Habari Mpya

OCHA inasema inahitaji msaada wa bilioni $4.8 kukidhi mahitaji ya waathirika maafa ulimwenguni

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti leo ya kuwa kuna upungufu wa dola bilioni 4.8 za msaada wa fedha zinazotakikana, katika miezi sita ya mwanzo wa 2009, kukidhi mahitaji ya kiutu kwa watu walioathirika na maafa.

Hali ya wasiwasi Usomali imekwamisha, kwa muda, huduma za kiutu

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), kwa kupitia msemaji wake Geneva, leo limeripoti kwamba muongezeko wa hali ya wasiwasi katika Usomali unazidisha ugumu wa uwezo wa watumishi wanaohudumia misaada ya kiutu kuwafikia waathirika wa karibuni wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Hapa na pale

Viongozi wa Tume ya Uchunguzi ya UM juu ya mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto imekamilisha ziara yake ya awali katika Pakistan Ijumaa iliopita. Wafanyakazi wa kusimamia shughuli za tume wanatazamiwa kubakia Pakistan kukusanya ushahidi zaidi, na ripoti juu ya uchunguzi wao inatarajiwa kutolewa rasmi kimataifa baada ya miezi sita.

Makundi ya upinzani Usomali yateka nyara mali za UM

Majengo mawili ya UM katika Usomali ya Baidoa na Wajid yalishambuliwa hii leo na wapiganaji wapinzani wa kundi la Al Shabaab na walichukua vifaa na magari ya UM, kwa mujibu wa taarifa iliopokelewa kutoka Ofisi ya UM katika Usomali.

Mkuu wa UNMIS ameahidiwa wanajeshi wa Sudan Kusini wataondoshwa kutoka Abyei kungojea maamuzi ya mpaka mpya

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan, Ashraf Qazi ametoa taarifa, leo hii, yenye kueleza kwamba amekaribisha ahadi ziada zilizotolewa na Chama cha NCP na kutoka lile kundi la jeshi la mgambo la SPLM, kuwa watahishimu uamuzi wa Mahakama ya Kudumu juu ya Suluhu ya eneo la mvutano, lenyo mafuta, la Abyei, au Mahakama ya PCA, ambayo inatazamiwa kutangaza uamuzi wa mgogoro wao wa mipaka Ijumatano ijayo.

Raisi mstaafu wa Ghana ameteuliwa na WFP kusaidia kukomesha njaa inayosumbua watoto

Raisi mstaafu wa Ghana, John Kufuor, ameteuliwa rasmi na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kuwa Balozi Mtetezi mpya dhidi ya Njaa Duniani.

Misaada kwa utafiti wa chanjo ya ukimwi imeteremka

Ripoti mpya kuhusu uwekezaji, kwa mwaka 2008, kwenye utafiti wa kutafuta tiba kinga dhidi ya maambukizi ya VVU, mchango huo uliarifiwa kuteremka, kwa mara ya kwanza, tangu wataalamu walipoanza kukusanya takwimu juu ya utafiti wa chanjo kinga dhidi ya UKIMWI.

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon ameshtumu, kwa kauli kali, mashambulio ya mabomu yaliofanyika leo Ijumaa kwenye hoteli mbili za Jakarta (Indonesia), ambapo taarifa ya kwanza inasema watu tisa waliuawa. Taarifa ya KM kuhusu tukio hili ilielezea juu ya ushikamano wake na Serikali pamoja na umma wa Indonesia, na alisisitza kwamba anatambua juhudi thabiti za Serikali ya Indonesia katika kukabiliana na matatizo ya ugaidi, kwa ujumla. Alisema anatumai Serikali ya Indonesia itafanikiwa kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na mashambulio hayo. KM aliwatumia mkono wa taazia aila zote za waathiriwa wa mashambulio na pia kuwaombea majeruhi wapone haraka.

ICRC inazingatia udhibiti wa biashara haramu ya silaha ndogo ndogo ulimwenguni

Kwa muda wa angalau miaka kumi hivi, Kamati ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (ICRC) ilijishirikisha kwenye jitihadi za kuyashawishi Mataifa Wanachama wa UM, kwa ujumla, kubuni kanuni kali mpya zitakazotumiwa kudhibiti biashara haramu ya silaha ndogo ndogo duniani.

WHO inasema itarekibisha utaratibu wa matangazo rasmi kuhusu A(H1N1)

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti leo kwamba ongezeko la kasi la idadi ya watu wenye kuambukizwa na maradhi ya homa ya mafua ya aina ya A(H1N1), katika nchi nyingi wanachama mnamo kipindi cha sasa hivi, ni tukio lenye kutatanisha juhudi za mataifa za kuthibitisha maambukizi ya maradhi kwa raia wao, kwa kulingana na vipimo vya kwenye maabara yao ya afya.