WHO na wadau tunafanya kila liwezekanalo kudhibiti kusambaa kwa mlipuko huu wa Ebola: Profesa Janabi
WHO na wadau tunafanya kila liwezekanalo kudhibiti kusambaa kwa mlipuko huu wa Ebola: Profesa Janabi
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, limetangaza mlipuko wa sasa ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Uganda kuwa ni “Dharura ya Kimataifa ya Afya ya Umma”. Katika jimbo la Ituri mashariki mwa DRC, maafisa wa afya wameripoti hadi sasa wagonjwa wanawane waliothibitishwa maabara, wengine 246 wanoshukiwa pamoja na vifo 80 vinavyoshukiwa katika maeneo ya Bunia, Rwampara na Mongbwalu.
Wakati huo huo mjini Kampala nchini Uganda, wagonjwa wawili wa Ebola wamethibitishwa kikiwemo kifo kimoja na wagonjwa hao ni miongoni mwa wasafiri waliowasili kutoka DRC. Je hali ikoje sasa? Na WHO inafanya nini kusaidia? Flora Nducha ameyaelekeza maswali hayo wa Profesa Mohamed Yakub Janabi Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika
Mamlaka za afya kwa kushirikiana na taasisi zingine za Umoja wa Kimataifa tayari zina baini wagonjwa zinafuatilia watu waliokutana nao na zimeweka hatua za kudhibiti kusambaa kwa virusi - Profesa Janabi-WHO
Profesa Janabi: Kwanza ni habari za kweli kwamba kuna mlipuko wa Ebola katika nchi zetu hizi mbili. Na sisi kwa taratibu zetu tunasubiri nchi kwanza itangaze tatizo ili tuweze kuendana sawasawa kwa namba wanazo taja wao na namba tutakazo taja sisi ili tusichanganye wananchi zaidi. Naomba nianze kwanza kuwahakikishia watu. Ebola ni ugonjwa hatari lakini tunaujua na tunaweza kuudhibiti. Hii ni Ebola ya kumi na saba DRC. Mamlaka za afya kwa kushirikiana na taasisi zingine za Umoja wa Kimataifa tayari zina baini wagonjwa zinafuatilia watu waliokutana nao na zimeweka hatua za kudhibiti kusambaa kwa virusi.
Hivi ninapozungumza nawe kuna wafanyakazi wetu ishirini na tumechukua na wafanyakazi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ishirini. Kwa jumla kuna wafanyakazi arobaini tayari wapo huko leo na vile vile tumepeleka ndege moja leo ambayo ilikuwa na mizigo karibu zaidi ya tani tano ni tano na nukta sita ambayo itaweza kusaidia kwenye hatua za kweli. WHO imetangaza hali hii kama dharura ya afya ya umma ya kimataifa au PHEIC kwa Kiingereza. Hii ni ngazi ya juu kabisa ya tahadhari ya kimataifa. Inasaidia kuhamasisha rasilimali haraka na kuhakikisha nchi zinashirikiana kwa karibu. Lakini muhimu zaidi kusisitiza, hii si sababu ya hofu. Inaonesha tu kwamba mfumo wetu wa afya wa kimataifa unafanya kazi kwa sababu ni makubaliano ya nchi zote mia moja tisini na nne ambazo ni wanachama wa WHO. Muhimu ni kugundua mapema na kuchukua hatua za mapema.
UN News: Huu mlipuko ambao umetangazwa sasa wa virunsi vinavyojulikana kama Bundibugyo WHO inasema virusi hivi havina tiba wala havina chanjo. Sasa hii inaongeza hiyo hofu kwa kiasi gani sio tu kwa DRC na Uganda na Afrika kwa dunia kwa ujumla.?
Profesa Janabi: Ni kweli kama ilivyotangazwa na makao makuu ya WHO na kuna aina tatu kubwa zinazojulikana zaidi za virusi. Kuna hiyo ya Zaire kuna Sudan na hii ya Bundibugyo. Kwa sasa hivi hamna chanjo yenye leseni. Twaweza kusema au matibabu yaliyo mahususi kwa ajili ya ugonjwa wa virusi hivyo, lakini kuna virusi vingine vingi tuu bado havijapata chanjo. Lakini hapa naomba wananchi kuwatoa hofu katika kitu kimoja. Chanjo sio tiba pekee hata kwa yale magonjwa ambayo yana chanjo. Hapa kubwa sisi tunarudisha maji mwilini na kuhakikisha kwamba hamna upungufu wa maji na madini kwenye mwili. Wale ambao wana shida ya oksijeni tunatoa oksijeni kwa wale wenye matatizo ya presha, tunawapa msaada. Na kama kuna magonjwa mengine yote yanatokea kwamba tunawapa msaada, tunawaweka kwenye vyumba maalum vya ICU na hii hii yote inasaidia wagonjwa kwa kiasi kikubwa. Kwanza, tujue wamekutana na nani ili tu wawahi wale watu kabla hawajaanza kutoa dalili na vitu vingine tutoe. Tahadhari zingine ni mikusanyiko ya watu kama ilivyotokea kipindi cha COVID 19, kwa sababu hata COVID watu wote kama mnakumbuka haikupatikana chanjo siku ya kwanza tulipogundua iliharakishwa watu wakawekeza fedha nyingi za kutosha, makampuni binafsi yakaingia. Baadaye ikaja kupatikana chanjo hata kwa magonjwa ambayo yana chanjo ni kwamba kuna huduma zingine za dharura. Ni muhimu zaidi ambazo zinasaidia
UN News: Sasa tuangalie kwa hali ya Afrika yenyewe. Kama tunavyojua mipakani mara nyingi ndio kunachangia kusambaza milipuko ya magonjwa. Sasa nyie kama WHO mnafanyaje ili kuhakikisha kwamba mnafuatilia na hivi virusi hivisambai zaidi na hasa kupitia maeneo ya mipakani?.
