Habari Mpya

Mkataba wa Haki za Watu Walemavu Duniani

Katika makala iliopita, iliwakilisha sehemu ya kwanza ya mazungumzo kati ya Redio ya UM na Maalim Khalfan Hemed Khalfan, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Watu Walemavu Zanzibar (UWZ)ambapo alielezea juu ya mataifa 80 ziada yalioridhia kutia sahihi Mkataba mpya wa Haki za Walemavu Duniani, yakijumuisha mataifa ya Afrika Mashariki ya Kenya, Tanzania na Uganda. Kadhalika, Maalim Khalfan alielezea umuhimu wa kuwepo ushirikianao wa kipamoja kati ya mataifa kwenye utekelezaji wa mapendekezo ya Mkataba huo, kwa sababu, alikumbusha, sio Mataifa yote Wanachama yenye uwezo au nyenzo za kuzitekeleza haki za kimsingi za watu walemavu. Halkadhalika, alitupatia dokezo juu ya tafsiri ya mtu mlemavu, kama inavyotafsiriwa na Mkataba, na alifahamisha fungamano ziliopo za kisheria zinazoyawajibisha mataifa yaliouridhia na kuuidhinisha Mkataba kuwatekelezea watu wenye ulemavu haki zao.

WHO yaonya uchafuzi wa hewa ya majumbani unakandamiza afya

Shirika la Afya Duniani (WHO) limewasilisha ripoti inayosema asilimia 5 ya jumla ya vifo vinavyotukia ulimwenguni sasa hivi, kwenye mataifa 21 yanayoendelea, husababishwa na nishati ngumu inayotumiwa kwa kupikia na kueneza joto ndani ya majumba. Kwa mujibu wa WHO, matumizi ya nishati ngumu – kama vile makaa, kuni, vinyesi na mabaki ya mimea – ni moja ya matishio makubwa 10 yanayohatarisha afya ya jamii kijumla.

Mkuu wa DPI anaripoti sera mpya mbele ya COI

Makamu-KM Kiyotaka Akasaka, mkuu mpya wa Idara ya Habari kwa Umma ya UM (DPI) aliwakilisha sera mpya ya taasisi yake mbele ya wajumbe wa kimataifa waliohudhuria kikao cha ufunguzi cha Kamati ya Habari, au Kamati ya COI. Alisema sera na ratiba mpya ya kazi na shughuli za DPI, chini ya uongozi wake, zitayapa umuhimu, na umbele zaidi masuala manne yanayohusu huduma za usalama na amani ya kimataifa, mabadiliko ya hali ya hewa, maendeleo ya kiuchumi na jamii, na utekelezaji wa haki za binadamu.~

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani

Tarehe 03 Mei huadhimishwa kila mwaka na jamii ya kimataifa kuwa ni ‘Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani’. Ujumbe wa risala ya KM Ban Ki-moon kuiheshimu siku hii, mwaka huu, ulitilia mkazo umuhimu wa kuzingatia, na kutafuta suluhu ya kuridhisha, inayotakikana kuwakinga waandishi habari dhidi ya taathira mbaya wanazokumbana nazo katika kutekeleza kazi zao.

Kamisheni ya CSD imeanzisha mjadala wa mwaka Makao Makuu

Kamisheni ya Baraza Kuu juu ya Maendeleo ya Kudumu (CSD), mnamo tarehe 30 Aprili (2007)imeanzisj kika cha mwaka kwenye Makao Makuu ya UM, ambapo wajumbe 2000 ziada, wakiwakilisha mataifa wanachama pamoja na wataalamu kadha kutoka kanda mbalimbali za kimataifa, walijiandaa kuzingatia suluhu ya muda mrefu kuhusu tatizo la nishati, kwa matarajio ya kukuza maendeleo ya, hasa, mataifa masikini, ikiwa miongoni mwa juhudi za kuyapunguzia mataifa yanayoendelea athari za kiuchumi na jamii kutokana na umwagaji wa hewa chafu angani.

Hali Usomali inaendelea kuharibika

Wataalamu 12 wa UM wametangaza, hadharani, taarifa ya pamoja iliodhirisha wasiwasi wao mkubwa juu ya athari za uhasama uliofumka karibuni kwenye mji wa Mogadishu, Usomali, ambapo mamia ya watu waliuawa na mamia elfu ya raia kulazimika kuhajiri makazi.

ICC yatoa hatia ya kukamata watuhumiwa wa jinai ya Darfur

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Halaiki (ICC) imetoa hati ya kuwakamata Ahmed Muhammad Haroun, Waziri wa Masuala ya Kiutu katika Sudan na vile vile kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed, Ali Muhammad Al Abd-Al-Rahman baada ya kutuhumiwa na Mahakama kuwa wanahusikana na jinai ya vita na kushiriki kwenye vitendo vilivyokiuka utu katika eneo la Darfur.

Kikao maalumu Libya kusailia mzozo wa Darfur

Jan Eliasson, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Darfur alihudhuria kikao maalumu kilichoandaliwa na Libya majuzi kuzingatia hali katika Darfur. Kwenye kikao hicho walijumuika wawakilishi kutoka Sudan, Chad, Misri, Eritrea na pia Libya, Uchina, Ufaransa, Uingereza, Marekani, Kanada, Uholanzi, Norway na pamoja na wajumbe waliowakilisha Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Nchi Huru za Kiarabu. Wawakilishi wote hawa waliafikiana juu ya ulazima wa kuharakisha suluhu ya jumla, na ya kudumu, kuhusu vurugu la Darfur.

Vikwazo vya almasi Liberia kuondoshwa na Baraza la Usalama

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Liberia, Alan Doss amepongeza uamuzi wa karibuni wa Baraza la Usalama, wa kuondoa vikwazo dhidi ya biashara ya kuuza almasi kutoka taifa hili la Afrika Magharibi.

UM imenuia kudumisha amani Cote d'Ivoire

Shirika la UM linalosimamia Huduma za Amani Cote d’Ivoire (UNOCI) majuzi liliongoza rasmi sherehe za kuwajumuisha kwenye brigedi mbili za jeshi la taifa wale raia waliokuwa waasi wakati uhasama wa wenyewe kwa wenyewe uliposhtadi siku za nyuma nchini mwao.