Habari Mpya

Hapa na pale

Kwenye taarifa aliotoa KM Ban Ki-moon Ijumanne, kwa waandishi habari, alielezea kuvunjika moyo juu ya kuendelea kwa vitendo visio halali vya Israel, kwenye eneo liliokaliwa kimabavu la Jerusalem Mashariki, ambapo alisema nyumba za WaFalastina zilibomolewa kihorera, na aila kadha zilifukuzwa kutoka majumbani mwao, mastakimu ambayo baadaye walikabidhiwa walowezi wa Kiisraili waliojisakama, kwa nguvu, katika mitaa ya WaFalastina. Vitendo hivi, alionya KM, ni miongoni mwa mambo yenye kupalilia mazingira ya wasiwasi na kudhoofisha zaidi hali ya kuaminiana miongoni mwa makundi yanayohusika na mvutano wa Mashariki ya Kati. Aliisihi Israel kusitisha, halan, vitendo hivi vya uchokozi. Kadhalika, KM alitoa mwito ziada unaoitaka Israel kutekeleza zile ahadi ilizotoa kabla, kuhusu mapendekezo ya Ramani ya Amani juu ya Suala la Mashariki ya Kati, na kusimamisha shughuli zake zote kwenye makazi ya walowezi, ikijumlisha pia vile vitendo vya kutaka kupanua zaidi majengo yaliopo kwenye maeneo yaliokaliwa; na vile vile Israel ilinasihiwa ing\'oe haraka vituo vyote vya mbali vya uangalizi na, hatimaye, iruhusu taasisi za KiFalastina zifunguliwe baada ya kufungwa kwa kitambo, ili zianze kuendesha shughuli zake halali katika eneo la Jerusalem Mashariki.

Baraza la Usalama limepitisha ajenda ya majadiliano kwa Novemba

Leo asubuhi wajumbe wa Baraza la Usalama walikutana kushauriana juu ya ajenda ya kazi kwa mwezi Novemba.

Mvua kali Kenya zimewanyima makazi maelfu ya raia

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imechapisha taarifa iliobainisha baadhi ya maeneo katika Kenya, hivi sasa yamepigwa na mvua kubwa kabisa, yenye taathira mbaya kieneo, licha ya kuwa sehemu kubwa ya nchi babdo inaendelea kusumbuliwa na athari za ukame uliotanda kwa muda mrefu huko katika kipindi cha karibuni.

Viongozi wa kidini na wasio wa kidini wanasihiwa na KM kuhusu ulazima wa kudhibiti kipamoja taathira za mabadiliko ya hali ya hewa

Kadhalika, Ijumanne, KM Ban Ki-moon alihutubia mkusanyiko wa viongozi wa kidini na wale wasiohusiana na dini, katika Kasri ya Windsor, juu ya ulazima wa kushughulikia kipamoja matatizo yanayoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

KM ana matumaini juu ya matokeo ya Mkutano wa Copenhagen

KM Ban Ki-moon, alinakiliwa akisema anaamini itifaki muhimu itakamilishwa mwezi ujao, kwenye Mkutano Mkuu wa Copenhagen, kuhusu udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

UNHCR yapeleka misaada ya dharura kufarajia Waangola waliofukuzwa JKK

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetangaza kuwa Ijumamosi, ilituma Angola, kutoka Afrika Kusini, ndege zilizobeba shehena ya misaada ya kufarajia kihali, makumi elfu ya raia wa Angola waliorejea nchini kwao mwezi uliopita, baada ya kufukuzwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK).

Hapa na pale

Michele Montas, Msemaji wa KM aliulizwa kwenye mahojiano ya Ijumanne na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu kama kuna ukweli juu ya madai ya ripoti ya shirika lisio la kiserikali, linalochunguza utekelezaji wa haki za binadamu linaloitwa Human Rights Watch, kuhusu ukiukaji wa haki za kiutu uliofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwaka huu, ambapo wanajeshi wa brigedi ya 213 ya Vikosi vya Taifa vya FARDC walituhumiwa kushiriki kwenye “mauaji na uvunjaji sheria dhidi ya darzeni ya raia” katika eneo la mashariki la JKK. Alain Le Roy, Naibu KM juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM, anayezuru eneo la mashariki la JKK, mapema wiki hii, alinakiliwa akisema Ijumatatu kwamba Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) na jeshi la FARDC wanalazimika kuanzisha, haraka, uchunguzi juu ya madai ya ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia ulioendelezwa na wanajeshi wa taifa; na wakati huo huo alitangaza MONUC itasitisha mchango wake kwenye uenezaji na usafirishaji wa wanajeshi wa brigedi 213 ya FARDC kwenye operesheni za pamoja, ili kusubiri matokeo ya uchunguzi juu ya wanajeshi waliohusika na vitendo haramu dhdi ya raia vilivyofanyika katika eneo la mashariki la JKK. Msemaji wa KM Michele Montas aliwaambia waandishi habari wa Makao Makuu, New York kuna “ushahidi unaoaminika” kwamba wanajeshi wa FARDC walihusika na mauaji ya raia 62, ikijumlisha fungu kubwa la wanawake na watoto wadogo, yaliofanyika katika eneo la mapigano la Lukweti, kwenye jimbo la Kivu Kaskazini, baina ya miezi ya Mei na Septemba 2009. Vikosi vya MONUC katika siku za nyuma vilishirikiana na wanajeshi wa FARDC kwenye operesheni za kuwang’oa waasi Wahutu wa Rwanda waliopiga kambi katika Kivu Kaskazini.

Mgombea uraisi Afghanistan alijitoa kwenye duru ya pili ya uchaguzi ambayo anasema hairidhishi kisheria

Mgombea uraisi wa Afghanistan, Abdullah Abdullah, aliripotiwa Ijumapili kujitoa kwenye duru ya pili ya uchaguzi ilioandaliwa kufanyika tarehe 07 Novemba.

Wahalifu wanane wa makosa ya vita Sierra Leone wahamishiwa kifungoni Rwanda

Wahalifu wanane waliopatikana na hatia ya kushiriki kwenye jinai ya vita na makosa dhidi ya utu, na Mahakama Maalumu juu ya Makosa ya Vita katika Sierra Leone (SCSL), Ijumaa walisafirishwa kutoka vituo vya kufungia watu viliopo Freetown, Sierra Leone na kuhamishiwa kwenye Jela ya Mpanga, iliopo Kigali, Rwanda, kutumikia adhabu yao. Mahakama ya SCSL, inayoungwa mkono na UM, iliamua kuwapeleka wafungwa hawo wanane Rwanda kwa sababu magereza ya Sierra Leone hayatoshelezi viwango vya sheria ya kimataifa.

UM umeanzisha mradi mkuu wa kusambaza vifaa vya kusajili wapiga kura Sudan

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS) na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) yameanzisha operesheni kuu, za kugawa vifaa vya uchaguzi vitakavyotumiwa kusajilia wapiga kura kuanzia Ijumatatu ya leo.