Profesa Janabi: Mipakani, kipaumbele chetu kiko wazi kusimamisha mlipuko huu haraka kama tulivyofanya huko nyuma na na kulinda jamii. Ituri ni sehemu ambayo watu wanavuka sana kati ya mipaka kutoka kwenye jimbo hilo na kuelekea Uganda na Rwanda kwa sababu tofauti. Sisi kama shirika la afya la WHO upande wa Afrika tunafanya kazi bega kwa bega na hizi Serikali zote mbili. Mimi nimekuwa katika mawasiliano ya simu na mawaziri wa nchi zote mbili. Nimekuwa katika simu na watu wetu ambao wako pale na mashirika mengine ya afya pamoja na sisi jambo kubwa kwetu ni kubaini wagonjwa mapema na kuwahudumia haraka kupitia ufuatiliaji na uchunguzi makini. Pili, kuimarisha vituo vya matibabu na kulinda wahudumu wa afya ili wagonjwa wapate huduma salama kwa sababu sisi tunapeleka wahudumu wengi sana, tunao kama arobaini na mbili ni lazima tuhakikishe wanalala wapi, wanakaa wapi? Wana kinga gani. Kushirikiana na jamii kwa sababu uelewa na imani ni muhimu sana kudhibiti Ebola. Ndio maana nasema chanjo sio kitu pekee unaweza kuwa na chanjo, lakini jamii isipokubali haitakusaidia.
UN News: Itaongeza changamoto.
Profesa Janabi: Ndio na kuimarisha ushirikiano wa mipakani ili kuzuia kuenea zaidi ni muhimu. Pia tunashirikiana na washirika kote wa Afrika na wa dunia kuhakikisha nchi hizi zinapata vifaa, zinapata wataalamu na zinapata msaada unaohitajika.
UN News: Suala la ufadhili na hii ni kwa kimataifa. Mfumo wa afya umekuwa na ukata wa fedha. Hili unafikiri linaweza kuchochea ile hofu ya watu kuona kwamba sasa nchi zitashindwa kukabiliana na hii milipuko kwa sababu hakuna hela.
Profesa Janabi: Upungufu wa hela ni kweli ni mkubwa, umeathiri hata bajeti yetu sisi ya Shirika la Afya Duniani kwa asilimia kumi na tano. Lakini bora nikwambie kwamba viongozi wa Afrika wamebadilika kwa maana ya kutoa kipaumbele kwa afya. Bajeti zimebadilika na sasa hivi tu nimetoka kwenye mkutano na mawaziri wote wa Afrika arobaini na saba tayari kujitayarisha na World Health Assembly ni kwamba vipaumbele kwenye afya vimekuwa vikubwa. Hii ya fedha za ndani yaani uwekezaji wa ndani umeongezeka. Ushirikiano kati ya mashirika binafsi na serikali umeongezeka. Tunaendelea kujenga imani kwa washirika wetu kama Gates Foundation na wengine na wote katika bara hili. Sasa hivi lugha ni moja kwamba tunatakiwa kuongeza bajeti zetu za afya.
UN News: Mwisho kabisa, kwa wale ambao tayari wameshapitia milipuko ile, hofu waliyo nayo. Unapenda kuwaeleza nini hasa kuwa na imani kwamba huu nao ni mlipuko wataushinda pia?
Profesa Janabi: Ujumbe ni kwamba hali hii wote sisi na serikali zote mbili tunaichukulia kwa uzito mkubwa. Lakini inadhibitiwa kikamilifu kwa ushirikiano madhubuti, uangalizi wa karibu na ushiriki wa jamii. Tuna imani kwamba tutadhibiti mlipuko huu, muhimu ni kutoa tahadhari mapema kwa jamii kutoa tahadhari mapema unapomwona mtu ana homa na shida ya kupumua na ana uchovu usioeleweka. Ndio maana mimi nina uhakika mkubwa mlipuko huu tutaweza kuudhibiti.