Habari Mpya

KM asihi UA juu ya umuhimu wa mioundombinu kuimarisha maendeleo

Ifuatayo ni taarifa fupi juu ya risala ya KM Ban Ki-moon, alioiwasilisha mbele ya viongozi waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika unaofanyika sasa hivi katika mji wa Addis Ababa, Ethiopia.

Makundi yanayohasimiana Sudan Kusini yaombwa yasimamishe mapigano, haraka

KM Ban ametoa mwito maalumu kwa Serikali ya Sudan na kundi la waasi la JEM kusimamisha, halan, shughuli zote za mapigano katika Darfur Kusini, na kuonya juu ya hatari inayoletwa na mapambano yao, kuhusu usalama wa raia. UM umepokea taarifa zenye kuonyesha kuwepo muongezeko wa vikosi vya Serikali na waasi kwenye eneo la karibu na Muhajeria, Sudan Kusini.

ICTR imethibitisha tena kifungo cha maisha kwa mtuhumiwa Karera

Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) imethibitisha tena kifungo cha maisha kwa mtuhumiwa François Karera, ambaye mnamo 07 Disemba 2007 alipatikana na hatia ya kushiriki kwenye mauaji ya halaiki, pamoja na maangamizi dhidi ya raia wenye jadi ya Kitutsi katika sekta ya Nyamirambo, wilaya ya Kigali Ville, na mauaji katika Kanisa la Ntarama mnamo 15 Aprili 1994, na pia kushiriki kwenye jinai dhidi ya utu iliofanyika katika kijiji cha Rushahi, kwenye Wilaya ya Kigali.

Hapa na Pale

Shirika la UM Linalosimamia Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limetangaza taarifa yenye kufafanua, kinaganaga, kwamba haitoshiriki kamwe, kwenye shughuli za aina yoyote au kujihusisha na operesheni zinazoambatana na Bosco Ntangada, kiongozi wa kundi la wanamgambo katika JKK. MONUC ilikumbusha ya kuwa Ntangada sasa hivi ameshtakiwa na Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) kwa makosa ya vita, ikijumlisha jinai ya kuajiri kimabavu watoto chini ya umri wa 15, waliolazimishwa kushiriki kwenye mapigano na uhasama.