Habari Mpya

Tume ya Baraza la Usalama imeanza safari rasmi ya kuzuru mataifa matano Afrika

Ujumbe maalumu wa Baraza la Usalama unaoongozwa na Balozi wa Uingereza Emyr Jones-Parry pamoja na Balozi Dumisani Khumalo wa Afrika Kusini uliondoka New York Alkhamisi, tarehe 14 Juni (2007) kuanza ziara ya wiki moja kutembelea mataifa matano katika Afrika, ikiwemo Ethiopia na Sudan.

Suala la Usomali lazingatiwa tena na Baraza la Usalama

Baraza la Usalama lilikutana kwenye kikao cha faragha tarehe 14 Juni kusailia hali, kwa ujumla, katika Usomali na pia kusikiliza ripoti ya Lynn Pascoe, Makamu KM juu ya Masuala ya Kisiasa juu ya matukio ya ziara yake ya Usomali hivi majuzi ambapo pia alitembelea nchi jirani zinazopakana na taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Jedwali ya kukamilisha kesi kwa wakati imeripotiwa rasmi na ICTR

Erik Mose, Raisi wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR), ametuma ripoti kwa Baraza la Usalama inayoelezea mpango wa matarajio ya kukamilisha kesi zake kwa wakati.

ICTR yafungua mashtaka, kwa mara ya awali, kwa ushahidi wa uongo

Mahakama ya ICTR, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa, imefungua mashtaka kwa shahidi fulani aliyetoa ushahidi wa uwongo kwenye kesi ya aliyekuwa Waziri wa Ilimu wa Rwanda, Jean de Dieu Kamuhanda, ambaye alishtakiwa kushiriki kwenye mauaji ya halaiki yaliotukia nchini mwao katika 1994. Jina la mshtakiwa wa ushahidi wa uongo bado halijadhihirishwa rasmi hadharani.

UM walaani mauaji ya mhudumia misaada ya kiutu katika CAR

John Holmes, Makamu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Mshauri wa Misaada ya Dharura amelaani vikali mauaji ya Elsa Serfass mfanyakazi wa shirika linalotoa huduma bure za afya la Medecins sans Frontiere, mauaji ambayo yalitukia katika eneo la kaskazini-magharibi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

MONUC imechukizwa na mauaji ya mwanahabari wa Redio Okapi

Mwakilishi Maalumu wa KM katika JKK (DRC), William Swing ametoa taarifa yenye kulaani vikali mauaji ya Serge Maheshe mwanahabari wa Redio Okapi, steshini ambayo hudhaminiwa na UM pamoja na Shirika la Kiswiss la Taasisi ya Hirondelle.

Ukame wazusha upungufu mkubwa wa chakula Lesotho

Ripoti mpya ya Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) imedhihirisha ya kwamba khumsi moja ya idadi ya watu nchini Lesotho, yaani watu 400,000, inakabiliwa na tatizo hatari la ukosefu mkubwa wa chakula, kufuatia ukame mbaya uliotanda karibuni kwentye taifa hilila kusini ya Afrika. Kwa mujibu wa taarifa UM hali hii haijwahai kuhushudiwa kieneo kwa muda wa miaka 30 ziada. Jumuiya ya kimataifa pamoja na wahisani wa kimataifa, wamehimizwa kushirikiana kipamoja kupeleka misaada ya dharura ya kihali, na pia misaada ya chakula, kwa Lesootho na katika mataifa jirani yanayokabiliwa na tatizo la ukame mbaya ili kunusuru maisha ya mamilioni ya raia wa kusini ya Afrika.

Mwimbaji Stara Thomas wa Tanzania kutetea uzazi salama

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) imetangaza ya kuwa mwimbaji wa Tanzania, Stara Thomas, aliye maarufu katika ulimwengu unaozungumza Kiswahili, atatumia ujuzi wake wa kisanii kwa kushirikiana na UM katika huduma za kusaidia mama waja wazito nchini kwao na katika bara la Afrika kujikinga dhidi ya vifo vya katika uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Hapa na pale

Juni 14 iliadhimishwa na UM kuwa ni Siku ya Kuchangia Damu Duniani, na mwaka huu Shirika la Afya Duniani (WHO) limetilia mkazo ulazima wa mama wazazi kupatiwa damu salama, hasa ilivyokuwa kila mwaka inakadiriwa mama wajawazito nusu milioni ziada hufariki kwa sababu ya kuvuja damu kunakokithiri wakati wa mimba na wakati wa kujifungua.~

Uchambuzi wa NGOs kuhusu mijadala ya Tume ya UM juu ya Haki za Wenyeji wa Asili Duniani

Wasikilizaji, mnamo mwezi Mei, kwa muda wa wiki mbili mfululizo, wawakilishi wa jamii za wenyeji wa asili kutoka pembe mbalimbali za ulimwengu walikutana kwenye Makao Makuu ya UM na kuhudhuria Kikao cha Sita cha Tume ya Kudumu ya UM juu ya Masuala yanayohusu Haki za Wenyeji wa Asili Duniani.