Mnamo mwaka 2007 UM ulikabiliwa na matatizo kadha wa kadha yaliohitajia suluhu ya pamoja, kutoka jamii ya kimataifa, kwa UM kufanikiwa kulinda usalama na amani na kuimarisha maendeleo ya uchumi na jamii yatakayokuwa na natija kwa umma pote duniani.
KM wa UM Ban Ki-moon aliripotiwa akisema kama alishtushwa na kughadhibiwa, halkadhalika, baada ya kuarifiwa kwamba kiongozi wa Chama cha PPP, na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto, aliuawa Alkhamisi kwa bomu la kujitolea mhanga.
Shirika la UM juu ya Operesheni za Amani Mipakani Ethiopia na Eritrea (UNMEE) limeripoti kuwa na wasiwasi kuhusu utulivu wa mipaka kwenye Eneo la Usalama wa Muda (TSZ), baada ya kutukia mashambulio ya risasi karibuni katika Tsorena, eneo iliopo upande wa Eritrea.
Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah amesema ameshtushwa na utekaji nyara wa wafanyakazi wawili wa shirika la madakatari, lisio la kiserekali la Medecins Sans Frontieres (MSF) uliojiri karibuni katika mji wa Bosasso, Puntland.
Ofisi ya UM inayohusika na Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba majambazi bado wanaendelea kuhujumu wafanyakazi wa kimataifa wanaohudumia misaada ya kiutu katika sehemu kadha nchini Chad, hali ambayo inazorotisha zile juhudi za kuitekeleza kadhia hiyo umma muhitaji.
UM umepongeza uamuzi uliofikiwa karibuni na Serikali ya JKK pamoja na wakazi wa majimbo ya Kivu Kusini na Kaskazini kuitisha Mkutano wa Kuzingatia masuala ya Amani, Usalama na Maendeleo katika eneo lao lenye matatizo.
Kikundi Kazi cha Baraza Kuu kinachosimamia juhudi za kukomesha na kufyeka ukandamizaji wa kijinsia, na unyayanyasaji miongoni mwa watumishi wa UM, wamepitisha azimio muhimu karibuni litakalowahakikishia waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia kuwa wanapatiwa tiba maridhawa, ushauri, misaada ya jamii na vile vile msaada wa kisheria.
Raisi wa Baraza Kuu Srgjan Kerim alipokutana na waandishi habari wa kimataifa, hapa Makao Makuu, wiki hii, kuzingatia kikao cha mwaka cha 62, alibainisha matukio ya kutia moyo.
Hivi majuzi, Baraza Kuu la UM lilifanyisha kikao makhsusi cha siku tatu, kilichokuwa na lengo la kufuatilia utekelezaji wa nchi wanachama wa zile ahadi zilizopendekezwa mwaka 2002 kwenye mkutano mkuu wa UM, ambapo kulipitishwa ‘mpango wa utendaji’ wa kujenga mazingira salama yatakayotunza haki na maisha bora kwa watoto wote, pote ulimwenguni. Mpango huo ulipewa muktadha usemao “Ulimwengu Unaostahili Kuishi Watoto kwa Utulivu na Amani.”
Mapema wiki hii, mnamo tarehe 17 Disemba, watumishi wa UM walijumuika kote duniani kuwakumbuka wenziwao 17 waliouawa na shambulio la magaidi liliotukia Disemba 11 kwenye ofisi za UM mjini Algiers, Algeria. Wafanyakazi wa UM walikaa kimya kwa dakika moja kuheshimu kumbukumbu za wenziwao waliofariki Algiers.