Habari Mpya

Mahojiano na Armando Swenya wa SAHRiNGON, Tanzania

Armando Swenya anfanya kazi na shirika la SAHRiNGON, kumaanisha \'Southern Africa Human Rights and Geonetwork, Tanzania Chapter\' au kwa Kiswahili ni Shirika la Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu, kusini mwa Africa, Tawi la Tanzania. Kwenye mahojiano yafuatayo anazumgumzia namna shirika lao linavyohudumia na kuelimisha umma juu ya haki za binadamu. ~

Mazungumzo na Tabibu wa Hospitali ya Muhimbili, Tanzania kuhusu udhibiti bora wa UKIMWI

Takwimu mpya za Taasisi ya UNAIDS na Shirika la Afya Duniani (WHO)zimethibitisha kwamba katika kipindi cha sasa karibu watu wazima milioni 33.2 na watoto milioni 2.7 chini ya umri wa miaka 15 wanaishi na virusi vya UKIMWI (VVU). Lakini, kwa bahati mbaya watu wanaoishi na VVU mara nyingi hutengwa na kufedheheshwa na jamii zao kwa sababu ugonjwa huo huambatanishwa na tabia na vitendo visivyolingana na tamaduni za kijadi. Kwa hivyo umma huu hujikuta wanabaguliwa na kunyimwa haki zao za kimsingi.

Kongamano maalumu DSM lasailia matumizi ya Kiswahili fasaha katika vyombo vya habari

Hivi karibuni mjini Dar es Salaam, Tanzania kulifanyika Mkutano wa Kimataifa wa Idhaa za Kiswahili ambapo kulisailiwa taratibu za kuchukuliwa kipamoja kueneza matumizi sahihi, sanifu na fasaha ya lugha ili kujenga mazingira mapya ya utangazaji. Kongamano hili liliandaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)na kuhudhuriwa na mashirika kadha ya redio na televisheni, ikiwemo pia Idhaa ya Redio ya Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa wa BAKITA, Suleiman Hegga, moja ya maazimio yaliopitishwa ni lile pendekezo linalotilia mkazo umuhimu wa kupunguza makosa ya utumiaji wa Kiswahili kisicho sahihi katika utangazaji, tatizo liliochipuka katika kipindi cha karibuni baada ya kukithiri kwa wadau wa lugha ya Kiswahili, ndani na nje ya Afrika ya Mashariki. Kwenye kipindi, tumeandaa mahojiano na Mwenyekiti Hegga ambaye anafafanua umuhimu wa idhaa zinazotumia Kiswahili kuimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu.

UM yanuia kukomesha karaha ya utumiaji mabavu dhidi ya wanawake

KM wa UM Ban Ki-moon aliwasilisha risala maalumu, na muhimu, kwenye taadhima za kuiheshimu Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumiaji Mabavu dhidi ya Wanawake. Jumuiya ya Kimataifa iliafikiana kuitambua tarehe 25 Novemba, kila mwaka, kuwa ni siku kuuzindua umma wa dunia juu ya jukumu kuu, na tukufu, la kupiga vita, kipamoja, vitendo karaha vya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya watoto wa kike na wanawake.

Hatua za dharura zinatakikana kuondoa mtego wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa dhidi ya masikini duniani

Ripoti ya Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP)iliowasilishwa mbele ya waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu, na mtaalamu wa takwimu, Claes Johansson ilibainisha kwamba wanaoumia, na kuathirika zaidi kihali na mali, kutokana na uchafuzi wa mazingira duniani ni lile fungu la umma wa kimataifa ambalo halihusiki kamwe na uharibifu huo

Manadalizi ya vikosi mseto vya UM/UA katika Darfur yasonga mbele

Kundi la kwanza la wahandisi wa kijeshi 135 kutoka Uchina wamewasili karibuni mjini Nyala, katika Darfur Kusini, wakijumuisha furushi la mchango wa UM kusaidia Operesheni za Umoja wa Afrika za AMIS katika Darfur. Vikosi hivi vya Uchina vitahudumia kazi muhimu ya kutayarisha makazi kwa vikosi mseto vya ulinzi wa amani vya UM na UA vya UNAMID.

John Holmes, Mkuu wa OCHA ameanza ziara ya siku tisa Afrika

Naibu KM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes ameanza ziara ya siku tisa Afrika na alitazamiwa kuzuru Ethiopia, Sudan na Kenya. Holmes atakutana kwa mashauriano na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayohudumia misaada ya kiutu pamoja na maofisa wa UM, na pia wanadiplomasiya waliopo kwenye nchi anazozuru kushauriana juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa shirika, ili kuwanusuru kimaisha mamilioni ya watu walioathirika kihali kutokana na mifumko ya vurugu liliotanda kwenye maeneo yao katika siku za karibuni.

Mkuu wa UNDOC ahimiza hatua za haraka kupambana na wizi wa watoto Afrika

Antonio Maria Costa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Uhalifu na Madawa ya Kulevya (UNDOC) amezihimiza serekali za Afrika ya Magharibi na Kati kuongeza huduma za usalama zinazohitajika kuwakinga watoto dhidi ya hatari ya kutekwa nyara na baadaye kuuzwa kwenye soko la kimataifa kuhudumia utumwa mamboleo.

UM umechapisha kitabu cha mwongozo kusaidia vijana wa vijijini Afrika

Mashirika mawili ya UM yanayohusika na chakula na kilimo, FAO, na miradi ya chakula duniani, WFP yamechapisha kitabu kipya cha mwongozo kuwasaidia vijana walioathiriwa na UKIMWI/VVU katika mataifa ya Afrika kusini ya Sahara kuanzisha skuli za ukulima za kuilimisha watoto mayatima ufundi na ujuzi wa ajira ya kudumu. Mafunzo haya vile vile yatwasaidia vijana wanaoishi vijijini Afrika kupata uzoefu wa kudhibiti bora akiba ya chakula kwa muda mrefu, hasa ilivyokuwa wanakabiliwa hivi sasa na mazingira magumu ya kimaisha.

Mtaalamu wa haki za binadamu anakhofia upungufu wa uhuru wa dini Angola

Asma Jahangir, Mkariri Maalumu anayehusika na masuala ya uhuru wa dini na itikadi alizuru Angola karibuni kwa wiki moja. Baada ya kumaliza ziara yake Jahngir aliripoti kwamba licha ya kuwa katiba ya taifa inaruhusu uhuru wa kuabudu na kufuata itikadi za dini mbalimbali kwa raia, aligundua kwamba baadhi ya vikundi vya Kikristo pamoja na jamii ya Kiislamu katika Angola bado wanaendelea kubaguliwa kisheria.