Habari Mpya

Siku ya Kufyeka Malaria Afrika

Wiki hii, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kurudisha Nyuma Malaria imewasilisha mradi mpya wa kufadhilia huduma za kupiga vita maradhi ya malaria Afrika. Jumuiya hiyo inatumai kwamba nusu ya maombi yote ya yale mataifa yanayohitajia msaada huo yatatekelezewa mataifa husika, hususan katika bara la Afrika, eneo ambalo, kila mwaka, asilimia 90 ya vifo milioni 1 vya malaria hutukia.

Vurugu la Usomali limefurutu ada, na ni la hatari mno

Ijumanne, Makamu KM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes aliripoti mbele ya Baraza la Usalama kwamba hali ya mapigano nchini Usomali kwa sasa ni mbaya sana, hususan kwenye mji wa Mogadishu. Holmes aliirudia tena taarifa hii pale alipokutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu:~

Balozi wa Kenya azingatia mkataba mpya dhidi ya silaha ndogo ndogo

Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika UM, Balozi Zachary Muburi-Muita alifanya mahojiano na Redio ya UM ambapo alizungumzia, na kuzingatia yale mapendekezo ya baadhi ya wanadiplomasiya wa kimataifa - akiwemo pia Kamishna Mkuu Mstaafu wa Haki za Binadamu, Mary Robinson - ya kuanzisha kampeni ya kubuni chombo kipya cha sheria ya kimataifa ili kudhibiti bora biashara ya silaha ndogo ndogo ulimwenguni.

Sudan kupatiwa msaada wa ngano wa dola miloni mbili kutoka Urusi: imeripoti WFP

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), limepokea kutoka Urusi, msaada wa ngano, wa dola milioni 2, uliokusudiwa kufufua tena zile operesheni za kuwapatia chakula watoto wa skuli muhitaji karibu 300,000 waliopo kwenye majimbo matatu ya Sudan yaliokabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

UNHCR itapanua operesheni zake Darfur Magharibi

Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) baada ya kumaliza ziara muhimu katika kambi za wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs), katika Sudan wiki hii, aliripoti kuwa amefikia maafikiano, na Serekali ya Sudan, yanayoruhusu kupanuliwa shughuli za UNHCR katika eneo la Darfur Magharibi.

Naibu KM azuru DRC kuimarisha amani

Naibu KM Asha-Rose Migiro wiki hii alifanya ziara ya siku tatu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC). Alipokuwepo huko alikutana kwa mazungumzo, na pia mashauriano, na Raisi Joseph Kabila pamoja na viongozi kadha wengine wa kisiasa, wakijumuisha vile vile wanasiasa wa kutoka vyama vya upinzani.

WFP imeanzisha operesheni za kuhudumia waathiriwa wa kimbunga Bukini

Shirika la WFP limeanzisha misafara ya ndege, za kupeleka chakula na misaada ya dharura inayohitajika kuwahudumia kihali maelfu ya watu wanaoishi kaskazini-magharibi ya Bukini, eneo ambalo hivi karibuni lilichafuliwa vibaya na kimbunga kilichoharibu vibaya sana barabara na madaraja.

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon aliwanasihi wajumbe wa kimataifa waliohudhuria Kikao cha Saba juu ua Demokrasia, Maendeleo na Biashara Huru, kilichofanyika Doha, Qatar kuhakikisha duru yao ya mazungumzo itawasilisha mafanikio ya kuridhisha, maana bila ya kuyafannya hayo, alionya, nchi masikini zitaporomoka zaidi kimaendeleo, hali ambayo anaamini itafumsha mitafaruku na kueneza hali ya wasiwasi kwenye mfumo mzima wa biashara katika soko la kimataifa.~

Mkataba wa Haki za Watu Walemavu Duniani Kuridhiwa Kimataifa (Sehemu ya Kwanza)

Mnamo mwisho wa mwezi Machi, Mataifa Wanachama 81 pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) walijumuika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UM) kutia sahihi mkataba mpya wa kihistoria, uliokusudiwa kuboresha maisha ya watu milioni 650 walemavu duniani na kuwatekelezea haki zao za kimsingi kama inavyostahiki. Mkataba huu, kwa ujumla, unakataza na kupiga marufuku, ubaguzi wa aina yoyote, katika sehemu zote za jamii dhidi ya watu walemavu.

Sudan imekubali furushi la ulinzi wa amani kwa Darfur

Serekali ya Sudan wiki hii ilituma barua kwa Baraza la Usalama ilioelezea kukubali kupelekwa katika Darfur helikopta zitakazotumiwa na vikosi vya mseto vya AU na UM katika shughuli za kuimarisha usalama na amani kwa raia wa jimbo la magharibi la Sudan la Darfur.