limetoa taarifa yenye kuthibitisha waasi wa Uganda wa kundi la LRA, waliojificha kwenye maeneo ya kaskazini-mashariki, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) wanaendelea kuhujumu na kuteka nyara, pamoja na kuua raia wa katika eneo.

'Juhudi ziada zahitajika kukomesha uhamisho wa mabavu Uganda Kaskazini', aonya mtetezi wa IDPs

Walter Kaelin, Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Haki za Kibinadamu kwa wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) amenakiliwa akisema ameingiwa moyo na kufurahika kwa "maendeleo aliyoyashuhudia kuhusu utekelezaji wa mahitaji ya watu waliong\'olewa makazi, kwa sababu ya mapigano, katika Uganda Kaskazini, ambapo takriban asilimia 80 ya umma huo, unaojulimsha wahamiaji milioni 1.8, wamesharejea vijijini mwao kwa khiyari."

ICC imekabidhiwa ushahidi ziada juu ya fujo kufuatia uchaguzi uliopita Kenya

Luis Moreno-Ocampo, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) ameripotiwa kupokea wiki hii taarifa ziada kuhusu vurugu na fujo zilizozuka Kenya baada ya uchaguzi uliopita.

Hatua za dharura kwenye sekta ya afya zinahitajika Usomali kunusuru maisha ya waathirika wa mapigano na vurugu

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza kwamba mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalioshtadi nchini Usomali kwa sasa hivi, yamesawijisha na kudhoofisha sana huduma za afya pamoja na miundombinu ya kijamii, hususan kwenye maeneo ya Kati na Kusini mwa nchi.

UNCTAD inasisitza kunahitajika wizani bora kuhamasisha maendeleo katika LDCs

[Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), kwenye ripoti yake iliotolewa rasmi Ijumanne, yenye mada isemayo Ripoti ya 2009 kwa Nchi Zinazoendelea - Utawala wa Kitaifa na Maendeleo, ilihimiza serikali ziruhusiwe kuongoza majukumu ya kufufua shughuli halisi za uchumi na maendeleo kwa hivi sasa.

'Bei za chakula kwenye nchi maskini bado ni za juu sana' kuhadharisha FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limewasilisha ripoti mpya yenye kuhadharisha ya kuwa bei za chakula za ndani ya nchi, kwenye mataifa kadha yanayoendelea, zimesalia kuwa za juu sana, licha ya kuwa kimataifa bei za chakula, kijumla, zimeteremka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha karibuni, ambapo pia palishuhudiwa mavuno mazuri ya nafaka.

Hapa na pale

Ofisi ya Msemaji wa KM imeripoti kuwa Ban Ki-moon alishtushwa sana na kuhuzunishwa na taarifa alizopokea juu ya mauaji ya Zill-e-Usman, mtumishi raia wa Pakistan mwenye cheo cha juu katika Ofisi ya UM Juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), mauaji yaliotukia kwenye kambi ya wahamiaji ya Katcha Garhi karibu na mji wa Peshawar, Pakistan. Usman alishambuliwa na watu waliojaribu kumteka nyara wakati alipokuwa anatoka kwenye kambi ya wahamiaji. Alipigwa risasi kifuani mara kadha na alifariki baadaye kutokana na majeraha aliopata kwenye tukio hili. Kadhalika, mlinzi wa kambi aliuawa kwenye shambulio, na mfanyakazi mmoja raia wa UM pamoja na mlinzi mwengine walijeruhiwa. KM amelaani vikali shambulio katili hili dhidi ya watumishi wa UM waliojitolea kusimamia misaada ya kiutu kwa umma muhitaji wa Pakistan. Licha ya tukio hili, UM umeripoti utaendelea kuhudumia mahitaji ya idadi kubwa ya waathirika wa maafa Pakistan na kuwanusuru maisha. KM aliwatumia aila zote za waathirika wa tukio hili pamoja na Serikali ya Pakistan mkono wa pole.

Hapa na pale

Upande wa mashtaka, kwenye kesi ya ya mshtakiwa Thomas Lubanga Dyilo, kiongozi wa jeshi la mgambo la JKK (Union of Congolese Patriots) katika jimbo la mashariki la Ituri umeripotiwa kukamilisha kuwasilisha ushahidi wake dhidi ya mtuhumiwa, mbele ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) iliopo Hague. Lubanga ni mtuhumiwa wa awali kuwekwa rumande chini ya uangalizi wa mahakama, na kesi yake inawashirikisha, kwa mara ya kwanza katika historia ya sheria ya kimataifa, waathirika wa mashitaka wakati kesi ikiendeshwa, ikijumlisha vile vile watoto wapiganaji. Lubango ameshtakiwa makosa mawili juu ya jinai ya vita: kuandikisha na kuwaunganisha watoto wapiganaji, chini ya umri wa sheria, kwenye jeshi la mgambo la kundi lake, fungu ambalo lilioshiriki kwenye mapigano nchini baina ya Septemba 2000 mpaka Agosti 2003. Mnamo kipindi cha wiki 22, watu 28 walitoa ushahidi - ikijumuisha wataalamu watatu - umma ambao vile vile walidadisiwa na kuhojiwa na mawakiliwanaomtetea mshitakiwa. Takriban mashahidi wote wa upande wa mashitaka walipatiwa ulinzi, pamoja na hifadhi iliowakinga na mashambulio, mathalan, sauti zao zilibadilishwa wakati walipotoa ushahidi na nyuso zao hazikuonyeshwa na walipewa hata majina ya bandia kuficha utambulizi binafsi. Waathirika karibu 100 walishiriki kwenye kesi tangu kuanza kusikilizwa mnamo tarehe 26 Januari (2009).

UNOMIG yakamilisha rasmi uhamisho Georgia kufuatia kura ya vito ya Urusi

Shirika la Uangalizi wa Kusimamisha Mapigano katika Georgia (UNOMIG) limeripoti kukamilishwa, kwa leo hii, uhamisho wa waangalizi wote wa kimataifa kutoka nchini humo, kufuatia kura ya vito ya karibuni ya Urusi kwenye Baraza la Usalama, kura ambayo ilipinga rai ya UM kuongeza muda wa operesheni za kusimamia amani kwenye eneo hili.