Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa yaondokane na mila potofu ili wanawake na wasichana wawe huru - Salome Gatakaa 

Mwanamke Mkenya amevaa mavazi ya Kiafrika yenye rangi na miwani, akizungumza katika mazingira ya ofisi.
UN News Salome Gatakaa Araka wa FODDAJ ambalo ni Jukwaa la Maendeleo ya Wanawake, Demokrasia na Haki, nchini Kenya ni shirika la kiraia nchini Kenya.

Mataifa yaondokane na mila potofu ili wanawake na wasichana wawe huru - Salome Gatakaa 

Na Assumpta Massoi, UN News Kiswahili
Wanawake

FODDAJ ambalo ni Jukwaa la Maendeleo ya Wanawake, Demokrasia na Haki, nchini Kenya ni shirika la kiraia ambalo mwaka huu kwa mara nyingine lilishiriki mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani CSW70 uliofanyika mwezi Machi mwaka huu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Baada ya kushriki vikao mmoja wa viongozi wa shirika hilo amezungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na ndio msingi wa mahojiano haya.

FODDAJ inajinasibu kuwa imekuwa sehemu ya harakati za mchakato wa rasimu ya sera ya kukabiliana na ukatili au dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana nchini Kenya.

“Kwa sasa tunasubiri ipitishwe ili iwe sheria kwani muswada huu ni wa kusimamia waathirika ili waweze kusikika,  haki zao ziweze kuzingatiwa kokote kule waliko,” amesema Bi. Arakaa.

Mathalani manusura wa ukatili afahamu kuwa anatakiwa kwenda kuripoti polisi ili haki yake iweze kuzingatiwa.

Alipoulizwa alichokipata CSW70, mwakilishi huyu wa FODDAJ ameweka bayana kuwa wakati wa mashauriano wamejifunza kuhusu mambo mbali mbali kutoka kwawashiriki wengine lakini kile alichojifunza ni kwamba, “kama mashirika ya kiraia ni lazima tuhakikishe wanawake waathiriwa wa dhuluma wanapata haki zao. Kwa hiyo ili waweze kupata haki zoa ni lazima tuendelee kuwaelimisha sana.”

Amesema iwapo mwanamke au mama ataelimika basi atafahamu kuwa kama atakumbwa na dhuluma anahitaji kwenda kuripoti polisi.

“Ataweza kujisaidia yeye mwenyewe na atapata haki yake,” amesema Bi. Arakaa akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Kuhusu ushirikiano na serikali ya Kenya, Afisa huyu wa FODDAJ amesema ni uko bayana kwani hata kwenye CSW70 Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Masuala ya Jinsia alieleza bayana umuhimu wa kuondolewa kwa vikwazo vya kitamaduni.

Alisema kuwa vikwazo vya kiutamaduni lazima vivunjwe ili wanawake na akina mama waweza kuwa huru. Na hii pia akasema ya kwamba tunahitaji kuhusisha na wanaume katika hili suala ili waweze kutumika kwa kuongea na wanaume wenzao waweze kuachana na hizi tamaduni ambazo zinadhuru wanawake,” amesema Bi. Arakaa akimnukuu Katibu Mkuu.

Amesema “serikali yetu inahusika katika kufanikisha mapambano ya dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana. Inapatia kipaumbele kwa kusema kuwa lazima akinamama waelimishwe na watu wale wanaohusika katika hili jambo ili tuweze kuvunja hizo dhuluma.”