Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunatoka nje ya mahakama na kufuata wananchi kuwaelimisha – TAWJA

Mwanamke aliyevaa hijabu na mshipi wenye rangi za bendera ya Tanzania akizungumza kwenye kipaza sauti katika tukio la Umoja wa Mataifa.
UN News Barke Sehel, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Majaji, (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa nchini Tanzania.

Tunatoka nje ya mahakama na kufuata wananchi kuwaelimisha – TAWJA

Wanawake

Upatikanaji wa haki hususan kwa wanawake na wasichana hukumbwa na vikwazo lukuki ikiwemo ukosefu wa uelewa wa haki zenyewe. Nchini Tanzania Chama cha Wanawake Majaji, (TAWJA) kimetambua pengo hilo na ndio maana tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 kimekuwa kinachukua hatua kuhakikisha kwamba kabla ya kusaka haki, wanawake na wasichana wanatambua haki zao. Kufahamu nini kinafanyika, Assumpta Massoi wa Idhaa hii mwezi Machi mwaka huu kando ya mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70 hapa Umoja wa Mataifa, alizungumza na Mwenyekiti wa TAWJA, Barke Sehel ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Jaji Barke Sehel : Tulifanya mkutano pale Dodoma na kauli mbiu ya mkutano ule ilikuwa ni Majaji kutoka nje ya kuta za mahakama. Ndicho ambacho TAWJA tunafanya, tunatoka nje tunawafuata wananchi kwenda kuwapa elimu. Sisi sana sana tunajihusisha na kutoa elimu ili mtu afahamu haki yake si tu kutoa elimu kwa wananchi pia kukuza vipaji vya wanachama wetu wachanga ili nao waweze kujiona kwamba siku moja na yeye wanaweza akafika hapo sisi ambapo tupo na baadaye waje kuwa viongozi bora zaidi. Kwa hiyo huwa tunawafuata wananchi. Tunaweza tukawa tunaenda kwenye masoko, Tunaenda kwenye vituo vya mabasi, huwa tunaenda hospitali, tunaenda magerezani, shuleni, vyuoni na tunatumia redio na televisheni. Na mikoa mingi na ina redio zao kwa hiyo TAWJA imesambaa mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar. Kwa hiyo, kama kuna redio huko Katavi wanachama wa Katavi watakuja kule wanaenda kwenye ile redio ya kule Katavi kutoa elimu. Kwa hiyo huwa tunafanya hivi hatujifungii tu ndani ya kuta za mahakama tukiandika tu kwamba ndio mtu akisoma hukumu watajifunza hapana tunatoka nje.

Kauli mbiu yetu ilikuwa kutoka nje ya kuta za mahakama. Kwa hiyo huwa tunawafuata wananchi. Tunaweza tukawa tunaenda kwenye masoko, kwenye vituo vya mabasi, huwa tunaenda hospitalini, tunaenda magerezani, shuleni, vyuoni na tunatumia redio na televisheni. - Jaji Barke Sehel – Mwenyekiti TAWJA

Idhaa ya UN: Hapo tulivyozungumza hilo limenijia suala la sheria ya ndoa ninyi kama majaji na mahakimu, sheria ya ndoa, ile ya mwaka 1971 ndiyo inamuweka mtoto wa kike katika kushindwa kupata haki zake za msingi. Haki ya kuendelea; haki ya kushirikishwa; haki ya Elim una haki ya Afya. TAWJA mnasemaje?

Jaji Barke Sehel: Kwa upande wa mahakama tulishatoa uamuzi kuhusiana na mtoto kuolewa chini ya umri miaka 18. Kama ulishasikia kesi ya Rebeca Gyumi,  sasa ile kwa upande wa mahakama ilitoa uamuzi kwamba Serikali ijaribu kuangalia jinsi ya kubadilisha sheria. Tunafahamu kwamba Serikali iko kwenye mchakato wa kulifanyia kazi. Kwa hiyo, tutegemee kwamba litafanyiwa kazi. 

