Ili kupunguza upotevu wa chakula, zana za AI zinapima chakula kilichotupwa na kuboresha ununuzi na maandalizi ya chakula katika hoteli - Michael Muratha, UNEP
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) linaimarisha juhudi za kukabiliana na upotevu na utupaji wa chakula kupitia teknolojia bora za uhifadhi, usambazaji wa chakula kilichozidi na matumizi ya Akili Mnemba (AI), hatua zinazolenga kuharakisha utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu, (SDG) namba 12.3.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya UNEP jijini Nairobi, Kenya, Meneja wa Miradi na Mtaalamu wa Maarifa wa shirika hilo, Michael Muratha, amesema kupunguza upotevu wa chakula ni muhimu katika kuimarisha uhakika wa chakula, kulinda mazingira na kuongeza kipato cha wakulima.
Teknolojia na miundombinu kuboresha uhifadhi
Muratha amesema takribani asilimia 13 ya chakula duniani hupotea baada ya mavuno na kabla hakijafika madukani. Barani Afrika, changamoto za uhifadhi, usafirishaji na upatikanaji wa masoko huchangia tatizo hilo.
Ametaja mfano wa ushirika wa wakulima 179 karibu na jiji la Nairobi, ambao ulikuwa ukipoteza hadi asilimia 40 ya mazao baada ya mavuno. “Kupitia uhifadhi wa baridi na usafirishaji wa vyakula kwa kutumia magari yenye majokofu endelevu, ushirika huo uliweza kuongeza kipato kwa asilimia 50,” amesema.
UNEP pia inaunga mkono mipango ya benki za chakula nchini Kenya, kwa ushirikiano na ubi awa Tabianchi na Hewa Safri au Climate and Clean Air Coalition, ili kuelekeza kwenye vituo vya elimu vya kulelea watoto au jamii zisizo na huduma za kutocha, chakula salama kilichozidi.
Akili Mnemba na ubunifu wa kupunguza taka
Katika sekta ya hoteli, zana za Akili Mnemba, (AI) zilizotumika katika mpango unaohusisha hoteli 13 zilisaidia kupima chakula kinachotupwa na kuboresha ununuzi pamoja na maandalizi.
Kwa mujibu wa Muratha, hatua hizo zilipunguza kwa asilimia 62 taka za chakula cha kifungua kinywa ndani ya miezi minne.
Ubunifu mwingine ni kutumia mabuu ya nzi askari mweusi kubadilisha taka za kikaboni kutoka masokoni kuwa chakula cha mifugo na mbolea, hivyo kupunguza taka na kufungua fursa za ajira.
Faida kwa mazingira na uchumi
Muratha amesema “kufikia SDG 12.3 kutapunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, ikiwemo methane, na shinikizo kwa ardhi na maji. Pia kutasaidia kupunguza hasara za kiuchumi zinazozidi dola trilioni moja kila mwaka kutokana na upotevu na utupaji wa chakula duniani.”
Amesisitiza kuwa kupunguza upotevu pekee hakutamaliza njaa, lakini ni hatua muhimu kuelekea mifumo ya chakula iliyo endelevu, salama na yenye ustahimilivu zaidi.