Habari Mpya

Siku Kuu ya Wahamiaji Duniani 2009

Ijumamosi ya tarehe 20 Juni 2009, itahishimiwa rasmi na UM kuwa ni ‘Siku ya Wahamiaji Duniani\'. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema "Mahitaji Hakika, kwa Umma Halisi".

Hali Iran inamtia wahka Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu amenakiliwa akieleza ya kuwa ameingiwa wahka juu ya ripoti alizipokea zenye kudai wenye madaraka Iran wanatumia nguvu mno kudhibiti vurugu liliozuka nchini kufuatia matokeo ya uchaguzi wa uraisi uliofanyika wiki moja iliopita.

Mkutano wa kudhibiti athari za maafa wapendekeza vifo vipunguzwe kwa nusu 2015

Mkutano wa Kimataifa Kupunguza Hatari Inayoletwa na Maafa umemalizika mjini Geneva leo Ijumaa, ambapo kulitolewa mwito maalumu unaowataka viongozi wa kisiasa katika Mataifa Wanachama kuchukua hatua za dharura kupunguza, angalaukwa nusu idadi ya vifo vinavyosababishwa na maafa ya kimaumbile itakapofika 2015, .

Idadi ya wenye njaa kukiuka bilioni 1 duniani katika 2009, inasema FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limetangaza jumla ya watu waliopo kwenye ukingo wa kubanwa na matatizo ya njaa ulimwenguni katika 2009, inakaribia watu bilioni 1.02 - sawa na sehemu moja ya sita ya idadi nzima ya watu duniani.

Mauaji ya Waziri wa Usalama Usomali yaichukiza sana jumuiya ya kimataifa

Waziri wa Usalama wa Usomali, Omar Hashi Aden, aliuawa Alkhamisi wakati akizuru mji wa Beledwenye, uliopo kaskazini ya Mogadishu na baada ya kuhujumiwa na shambulio la bomu la kujitolea mhanga liliogheshwa ndani ya gari moja kubwa.

Hapa na pale

Alain Le Roy, Naibu KM wa Idara ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM (DPKO) amezuru Abuja, Nigeria Alkhamisi ikiwa miongoni mwa maeneo anayozuru katika Afrika Magharibi. Alifanya mazungumzo na maofisa wanaohusika na masuala ya nchi za kigeni, maofisa wanaowakilisha wizara ya ulinzi pamoja na kukutana na Mshauri Mkuu wa Masuala ya Usalama wa Taifa. Vile vile alionana na Rasisi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi, Dktr Mohamed Ibn Chambas.

Kilimo hujiokoa zaidi na mizozo ya kiuchumi kushinda sekta nyenginezo, inasema ripoti ya FAO/OECD

Ripoti ya pamoja iliotolewa na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), iliowakilishwa rasmi Ijumatano, imeeleza kwamba ilivyokuwa uchumi wa kimataifa hautarajiwi kufufuka na kuota mizizi ya kuridhisha mpaka baada ya miaka miwili/mitatu ijayo, wataalamu wanaashiria mporomoko wa muda wa bei za bidhaa za kilimo kimataifa utakuwa wa wastani.

Wanariadha wa kimataifa kushiriki kwenye miradi ya kupiga vita njaa ulimwenguni

Jarno Trulli na Timo Glock, madereva wa mashindano ya mbio za gari, wenye kuwakilisha kampuni za Panasonic na Toyota, wanatazamiwa kuvalisha na kupamba gari zao na alama ya kitambulisho ya lile Shirika UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), pale watakaposhiriki kwenye mashindano ya gari Uingereza mnamo Ijumapili ijayo.

Mawasiliano ya simu za mikononi yatazamiwa kuhamasisha mapinduzi kwwenye utabiri wa hali ya hewa Afrika

Baraza juu ya Misaada ya Kiutu Duniani, na Raisi wake, KM wa UM mstaafu Kofi Annan, akijumuika na kampuni ya mawasiliano ya Ericsson, Shirika la UM juu ya Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO), na vile vile kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi, Zain, pamoja na Taasisi ya Huduma za Maendeleo Duniani ya Chuo Kikuu cha Columbia, Marekani wote pamoja wametangaza, leo hii, taarifa ya kufadhilia mradi mkuu, unaojulikana kama "Mradi wa Taarifa za Hali ya Hewa kwa Wote", ambao ukitekelezwa una matumaini ya kuwasilisha mapinduzi ya kuridhisha katika kuimarisha zaidi uwezo wa kusimamia mtandao wa utabiri wa hali ya hewa, hususan kwenye yale mazingira yanayoendelea kuathiri hali ya hewa barani Afrika.

WHO-UNICEF yasisitiza jitihadi kuu zahitajika kuhifadhi mahospitali na skuli penye maafa

Mashirika ya UM juu ya afya na maendeleo ya watoto, yaani mashirika ya WHO na UNICEF, yametoa mwito wa pamoja wenye kuzihimiza serikali za kimataifa, kuchukua hatua madhubuti, katika sehemu nne muhimu zinazohitajika kupunguza athari za maafa katika mahospitali na maskuli.