Idhaa ya UN: Tunaangalia kwa mfano, masuala ya kesi za ukatili wa kijinsia. Mara nyingi huhitaji uelewa wa kina na mwitikio madhubuti wa kisheria. Sasa majaji wanawake mna nafasi gani hasa katika kuimarisha mwitikio wa mahakama dhidi ya ukatili wa kijinsia, kuhakikisha kwamba manusura wanapata haki kwa usawa na kwa wakati.?

Jaji Barke Sehel: Tunatoa elimu kwamba ukipatwa na janga ufanye nini ukiripoti wapi na ukisha ripoti nini cha kufanya na kesi zikija tunaamua kwa haki kwa sababu jukumu letu sisi ni kusikiliza pande zote mbili. 

Idhaa ya UN: Kwa hiyo, huko kwenye mahakama mnaangalia haki kwenye TAWJA, mnatoa elimu. Tumezungumzia kwamba idadi ya wanawake, majaji na mahakimu inaongezeka. Tungependa kujua kwa mfano, tunapozungumzia kuongezeka ni kwa kiasi gani?

Jaji Barke Sehel: Kulikuwa hamna jaji hata mmoja wa kike kwenye Mahakama ya Juu kabisa, yaani Mahakama ya Rufaa wakati TAWJA inaanzishwa mwezi wa Mei mwaka 2000  kulikuwa hamna kabisa. Kulikuweko majaji wa kiume wote na walikuwa tisa. Baada ya TAWJA kuanzishwa na nafikiri hiyo ndio ilikuwa ni jukwaa zuri. Jukwaa zuri ambalo lilionesha umma kwamba kuna majaji wa kike hapa hawako wanaume peke yao kwa jukwaa lile. Nafikiri ndio lilipelekea mwanzilishi wa chama chetu, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mstaafu mwezi wa Agosti mwaka 2000 akateuliwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa. 

Sasa hivi tuko 12 kati ya majaji 38. Tulikuwa 13, mmoja amestaafu. Utaona ni hatua gani ambayo tumepiga. Na mahakimu ni wengi sana ukichukulia hasa kwenye mahakama za chini. Karibu nusu nusu na nyingine kama za mwanzo, nafikiri wanawake kama ni hamsini. Na Mahakama Kuu. wako 39. Jumla ya majaji ni105 na kuna kwenye mahakama zetu kuna wale tunawaita majaji wafawidhi ambao wanaongoza vituo kwenye kanda. Pia nako wanawake na ni wengi tu. 

Idhaa ya UN: Je, idadi kubwa imetafsiri pia katika kupatikana kwa haki sawa?

Jaji Barke Sehel: Ndio imesaidia. Unajua huwa tunakuja na fikra tofauti na wanaume. Kwa hiyo tunapoingia na sisi kwenye huo mfumo na sisi tunachangia na mawazo yetu pia. Kwahiyo kwenye kutoa haki nako kunakuwa sasa na fikra za upande wake name. Kwa hiyo imesaidia kwa namna fulani na pia imesaidia kwa mtazamo kwa wananchi kwamba akija mahakamani  mwanamke akikuta mwanamke mwenzake anapata faraja zaidi au itasikilizwa kuliko labda akienda kwa mwanaume atakuwa anaogopa. 

Idhaa ya UN: Katika suala la utoaji wa haki za wanawake na watoto, mnapenda kuona nini? 

Jaji Barke Sehel: Tunapenda kuwe na amani na wote tuwe sawa tu. Mwanamke athaminiwe kwa hali na utu wake ambao anao kama anavyothaminiwa mwanaume wa mtoto wa kiume. Hii ndio ndoto yetu. Unaweza kufuatilia kwenye mitandao yetu TAWJA na tuko kwenye Instagram na pia tuko kwenye Facebook mtaona kazi mbalimbali ambazo TAWJA inafanya.