Kubadili mtazamo wa jamii ya Samburu kuhusu haki za wanawake ni mtihani tunaoukabili kila siku: Lemachokoti
Kubadili mtazamo wa jamii ya Samburu kuhusu haki za wanawake ni mtihani tunaoukabili kila siku: Lemachokoti
Kwa wanawake na wasichana wa jamii ya Kaunti ya Samburu Kaskazini mwa Kenya kutorithi chochote katika jamii imekuwa kama ada, kwani mila na utamaduni uliokita mizizi miaka nenda miaka rudi ni chachu kubwa ya kuwakosesha haki. Sasa mambo yameanza kubadilika ingawa changamoto hazikosekani kama anavyoeleza Severina Lemachokoti kutoka asasi ya kiraia ya Naretu Girls and Women Empowerment Programme katika kaunti hiyo, alipozungumza na Flora Nducha wa Idhaa hii kandoni mwa mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani CSW70 uliokunja jamvi mwezi uliopita. Severina naanza kwa kufafanua wanachofanya kuhakikisha wanawake na wasichana Samburu wanapata haki.
Severina: Katika kaunti ya Samburu tunafanya kazi mbalimbali kuhakikisha tunahamasisha wasichana, wanawake na jamii nzima kuhusu haki zao. Tunajua Kenya ina sheria ambazo zinapaswa kutekelezwa hadi mashinani. Katika shirika letu tunahakikisha tunawaelimisha wasichana na kina mama kwamba wana haki sawa, ikiwemo haki ya elimu, kumiliki mali na kurithi ardhi. Pia tunapambana na changamoto za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana ambazo mara nyingi husababishwa na mila na desturi zilizokita mizizi katika jamii. Tunatumia lugha ya Kisamburu kufikisha ujumbe wetu na tunashirikisha wazee pamoja na vijana kwa sababu katika jamii yetu mwanamke au msichana mara nyingi haruhusiwi kuzungumza mbele ya watu.
UN News: Mnafanyaje kuhakikisha jamii, hasa wanaume, wanaelewa umuhimu wa haki za wanawake na wasichana?
Severina: Ni kazi ngumu na inahitaji uvumilivu mkubwa. Tunaanza kwa kutambua viongozi wa jamii na kuwashirikisha katika mazungumzo. Tunatumia vijana walio katika nafasi za uongozi kutusaidia kufikia jamii na kuzungumza na wanawake kuhusu haki zao. Pia tunashirikiana na wazee wa kanisa ambao sasa wameanza kutuunga mkono katika kuhakikisha haki za wasichana zinazingatiwa. Aidha, tunatafsiri sheria zinazohusu haki za watoto na wanawake kwa lugha ya Kisamburu ili jamii iweze kuelewa vizuri zaidi.
UN News: Changamoto kubwa mnazokutana nazo ni zipi?
Severina: Changamoto ni nyingi. Kwanza ni kiwango kidogo cha elimu katika jamii ya Wasamburu, hasa kwa wale tunaotegemea kusaidia kusimamia utekelezaji wa sheria mashinani. Pia kuna mila na desturi ambazo bado zinazuia mabadiliko. Kwa mfano, ni vigumu kwa baba wa Kisamburu kumpatia msichana ardhi au mali kama ng’ombe wakati wa kugawa urithi. Pia bado kuna mtazamo kuwa msichana anapaswa kubaki nyumbani na kuolewa badala ya kwenda shule. Hata hivyo, mambo yanaanza kubadilika polepole kutokana na elimu na juhudi za serikali kuhakikisha watoto wote wanapata haki ya kwenda shule. Tunashirikiana pia na polisi, maafisa wa watoto na maafisa wa probation kusaidia kulinda haki za watoto.
UN News: Je, jamii imeanza kubadilika mtazamo kuhusu haki za wasichana na wanawake?
Severina: Polepole jamii inaanza kuelewa. Tumeshuhudia kupungua kwa ukeketaji wa wasichana na ndoa za utotoni. Hii inasaidia kwa sababu wasichana wengi sasa wanaenda shule. Mimi mwenyewe nilikuwa mwalimu na nimeona wasichana wengi ambao hawakukeketwa wakifaulu hadi vyuo vikuu na kurejea Samburu kufanya kazi. Wasichana hao sasa wamekuwa mfano mzuri kwa jamii. Wazee wanaona kuwa mtoto wa kike pia anaweza kusoma, kufanikiwa na kusaidia familia kama mtoto wa kiume. Tunatumia pia wasichana walioelimika kuwashauri na kuwahamasisha wengine.
UN News: Ushirikiano wenu na serikali ukoje katika kuhakikisha sheria zinatekelezwa?
Severina: Naweza kusema ni asilimia hamsini kwa hamsini. Kuna changamoto nyingi, ikiwemo rushwa na ukosefu wa usalama. Wakati mwingine maafisa wa serikali wanaogopa kufika mashinani kwa sababu ya ukosefu wa amani na hofu ya kushambuliwa.
Bado ni vigumu kwa jamii kuacha mila kwa sababu wengi wanaamini “mwacha mila ni mtumwa.” Tunahitaji ushirikiano mkubwa kati ya serikali, mashirika ya kijamii na jamii yenyewe. Lazima tuhakikishe watoto wanapata elimu, huduma za afya, barabara nzuri na mazingira salama. Tukifanya hivyo, wazazi wataona manufaa ya kuwapeleka watoto wao shule badala ya kushikilia mila potofu. - Severina Lemachokoti
Pia kesi nyingi za watoto zinashindwa kuendelea mahakamani kwa sababu jamii hukataa kutoa ushahidi. Tunahitaji serikali kuwapa mafunzo zaidi maafisa wanaotumwa mashinani kuhusu sheria za watoto ili waelewe wajibu wao na wasiangalie vitendo vya ukatili kama sehemu ya mila za kawaida.
UN News: Unaamini nini kifanyike ili kusaidia zaidi wanawake na wasichana katika jamii ya Wasamburu?
Severina: Kitu kikubwa ni elimu. Serikali ya Kenya ilipitisha sheria dhidi ya ukeketaji mwaka 2011, na juhudi hizo zimeanza kusaidia kupunguza tatizo hilo. Lakini bado ni vigumu kwa jamii kuacha mila kwa sababu wengi wanaamini “mwacha mila ni mtumwa.” Tunahitaji ushirikiano mkubwa kati ya serikali, mashirika ya kijamii na jamii yenyewe. Lazima tuhakikishe watoto wanapata elimu, huduma za afya, barabara nzuri na mazingira salama. Tukifanya hivyo, wazazi wataona manufaa ya kuwapeleka watoto wao shule badala ya kushikilia mila potofu. Pia tunahitaji programu za kuwawezesha wanawake na vijana kuona kuwa maendeleo yanawezekana hata katika maeneo ya vijijini kama Samburu.
UN News: Ujumbe wako wa mwisho kwa dunia kuhusu jamii ya Wasamburu na haki za wanawake ni upi?
Severina: Ningependa kusema tushirikiane na tufanye kazi pamoja, kwa sababu kidole kimoja hakivunji chawa. Tuunganishe nguvu zetu kuhakikisha watoto wa kike na wanawake wanapewa nafasi katika elimu na haki zao zinazingatiwa. Tukifanya hivyo, jamii zetu zinaweza kusonga mbele na kuwa na maendeleo ya kweli.