Habari Mpya

Mjumbe wa KM ahimiza majadiliano kuharakisha amani Darfur

Mkutano wa kuleta amani kwenye eneo la vurugu la Darfur, Sudan ulifunguliwa rasmi Ijumamosi kwenye mji wa Sirte, Libya. Katika mahojiano na waandishi habari kwenye ukumbi wa mkutano Mjumbe Maalumu wa KM kwa Darfur, Jan Eliasson alisema ya kuwa, kwa makadirio yake yeye binafsi, anaamini asilimia kubwa ya makundi husika na mgogoro wa Darfur yaliwakilishwa vizuri mkutanoni na ana matumaini mema juu ya kikao cha Sirte:~~

Juhudi za kukamilisha MDGs Tabora, Tanzania

Hivi karibuni nilizuru Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nilipatiwa fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliohusishwa kwenye huduma za utekelezaji wa ile miradi ya UM ya inayoambatana na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).

Mawaziri wanazingatia msukumo mpya kugharamia maendeleo

Mkutano wa Hadhi ya Juu ulifanyika kwenye Makao Makuu mjini New York kusailia hatua za kuchukuliwa kukamilisha maafikiano yaliopitishwa mwaka 2000 kwenye mji wa Monterrey, Mexico. Maafikiano ya Monterrey hasa yalidhamiria kuongeza ushirikiano wa kiuchumi wenye nguvu, na ulio bora, kwa umma wa kimataifa ili kupiga vita umasikini. Maafikiano ya Monterrey yalipendekeza kuzingatiwe masuala yanayoambatana na usimamizi wa kizalendo wa gharama za kuhudumia maendeleo; na kusailia taratibu madhubuti za ugawaji wa misaada ya kimataifa. ~~Sikiliza ripoti kamili kwenye idhaa ya mtandao.

Mkutano muhimu wafanyika London kuzuia vifo vya mama wazazi

Taarifa za UM zimeripoti kwamba wajumbe zaidi ya 1,800 wanaohusika na maandalizi ya sera za kitaifa, pamoja na wataalamu, wawakilishi wa mashirika yasio ya kiserekali (NGOs), wanaharakati wanaogombania haki za wanawake na vile vile watu mashuhuri kadha wa kadha kutoka nchi 100 ziada walikusanyika karibuni mjini London kwenye mkutano maalumu ulioahidi kulipa “umuhimu, wa kiwango cha juu, suala la kuboresha afya ya mama wazazi." Kadhalika wajumbe hawo waliahidi kuliingiza suala la kuboresha huduma za uzazi kwenye ajenda za miradi ya afya, kitaifa, kikanda na kimataifa.

UM waadhimisha miaka 62 tangu Mkataba kuthibitishwa

Alkhamisi, 24 Oktoba (2007) iliadhimishwa duniani kote kuwa ni ‘Siku Kuu ya Kuzaliwa UM’. Miaka 62 iliopita, mnamo tarehe 24 Oktoba 1945 Mkataba wa UM uliidhinishwa na kuanza kutumika kimataifa.

KM amewasilisha bajeti la dola bilioni 4.2 kujadiliwa na Baraza Kuu

Kadhalika Alkhamisi KM Ban Ki-moon aliwakilisha kuzingatiwa mbele ya Baraza Kuu bajeti la kuendesha shughuli za UM katika miaka miwili ijayo liliogharamiwa dola bilioni 4.2

Mjumbe wa KM kwa Darfur kuhimiza makundi yote husika kushiriki katika mazungumzo ya amani ya Sirte

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Darfur, Jan Eliasson alifanya mahojiano na waandishi habari waliopo Makao Makuu, kwa kutumia njia ya vidio, kutokea Asmara, Eritrea ambapo alidhihirisha ya kuwa hana uhakika juu ya viongozi wa makundi ya waasi na wapinzani wepi watakaoshiriki kwenye mazungumzo ya upatanishi yanayofanyika mwisho wa wiki kwenye mji wa Sirte, Libya.

Mwakilishi mpya wa KM kwa Sudan kawasili Khartoum

Ashraf Jahangir Qazi, Mwakilishi Maalumu mpya wa KM kwa Sudan, ambaye pia ni mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Amani la UM Sudan (UNMIS), amewasili Khartoum wiki hii na kutarajiwa kufanyisha msururu wa mikutano na maofisa wa ngazi ya juu wa Serikali, akiwemo vile vile Raisi wa Sudan Omar AlBashir na pia Makamu wa Kwanza wa Raisi na Raisi wa Serikali ya Sudan Kusini, Salva Kiir.

UM umeshirikiana na Sudan kuchanja watoto dhidi ya polio

Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) yakijumuika na Wizara ya Afya ya Sudan yameendeleza huduma za pamoja za kuwachanja polio watoto wachanga katika Sudan kuanzia tarehe 23 hadi 25 Oktoba.

KM ana wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa raia Kivu Kaskazini

KM wa UM Ban Ki-moon ameripoti kuingiwa wasiwasi mkuu juu ya athari kwa raia kutokana na uharibifu wa hali ya utullivu Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Taarifa alizopokea KM zilionesha kukithiri kwa mateso dhidi ya umma raia, ambapo watu huwa wanafukuzwa makwao na unyanyasaji wa kijinsia kuongezeka. Hali hii ilisababishwa na mapigano KivuKaskazini kati ya vikosi vya Serikali na makundi ya wanamgambo na wanajeshi waasi, wafuasi wa Jenrali mtoro Laurent Nkunda.~~