Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wenye ulemavu wapewe fursa sawa kwa uwezo wao na si kwa ulemavu wao: Mbunge Nassriya Ali

Wanawake wawili wamekaa kwenye benchi la bustani mjini, mmoja akizungumza kwa lugha ya ishara huku mwingine akisikiliza kwa makini.

Hii ni fursa pekee ambayo naweza kuitumia kuweza kuhimiza nchi yetu iweze kutekeleza vitu kama hivyo kama ambavyo nchi zingine zinatekeleza. Mfano na nchi zingine mpaka kuna taa maalumu kwa ajili ya taa za barabarani ambazo ni maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wanafahamu hivi sasa anavuka mtu mwenye ulemavu - Mbunge Nassriya Nassir Ali

UN News Nassriya Nassir Ali (kushoto), Mbunge wa watu wenye ulemavu kutoka nchini Tanzania ambaye naye ni mlemavu wa kusikia au kiziwi, akiwa na mkalimani wake wa lugha ya Alama Tusajigwe Ernest (kulia) katika mahojiano na UN News Kiswahili Jijini New York Marekani.

Watu wenye ulemavu wapewe fursa sawa kwa uwezo wao na si kwa ulemavu wao: Mbunge Nassriya Ali

Na Leah Mushi, UN News Kiswahili
Haki za binadamu

Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu CRPD ukiendelea jijini New York Marekani, mbunge wa watu wenye ulemavu kutoka nchini Tanzania Nassriya Nassir Ali ambaye naye ni mlemavu wa kusikia au kiziwi amesema wakati juhudi za kusaka usawa kwa watu wenye ulemavu zikiendelea ni vyema jamii ikaelewa kuwa wanachotaka watu wenye ulemavu ni fursa sawa kwa uwezo wao na si kwa ulemavu wao.

Akizungumza katika mahojiano na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akiwa na mkalimani wake wa lugha ya Alama Tusajigwe Ernest, mbunge Nassriya ameeleza yale ambayo nchi yake imetekeleza ikiwa huu ni mwaka wa 20 tangu kusainiwa kwa mkataba wa watu haki za watu wenye ulemavu ambapo Tanzania ni moja ya nchi zilizosaini mkataba huo. 

“Serikali ya Tanzania imefanya mambo makubwa kuweza kutekeleza huu mkataba. Nchi yetu imetekeleza kikamilifu kwenye eneo la elimu, afya, ajira lakini na mambo mengine ya kijamii.”

Wanawake wawili wamekaa kwenye benchi la bustani katika mazingira ya jiji, huku mmoja akiwa amevaa skafu yenye mandhari ya Kitanzania.
UN News Nassriya Nassir Ali (kushoto), Mbunge wa watu wenye ulemavu kutoka nchini Tanzania ambaye naye ni mlemavu wa kusikia au kiziwi, akiwa na mkalimani wake wa lugha ya Alama Tusajigwe Ernest (kulia) katika mahojiano na UN News Kiswahili Jijini New York Marekani.

Mbunge Nassari ameeleza mambo manne ambayo anatarajia katika mkutano huu wa CRPD 

1. Kujifunza kutoka kwa nchi mbalimbali namna walivyofanikiwa kutekeleza matakwa ya mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu.

2. Kukuza uelewa wa masuala ya Ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye sekta mbali mbali 

3. Kuona watu wenye ulemavu wanatambulika na kupewa fursa sawa kwa uwezo wao na si kwa ulemavu wao.

4. Dunia kuweza kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya Watu wenye ulemavu na kutambua kuwa Haki za watu wenye ulemavu ni Haki za Binadamu pia.

Maswali na majibu 

Leah: Tuzungumzie kuhusu miundombinu kwa mfano, vitimwendo. Je, ni maeneo yote yametekelezwa? Au bado kuna changamoto, na kwa watu wenye ulemavu wa kuona na yenyewe kuna njia zimetengenezwa au hali ikoje? 

Nassriya: Naweza kusema kwamba Tanzania imetekeleza kwa asilimia kadhaa. Ipo miundombinu ambayo ni rafiki kwa watu wenye ulemavu tofauti na hapo nyuma, wanajaribu kuwa jumuishi kuhakikisha kwamba kila mtu anaweza kufikia hayo majengo kwenye asilimia sabini hivi. Lakini pia kuhusiana na njia maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa uoni, wasioona. Kwa Tanzania bado hatujafikia, lakini nadhani hii ni fursa pekee ambayo naweza kuitumia kuweza kuhimiza nchi yetu iweze kutekeleza vitu kama hivyo kama ambavyo nchi zingine zinatekeleza. Mfano na nchi zingine mpaka kuna taa maalumu kwa ajili ya taa za barabarani ambazo ni maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wanafahamu hivi sasa anavuka mtu mwenye ulemavu. Kwa hiyo, vitu kama hivyo ni vya kujifunza na hii ndio fursa ambayo tunaitumia kwa ajili ya kujifunza kuhakikisha kwamba kila mwenye ulemavu anafikiwa iwe kwenye kitimwendo, asiyeona na kila aina ya ulemavu. 

Leah: Kuhusu kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika maeneo ya kisiasa, nchi mbalimbali zimeeleza changamoto bado ni kubwa, watu wenye ulemavu hawajumuishwi sana. Wewe ukiwa kama Mbunge unadhani uwakilishi wenu kwenye kwenye nafasi za siasa unatosha? 

Nassriya: Ni ukweli wamejadili masuala ya ujumuishaji. Zaidi sana niongelee kwenye upande wa siasa wa Tanzania. Kwa zamani hakukuwa na mwamko mzuri kuhusiana na watu wenye ulemavu kushiriki siasa. Muamko ulikuwa mdogo sana, lakini naweza kusema nashukuru Mungu baada ya kupata nafasi ya kuingia bungeni na nikiwa Mbunge wa kwanza mwenye ulemavu wa kusikia kwa maana ya kiziwi, nimeona kuna umuhimu wa kushirikisha watu wenye ulemavu kwenye nafasi kama hizi, nafasi za maamuzi. Zamani walikuwapo watu wenye ulemavu mbalimbali wanashiriki, lakini sasa hivi kwa mara ya kwanza Mbunge kiziwi ambaye ndio mimi naamini tunaendelea kujengea uwezo kwenye eneo la siasa, ndio kitu ambacho naweza kusema kifanyike. Tuendelee kuwajengea uwezo, kuwapa elimu kwamba na wao wanaweza kusimama kama watu wengine. Na naamini kuanzia kipindi hiki bado kuelekea huko mbele watu wenye ulemavu wataongezeka zaidi. 

Nassriya: Kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zamani wabunge wenye ulemavu walikuwa wachache karibia saba au sita hivi. Kwa maana hiyo tayari mwamko upo, na kama mimi ambapo unaniona na ulemavu wangu wa kusikia nikiwa kama kiziwi na uwezo wa kuchangia kuhoji. Zamani kulikuwa kuna kikwazo wakidhani kiziwi hawezi kuwasiliana, hawezi kuchangia, hawezi kusema lolote au akaleta mchango wenye maana. Lakini sasa hivi kumekuwa na mwamko wanakupa nafasi kama kiziwi wanakusikiliza na wanaona kweli kuna mantiki ya kuweza kujumuisha makundi yote ya wenye ulemavu ndio sababu tuna uwezo wa kusema chini ya Serikali ya Mama Samia kwa mara ya kwanza inaweza kuridhia kumpata mbunge mwenye aina ya ulemavu kwangu kwa maana ya kiziwi. Nashukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia kwa kutuamini.