Habari Mpya

Mataifa yanajiandaa kubuni mfumo mpya wa kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa

Mkutano wa Tatu wa Dunia juu ya Udhibiti Bora wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (WCC-3) unatarajiwa kufanyika Geneva, Uswiss kuanzia tarehe 31 Agosti hadi Septemba 04, 2009.

Tiba ya majaribio dhidi ya usubi imeanzishwa rasmi katika nchi tatu za Afrika, imeripoti WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuanzisha majaribio ya tiba mpya dhidi ya maambukizi ya maradhi ya usubi, katika mataifa matatu ya Afrika - yakijumlisha Ghana, Liberia na JKK.

Uamuzi wa Tanzania kuongeza muda wa makazi kwa Waburundi wapongezwa na UNHCR

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limekaribisha uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kuruhusu muda zaidi wa kukaa nchini, kwa baadhi ya wahamiaji wa Burundi 36,000 wanaotaka kurejea makwao, kwa khiyari, kutoka kambi ya Mtabila iliopo wilaya ya Kasulu, kaskazini-magharibi katika Tanzania, kambi ambayo ilipangwa kufungwa mnamo tarehe 30 Juni 2009.

OCHA imeripoti 170,000 wahajiri Mogadishu kufuatia mfumko mpya wa mapigano

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti mapigano yalifumka tena katika wilaya za Mogadishu za Karaan na Hodan mnamo mwisho wa wiki iliopita.

Hapa na pale

KM anatarajiwa kuzuru rasmi Myanmar kuanzia tarehe 03 - 04 Julai, kwa kuitika ombi la Serikali. Atakapokuwepo huko atakutana, kwa mashauriano ya ana kwa ana, na viongozi wakuu wa Serikali ambapo wanatarajiwa kuzungumzia masuala kadha yenye umuhimu kwa UM na jamii ya kimataifa. Alitilia mkazo kwenye mazungumzo yao mambo matatu yatapewa umuhimu wa hadhi ya juu, kwa kulingana na hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa hivi sasa. Masuala hayo yanahusu, awali, kuachiwa wafungwa wote wa kisiasa, ikijumlisha Daw Aung Suu Kyi; kurudisha mazungumzo ya upatanishi kati ya Serikali na Wapinzani; na kusailia maandalizi ya uchaguzi wa taifa ulio huru na wa haki.

KM ameingiwa wasiwasi juu ya mripuko wa vurugu Honduras

KM Ban Ki-moon ametangaza taarifa ilioelezea kuwa na wasiwasi kuhusu mtafaruku uliozuka katika taifa la Honduras, la Amerika ya Kati ambapo inasemekana Raisi José Manuel Zelaya Rosales aliondoshwa madarakani kwa nguvu majuzi.

Bodi la Utawala UNCTAD kutathminia ufufuaji wa kilimo Afrika

Bodi la Utawala la Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) linatarajiwa Ijumanne jioni kukutana Geneva, kufanya tathmini kuhusu juhudi za kufufua kilimo katika bara la Afrika, huduma ambazo zimezorota katikati ya kipindi kilichopambwa na athari haribifu zilizoletwa na mizozo ya uchumi dhaifu kwenye soko la kimataifa.

Wajumbe wa Kundi la Kazi la UM kwa waliopotezwa na kutoweka wahitimisha kikao cha 88 Rabat

Wajumbe wa Kundi la Kufanya Kazi la UM juu ya Watu Waliolazimishwa Kupotea na Kutoweka baada ya kukukamilisha ziara yao ya siku nne katika Morocco walikutana kwenye mji wa Rabat na kukamilisha kikao cha 88 kilichofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 Juni walipozingatia masuala yanayohusika na watu kukamatwa kimabavu na kutoweka wasijulikane walipo.

ICRC inasema miezi sita baada ya mashambulio ya Israel Ghaza inaendelea kusumbuka na kuteseka kimaisha

Ripoti mpya ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (ICRC) iliotangazwa hii leo, inaeleza ya kuwa umma wa eneo liliokaliwa la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza, unaendelea kusumbuka na kuteseka kimaisha, miezi sita baada ya operesheni za kijeshi za Israel kuendelezwa dhidi ya eneo hili la Mashariki ya Kati.

Mkutano wa UM umepitisha ratiba mpya kupunguza athari za miporomoko ya uchumi duniani

Wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mzozo wa Uchumi na Fedha Duniani na Athari zake kwa Maendeleo, wameafikiana Ijumaa ratiba mpya ya mpango wa utendaji, utakaotumiwa na Mataifa Wanachama kipamoja, kupunguza makali na kasi ya miporomoko ya uchumi katika nchi zinazoendelea.