Habari Mpya

Mahakama ya ICTR yaamua hukumu iliopita iendelezwe kwa watuhumiwa watatu

Korti ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) imeidhinisha kuendelzwa ile hukumu iliotolewa kabla dhidi ya watu watatu waliokuwa wakurugenzi wa vyombo vya habari Rwanda katika 1994, ambao walituhumiwa kuchochea mauaji ya halaiki dhidi ya raia wenye asili ya KiTutsi.

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Maendeleo ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limewasilisha ripoti mpya yenye kuthibitisha maendeleo ya kutia moyo katika miaka 10 iliopita ambapo idadi ya watoto wanaohudhuria skuli za msingi iliongezeka, hususan miongoni mwa watoto wa kike, na pia kuliongezeka kwa fedha zinazotumiwa kimataifa katika sekta ya ilimu, licha ya kuwa ilimu ya watu wazima bado iliendelea kuzorota takriban duniani kote.

Siku ya Kuimarisha Haki kwa Watoto Duniani.

Tarehe 20 Novemba kila mwaka huadhimishwa na Mataifa Wanachama kuwa ni siku ya kukumbushana jukumu adhimu lilioikabili jumuiya ya kimataifa la kuwatekelezea watoto haki zao halali. Tangu mwaka 1989, pale Baraza Kuu la UM lilipoidhinisha Mkataba juu ya haki za Mtoto, umma wa kimataifa ulijitahidi sana kuwatekelezea watoto haki zao za kimsingi. Lakini maendeleo yaliopatikana yalikuwa haba sana na hayakuridhisha kikamilifu, hususan katika utekelezaji wa haki hizo kwa wale watoto wanaojikuta wamenaswa kwenye mazingira ya uhasama na mapigano.~~ Sikiliza ripoti kamili juu ya suala hili, kwenye idhaa ya mtandao, kutoka A. Aboud wa Redio ya UM.

Kongamano la kusailia mazingira mapya ya utangazaji wa idhaa za Kiswahili duniani

Hivi karibuni katika mji wa Dar es Salaam, Tanzania kulifanyika kongamano maalumu la Idhaa za Kiswahili Duniani lilioandaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)kwa lengo la "kujenga mazingira mapya ya utangazaji."

Raia wa Afrika Kusini kuongoza operesheni mseto za polisi Darfur

Michael J. Fryer wa Afrika Kusini ameteuliwa rasmi na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), baada ya kushauriana na KM wa UM Ban Ki-moon, kuwa Kamishna wa Polisi wa operesheni mseto za ulinzi wa amani katika Darfur. Operesheni hizi zitaendelezwa shirika kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika (UM/UA), na kuongozwa na Shirika la UNAMID.

Waalimu wa kazi za polisi wa UM wapelekwa Chad

Kundi la mwanzo la maofisa watano wa polisi kutoka Kitengo cha UM kinachohusika na Ujenzi wa Huduma za Dharura za Polisi (SPC) limepelekwa Chad wiki hii kuanzisha mafunzo maalumu ya polisi wa kuhudumia ulinzi na usalama wa wahamiaji wa ndani ya nchi 300,000 pamoja na wahamiaji wa kutoka eneo jirani la Darfur, Sudan walioathiriwa na hali ya mapigano.

Mjumbe Maalumu mpya wa KM kwa Cote d'Ivoire ameanza kazi

Mjumbe Maalumu mpya wa KM kwa Cote d’Ivoire, Choi Young-Jin amewasili nchini humo mapema wiki hii kuanza kazi. Choi ameahidi kushirikiana na makundi yote ya kisiasa yanayoanmbatana na mgogoro wa Cote d’Ivoire, bila ya upendeleo, ili kuhakikisha amani inaimarishwa nchini pote kwa masilahi ya umma kijumla.

Hali Usomali inawatia wasiwasi mkubwa wajumbe wa Baraza la Usalama

Baada ya mashauriano kukamilishwa ndani ya Baraza la Usalama juu ya hali katika Usomali, Balozi Marty Natalegawa wa Indonesia, Raisi wa Baraza kwa mwezi Novemba, aliwasilisha kwa waandishi habari taarifa ya pamoja, kwa niaba yawajumbe wa Baraza yenye kuelezea wasiwasi mkuu ulioivaa jamii ya kimataifa juu ya kuharibika kwa hali ya kisiasa, usalama na vile vile mazingira ya kiutu nchini Usomali.

Demokrasia inaanza kushika mizizi DRC, asema KM Ban

Katika ripoti ya UM iliowasilishwa karibuni kusailia hali katika JKK (DRC) KM Ban Ki-moon alithibitisha kwamba usalama wa taifa uliathiriwa nchini na haki za binadamu ziliharamishwa kwa sababu ya kuzuka migogoro miwili; kwanza, uhasama uliochipuka, baada ya kufanyika uchaguzi, baina ya serikali na wafuasi wa Makamu Raisi wa zamani, Jean-Pierre Bemba na, pili, mikwaruzuano ilioselelea kieneo kati ya Jeshi la Taifa na wanajeshi waasi, ambao huongozwa na Jenerali aliyetoroka jeshi Laurent Nkunda.

Burundi yapongezwa na UM kwa kuunda serikali mpya

Ofisi ya UM Inayosimamia Huduma za Amani Burundi (BINUB) pamoja na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa waliopo nchini humo wamepongeza maafikiano ya karibuni ya wanasiasa kwa mchango wao uliowezesha serekali mpya kuundwa, pamoja na kiongozi wa nchi kuteuliwa. Viongozi wote wa Burundi wamenasihiwa na UM kuchukua hatua zote muhimu ili kuhakikisha demokrasia inaimarishwa na kudumishwa kwenye taifa lao.